Date::11/16/2008
Zamu ya vigogo wa EPA kupanda mahakamani yakaribia
*Wamo mawaziri,wafanyabiashara wazito zaidi
Na Ramadhan Semtawa
Mwananchi
BAADA ya Mkurugenzi wa Mashitaka ya Umma (DPP), kusema bado kuna upelelezi zaidi kwa baadhi ya majalada ya watuhumiwa wa ufisadi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) iliyokuwa Benki Kuu (BoT), baadhi ya majina ya vigogo likiwemo la mmoja wa waliokuwa mawaziri wa wizara nyeti wa serikali iliyopita, yanatajwa kuwa katika orodha ya watu wanaoweza kufikishwa mahakamani wakati wowote.
Kutajwa kwa majina ya vigogo hao (tunayo) pamoja na waziri huyo, ambaye pia alitumikia serikali iliyopo kabla ya baraza la mawaziri kuvunjwa Aprili, kumekuja wakati kukiwa na taarifa za uhakika kutoka duru huru za kiserikali kwamba, Rais Jakaya Kikwete, ameachia vyombo vya dola vifanye kazi zake kwa uhuru.
Habari hizo za kuaminika kutoka serikalini zinasema uamuzi huo wa rais kuachia vyombo hivyo vifanye kazi zake kwa uhuru, umevipa nguvu za kuweza kuandaa baadhi ya taratibu za kushughulikia vigogo hao wa EPA na wengine wa ufisadi tofauti nchini.
Alipoulizwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishina Robert Manumba, kuhusu kukamilika upelelezi kwa baadhi ya majalada aliyoagiza, DPP, alijibu: "Nafikiri si vizuri sana kuanza kuelezea kwa kina na hadharani kuhusu taratibu za upelelezi."
Kamishina Manumba alisema upelelezi huo unafanywa na timu, hivyo si sahihi kuanza kuamka na kueleza mipango mbalimbali akasisitiza kwa kusema: "Nafikiri subiri tu, kila kitu kitafahamika na DPP ataweka wazi."
DCI Manumba aliongeza kwamba iwapo upelelezi utaanza kuelezwa kwa uwazi ni dhahiri utavurugika na akazidi kusihi akisema:"Tusubiri, maana hii ni kazi ya timu."
Wakati Kamishina Manumba akisema hilo, duru za kiserikali zilisema mmoja wa watu waliowahi kushika wadhifa wa katibu mkuu kwenye wizara moja na pia cheo katika ofisi ya waziri mkuu, anatajwa kuwa ni miongoni mwa watuhumiwa wa ufisadi ambao wanashughulikiwa kwa kujihusisha na kampuni ya Meremeta.
"Kwa sasa, bwana mkubwa (Rais) ameachia vyombo vifanye kazi zake kwa uhuru; amesema hataki kuviingilia, ndiyo maana ndugu yetu (huyo waziri wa zamani) na wenzake anaweza kufikishwa mahakamani wakati wowote," kilisema chanzo hicho cha kuaminika na kuongeza.
Kwa mujibu wa duru hizo, ndani ya orodha hiyo ya vigogo, wamo pia wafanyabiashara maarufu nchini ambao wanatajwa kwamba wanaweza kupanda kizimbani wakati wowote upelelezi ukikamilika na DPP akijiridhisha kwamba kuna ushahidi wa kesi.
Duru hizo za habari za kiserikali zilifafanua zaidi kuwa tayari waziri huyo wa zamani amekwishajua mchakato unavyoendelea na kwamba katika siku za karibuni ameamua kuwa kimya.
"Siku hizi amekuwa kimya... anajua kinachoendelea, labda apate msamaha wa bwana mkubwa (Rais) kabla ya kufikishwa mahakamani akienda kumuomba amsamehe, lakini hadi sasa ana wakati mgumu ndiyo maana yuko kimya," kilifafanua chanzo hicho.
"Hivi sasa watu wana wasiwasi... kwa mfano, ndugu yetu (jina tunalo) naye anatajwa katika kashfa ya Meremeta kipindi akiwa katibu mkuu wizara..."
"Bwana mkubwa hatabiriki, amechoka kuona anabebeshwa mizigo ambayo si yake. Sasa anataka kuonyesha wananchi kwamba yuko makini."
Hadi sasa tuhuma zinazotajwa kuwa zinaweza kufikisha vigogo mahakamani kwa nyakati tofauti ni pamoja na wizi wa fedha za EPA, kashfa ya utoaji zabuni ya ufuaji umeme wa dharura kwa Kampuni Richmond na sakata la Meremeta.
Lakini wengi wanasubiri kuona vigogo wanaotajwa kuhusika kwenye kashfa ya EPA wakipandishwa kizimbani baada ya Jeetu Patel pekee kuonekana kuwa ndiye kigogo miongoni mwa watuhumiwa 20 ambao wameshafikishwa mahakamani hadi sasa.
Ufisadi huo wa fedha za EPA ulibainika katika hesabu za BoT za mwaka 2005/06, baada ya Kampuni ya Deloitte&Touche ya Afrika Kusini kubaini ufisadi wa Sh40 bilioni zinazodaiwa kuchotwa na Kampuni ya Kagoda Agriculture Limited, lakini kampuni hiyo ya ukaguzi ikazuiwa kuendelea na kazi.
Hata hivyo, mwaka jana serikali ilimwagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kutafuta kampuni nyingine ya kimataifa, kufanya ukaguzi huo kubaini ukweli.
Ofisi ya CAG iliteua Kampuni ya kimataifa ya Ernst&Young, ambayo ilibaini ufisadi wa zaidi ya sh 133 bilioni, ambazo zilichotwa na makampuni 22.
Makampuni 13 yalijichotea Sh 90.3 bilioni, ni pamoja na Bencon International LTD of Tanzania, Vb & Associates LTD of Tanzania, Bina Resorts LTD of Tanzania, Venus Hotel LTD of Tanzania, Njake Hotel &Tours LTD, Maltan Mining LTD of Tanzania.
Mengine ni Money Planners & Consultants, Bora Hotels & Apartment LTD, B.V Holdings LTD, Ndovu Soaps LTD, Navy Cut Tobacco (T) LTD, Changanyikeni Residential Complex LTD na Kagoda Agriculture LTD.
Kwa upande wa makampuni tisa yaliyochota Sh 42.6 bilioni ni pamoja na G&T International LTD, Excellent Services LTD, Mibale Farm, Liquidity Service LTD, Clayton Marketing LTD, M/S Rashtas (T) LTD, Malegesi Law Chambers (Advocates), Kiloma and Brothers na KARNEL LtD.
Kumbukumbu za makampuni mengine mawili ya Rashtas (T) na G&T International LTD, zikiwemo nyaraka za usajili hazikuonekana katika daftari la Msajili wa Majina ya Makampuni na Biashara (BRELA).
Kufikia mwaka 1999 deni katika EPA lilifikia dola 623 milioni, ambazo kati ya hizo dola 325 milioni zilikuwa ni deni la msingi na dola 298 ni riba na kisha baadaye, deni likaongezeka hadi kufikia dola 677 milioni.
Hata hivyo, chini ya Mpango wa Kununua Madeni (Debt Buy Back Scheme) wa mwaka 1994 kati ya serikali na Benki ya Dunia (WB), waliokuwa wanaidai BoT waliombwa wakubali kulipwa sehemu tu ya fedha wanazodai, wapo waliokubali na wengine kukataa na kuongeza hadi mwaka 2004 taarifa zinaonyesha jumla ya dola 228 zililipwa chini ya mpango huo.
EPA ni akaunti ya madeni ambayo ilitumika wakati wa Mfumo wa Ujamaa, ambayo akaunti yake ilikuwa katika iliyokuwa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) chini ya usimamizi wa BoT.
Mwaka 1985, EPA ilihamishiwa moja kwa moja BoT, na ndipo mwaka juzi kulipoibuka utata wa tuhuma za ufisadi katika akaunti hiyo kwa mahesabu ya mwaka 2005/06, ambayo utata huo ulisababisha Ernst&Young kufanya ukaguzi kuanzia Septemba sita na kukabidhi ripoti yake kwa CAG mapema Desemba mwaka jana.