Teknolojia ya kilimo bila kutumia udongo, mwanga wakulima mbogamboga

Makanyaga

JF-Expert Member
Joined
Sep 28, 2007
Posts
11,129
Reaction score
7,321
Pale teknolojia inapokuja na uvumbuzi mpya, wanasayansi na waendelezaji wa teknolojia mpya huingia kazini wakitafuta namna nzuri ya kuiboresha zaidi, ili kuyafanya maisha ya watu yalete matumaini.

Kwa miongo mingi ya dunia ya uvumbuzi na ubunifu, hakuna shaka kwamba kila kunapokuwa na uvumbuzi mpya, faida kubwa imeonekana takriban katika nyanja zote na hivyo kunufaisha jamii, taifa na dunia kwa ujumla wake.

Kuna faida nyingi za teknolojia na uvumbuzi kwenye sekta mbalimbali ikiwamo ya uchumi, kama vile kuongeza faida kazini, kwenye biashara na tija katika uzalishaji.

Teknolojia inahitajika sana kwenye sekta ya kilimo ambayo kiuchumi inaajiri idadi kubwa ya Watanzania, takribani asilimia 70, wengi wakiishi vijijini.

Uvumbuzi katika sekta hii muhimu kiuchumi duniani na Tanzania kwa maana hiyo unatajwa kuwa hatua muhimu ya kuondoa baa la njaa.

Ukichukua taifa la Marekani kwa mfano, kwa mujibu wa Idara ya Kilimo ya taifa hilo, mkulima mmoja wa kawaida kwa hivi sasa analisha watu 155, ikiwa ni hatua kubwa ikilinganishwa na miaka ya 1960, ambapo aliweza kulisha watu wawili tu.

Mafanikio hayo yametokana na maendeleo makubwa ya teknolojia na uvumbuzi katika sekta hiyo.

Kumekuwa na maendeleo makubwa katika teknolojia ya mbegu bora, vifaa vya kilimo, matumizi sahihi ya ardhi na maeneo mengine ambayo yanaruhusu mashamba kuzalisha kwa tija na kwa ufanisi.

Kwamba teknolojia imewezesha wakulima kuwa na tija katika kilimo chao, wakitumia vilevile rasilimali katika kiwango cha kukubalika.

Hata hivyo, bado kuna changamoto mbalimbali kwenye sekta ya kilimo, zikiwamo migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji, changamoto ya kuwa na teknolojia za kuwakwamua wakulima ili watoe mchango katika suala zima la uhakika wa usalama wa chakula nchini na kujiwezesha kimapato.

Ndiyo maana kunapokuwa na uvumbuzi wowote wenye lengo la kuwanyanyua wakulima, ni vizuri ukiungwa mkono kwa faida yao.
Sasa mojawapo ya wadau waliokuja na uvumbuzi mpya katika sekta ya kilimo nchini ni Kampuni ya Green Fish Investment.

Kampuni hii imeingiza teknolojia ya kilimo bila kutumia udongo kwenye uzalishaji wa mbogamboga pamoja na mimea mingine samaki.

Kafyome anasema wao wamekuja na teknolojia hiyo ambayo inatumia kokoto ama unga wa kifuu cha nazi kuotesha mbogamboga badala ya udongo na kwamba kwa hivi sasa wana mashamba ya aina mbalimbali kwa ajili ya kuotesha mboga za aina tofauti.

"Huwa tunavisaga vifuu vya nazi na ule unga wake ndiyo tunaoutumia kuoteshea mbogamboga,” anasema na kuongeza:

“Faida zake ni nyingi, kubwa zaidi ni kwamba ukitumia unga wa vifuu vya nazi kuoteshea mbogamboga, zaidi ya asilimia 95 ya miche inaota, tofauti na ilivyo kwenye udongo ambapo ni asilimia 30 hadi 40 tu ya miche inayoota… tatizo ni kwamba watu hawajui kama kifuu cha nazi kinaweza kutumika katika matumizi ya kilimo.”

MBOGA ZINAZOTAMBAA

Kwa upande wa mashamba yaliyo na mboga zinazotambaa kama maboga na nyanya, Kafyome anasema mboga hizo wameziotesha katika ndoo ambazo ndani yake wameweka kokoto pamoja na maji.

“Boga likianza kutambaa,litapanda juu na hata hizi nyanya zitapanda juu kutokana na hizi kamba tulizoziweka,” anasema.

MAJI

Ofisa huyo anabainisha kwamba katika uvumbuzi wao wameshughulikia suala la hitaji la maji kwenye mashamba hayo ili yawe na uwezo wa kujimwagilia yenyewe.

Anasema wanafunga kifaa ambacho kinaeleza shamba limwagiliwe baada ya muda gani, na muda unapofika mazao hupata maji mara moja na moja kwa moja.

“Hata kama umeme umekatika muda haubadiliki, utabaki kuwa pale pale muda wa shamba kumwagiliwa… maji yataanza kutoka kwa muda uliopangwa,” anasema.

FAIDA

Mtaalam huyo anasema kuna faidi nyingi ya kutumia teknolojia hiyo ya maji na mojawapo ya faida hizo ni kwamba maji huwa hayapotei.

“Maji uliyoanza kupandia, ndiyo hayo hayo yatatumika hadi kuvunia,”anasema.

Kafyome anataja aina ya mboga wanazoziotesha kwa wingi katika mashamba yao kuwa ni mmea wa spinachi.

KWA NINI UDONGO SI CHAGUO

Ofisa huyo anasema kwa kawaida mmea huhitaji mambo manne ambayo ni kishikio, maji, mbolea na mwanga.

Anabainisha kwamba udongo hutoa vitu vitatu ambavyo ni maji, chakula na kishikio cha mmea.

“Ukiangalia mimea yetu utaona haijashikwa na udongo… hiyo inaonyesha kwamba si lazima mmea ushikwe na udongo,” anasema na kuongeza:

“Kama mmea unahitaji chakula, tunaweka mbolea katika maji na kama mmea unahitaji mwanga, hili eneo lina mwanga na maji tayari tumeshayaweka katika mimea wetu,” anasema.

CHANGAMOTO YA UDONGO

Kafyome anasema teknolojia hii waliyokuja nayo kimsingi ina faida nyingi, ikiwemo ile ya kuiepusha mimea dhidi ya magonjwa.

Anabainisha kwamba udongo ni chanzo kikubwa cha magonjwa katika mimea na ndio maana watu wengi wanahangaika katika kilimo cha mbogamboga kupambana na magonjwa.

Kwamba muda mwingi wanautumia kupulizia dawa mbogamboga ili kuzikinga na magonjwa kwa sababu udongo unasababisha magonjwa katika mimea.

KARATASI ZA NJANO

Ofisa huyo anabainisha kwamba njia wanayoitumia kuua wadudu kwenye mashamba yao ni nzuri kwa afya na haisababishi maradhi ya kiafya.

Anasema tofauti na ilivyo kwenye udongo ambapo njia ya kupulizia hutumika, katika uvumbuzi huu karatasi za njano ndizo zinazotumika ambapo zimewekwa maalum kwa ajili ya kunasa wadudu watakaoingia katika shamba.

“Tumeweka hizi karatasi za njano ambazo zitamvuta mdudu kuja katika karatasi hizo na anapofika ananaswa, hivyo shamba lako litakuwa safi, lisilo na wadudu,” anasema.

UKAGUZI

Kafyome anasema aina hii ya mashamba yasiyotumia udongo, mkulima ana uwezo wa kuyakagua kwa ukaribu kila siku ikilinganishwa na mashamba ya udongo.

“Ni muhimu wananchi wengi sasa wakajua uwapo wa teknolojia hii ambayo ni rahisi na pia inatumia gharama nafuu na mazao yanakuwa salama,”anasema.

KWA NINI UVUMBUZI HUU

Ofisa huyu anabainisha kwamba kampuni yake imekuja na teknolojia hii ya kulima bila udongo ili kukifanya kilimo kuwa cha kisasa zaidi na kuwaongezea wakulima tija katika uzalishaji wao na hivyo ustawi na maendeleo ya taifa kwa ujumla.

Anabainisha kuwa teknolojia hiyo imepunguza kwa zaidi ya asilimia 50 ya usumbufu na changamoto nyingi zilizomo katika kilimo cha kawaida au cha mazoea.

"Teknolojia hii inaongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo kwa kutumia maeneo madogo, kufanyika kwa uzalishaji mkubwa zaidi ya yule anayefanya kilimo kwenye udongo,” anasema na kuongeza:

“Mashamba yapo ya aina tofauti, kwanza shamba lenye ukubwa wa mita moja ya mraba linalobeba miche 200, ambapo kwenye udongo kungetumika eneo lisilopungua mita 6-8 (Growing tower).”

Aidha, anasema kuna shamba linalolimwa kwenye eneo la mita moja kwa kwa mita tatu na kupandwa miche 90 ambapo kama ingekuwa kwenye udongo mkulima angetumia mita zisizopungua 5-6 (Floating raft).

Kafyome anasema wananchi wanaweza kunufaika na kilimo hicho kwani kitawasaidia kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo, hususani mboga na pia kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira kwa wananchi wengi, hususani vijana.

MIGOGORO YA ARDHI

Faida nyingine anayoitaja ni ile ya kuondokana na migogoro ya ardhi ambapo wananchi watatumia maeneo madogo kufanya kilimo na kuzalisha kwa wingi.

“Aidha, kilimo cha aina hii hupunguza gharama za uwekezaji na uendeshaji kwa kuwa kwa sehemu kubwa hakitegemei upulizaji wa dawa ili kupambana na magonjwa shambani,”anasema.

Kafyome anasema kwa namna teknolojia hii walivyoiweka huzuia wadudu kuingia katika shamba na mbogamboga huwa salama.
 
Tatizo kubwa la wabongo ndiyo hili....unaleta taarifa nzuri sasa tutaifanyiaje kazi kama hakuna contacts nk?...au maelezo ya unataka tufanye nii baada ya hapa?
 
Habari kama hizi ingependeza mtaalamu wa kilimo ahoji na kuandika, bila hivyo mambo muhimu ya kitaalam yanakosekana
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…