PostGE2025 THRDC & TLS: Tunalaani vitendo vya mauaji na ukatili vilivyofanywa dhidi ya raia wasio na hatia wakati wa maandamano

Conversations and stories after Tanzania's 2025 General Elections

Mwanamwana

Platinum Member
Joined
Aug 1, 2011
Posts
9,604
Reaction score
22,722
Tamko Kuhusu Matukio ya Ukiukwaji wa Haki za Binadamu Wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2025 (29 Oktoba hadi 04 Novemba)

1.0 Utangulizi

Tamko la Mtandao Wa Watetezi Wa Haki za Binadamu Tanzania na Chama Cha Wanasheria Tanganyika Kuhusu Matukio ya Ukiukwaji wa Haki za Binadamu Wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2025. Kwa pamoja, tumestushwa na kuhudhunishwa na matukio makubwa ya ukiukwaji wa haki za binadamu yaliyotokea wakati wa uchaguzi kuanzia tarehe 29 Octoba na kuendelea hadi hivi sasa. Tumeshuhudia vijana wengi wakipigwa risasi na kupoteza maisha na wengine kubaki na majeraha makubwa bila matibabu wakati walipokuwa katika maandamano na wengine wengi kufuatwa katika makazi yao. Ni masikitiko yetu kwamba haya yanatokea baada ya jitihada za TLS, THRDC pamoja na makundi mengine kutafuta muafaka wa kitaifa kabla ya uchaguzi kutokuungwa mkono na wenye mamlaka.

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) tunalaani vitendo vya mauaji na ukatili vilivyofanywa dhidi ya raia wasio na hatia wakati wa maandamano. Tunataka vyombo vya usalama wakati wote kuheshimu maandamano ya raia na kuyaongoza vizuri kusudi yasigeuke kuwa vurugu na uharibifu kwa kuwa swala la kuandamana kwa amani ni haki ya kikatiba. Hili ni jukumu la msingi kwa Jeshi la Polisi. Vilevile tunatoa pole za dhati kwa familia zote zilizopoteza wapendwa wao, na kwa wote walioumia au kupoteza mali au mali zao kuharibiwa kutokana na vurugu hizo.

2.0 Matukio ya Ukiukwaji wa Haki za Raia

Uchaguzi Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ulipangwa kufanyika tarehe 28 Oktoba 2025 (Kura ya Mapema Zanzibar) na tarehe 29 Oktoba 2025. Hata hivyo, siku ya tarehe 29 Oktoba 2025, majira ya asubuhi, maandamano ya wananchi waliokuwa wakidai uchaguzi huru na kupinga matukio ya utekwaji wa raia yalianza katika maeneo mbalimbali nchini, yakidai maboresho ya mifumo na sheria ya uchaguzi, ulinzi wa haki za binadamu na democrasia nchini. Ni ukweli usiopingika kwamba kufanya mandamano ya amani nchini ni haki ya kikatiba kwa mujibu wa Ibara ya 18 na 20 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vijana hao wadogo walikuwa wanatumia haki yao ya kikatiba kuelezea malalamiko yao ya muda mrefu ambayo hayakusikilizwa wala kufanyiwa kazi kabla ya uchaguzi.

a) Mauaji ya Raia

Maandamano hayo yalijibiwa kwa nguvu kubwa na vyombo vya ulinzi na usalama, hasa Jeshi la Polisi, ambavyo vilitumia risasi za moto na mabomu ya machozi kuzuia maandamano hayo. Tukio hilo limesababisha mauaji ya kutisha ya raia wengi wasio na hatia, ingawa idadi kamili ya vifo bado haijathibitishwa taarifa tulizo nazo zinaonyesha watu kwa mamia hasa vijan wadogo kwa mamia wameuwawa na kujehuriwa na wengine kwa mamia kukamatwa. Matukio haya yameripotiwa katika mikoa kadhaa ikiwemo Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Arusha, Songwe, Geita, Mara, Shinyanga, na miji ya Tunduma, Katoro, Kahama, Tarime, pamoja na maeneo mengine nchini. Matendo haya yameweka doa kubwa kwa Taifa letu ndani na nje yan nchi.

Tumebaini kuwa watu wengi hasa vijana wamepigwa risasi wengine wakiwa kwenye maandamano na wengine wakiwa majumbani mwao au katika shughuli zao za kawaida. Miili ya waliouwawa tumeshuhudia ikitapakaa maeneo kadhaa na badaye kupelekwa katika hosptali mbalimbali.Wapo ambao wamepoteza maisha kwa kukosa matibabu na wengine kujitibia majeraha majumbani. Mfano wapo mawakili na waandishi wa habari ambao wamepoteza maisha yao wengine wakiwa katika kazi zao na wengine wakiwa majumbani mwao. Taarifa tulizopata toka kwa wananchi ni kuwa wazazi wengine ambao hawakuona mili ya watoto wao wameanza kuulizia watapataje miili hiyo ili wakawazike. Ni muhimu sana wazazi wakapewa miili ya vijana wao walioumia au kufariki.

b) Uharibifu wa Mali

Mbali na mauaji hayo, pia kumetokea uharibifu wa mali za umma na mali binafsi katika maeneo kadhaa. Miongoni mwa mali zilizoharibiwa ni vituo vya mwendokasi, vituo vya mafuta, magari, ofisi za serikali na vituo vya kupigia kura vilivyoteketezwa kwa moto, pamoja na masanduku ya kura yaliharibiwa au kuchomwa moto yakiwa na kura chache zilizopigwa na yale ambayo yalikuwa na karatasi za kupigia kura. Kwa ujumla , hatuungi mkono uharibifu huu na tunaendelea kushauri watanzania wakati wa maandamano wasifanye uharibu wa mali badala yake wajikite katika malengo ya kuandamana. Mali zote hizi za serikali ni mali za umma ambazo zinatokana na kodi za wananchi. Hivyo ni vyema kulinda mali za umma na kufanya maandamano ya amani kwa mujibu wa katiba.

Hata hivo, bado hii haiwezi kuwa sababu ya kutumia risasi za moto na kuua mamia ya vijana wetu na wengine kufuatwa hadi majumbani mwao na kuchukuliwa na kwenda kuteswa na wengine kushambuliwa kwa risasi. Hakukua na sababu yoyote ile ya kutumia risasi za moto dhidi ya raia tena raia wengine kufuatwa wakiwa majumbani mwao na walikuwa hawahusiki kabisa na maandamano. Siku zote raia wakiongozwa vizuri na vyombo vya usalama na kusimamiwa vizuri katika maandamano yao madhara huwa ni madogo sana au hakuna kabisa.

c) Kusimamisha Huduma ya Mtandao wa Intaneti

Katika kipindi hicho hicho pia, huduma ya msingi ya mtandao wa intaneti ilizimwa nchi nzima (tarehe 29 Oktoba hadi Novemba 03, 2025), hatua iliyosababisha athari kubwa kwa wananchi na taasisi mbalimbali. Uamuzi huo uliathiri haki ya watu kuwasiliana na kupata taarifa, ukasababisha kukwama kwa shughuli nyingi za biashara, huduma za kibenki, huduma za miamala ya fedha inayotumia intanenti, usafiri wa anga, huduma za afya katika vituo vya afya, usafiri wa umma na binafsi, na kukosekana kwa upatikanaji wa taarifa muhimu kwa umma. Hatua hiyo ni kinyume na masharti ya Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayolinda haki ya kupata taarifa na kujieleza bila vikwazo vya aina yoyote, Mikataba ya Kimataifa ya Haki za Binadamu pamoja na Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu. Kuzuia matumizi ya Mtandao wa intaneti ni kinyume na haki za binadamu na Katiba kwa kuwa matumizi ya mtandao kwa sasa ni mojawapo ya haki za msingi za binadamu na ni nyenzo muhimu ya kufikia na kuishi haki za binadamu. Taifa pamoja na watu binafsi watakuwa wamepata hasara kubwa sana kutokana na kuzimwa kwa mtandao wa intaneti.

d) Kukamatwa na Kupigwa

Pamoja na mauaji ya raia wasio na hatia, kumekuwa na matukio mengine ya uvunjaji mkubwa wa haki za binadamu, ikiwemo kukamatwa kwa waandishi wa habari, wanasiasa, na watetezi wa haki za binadamu. Wengi wao wamefanyiwa vitendo vya mateso, na ukamataji holela usiozingatia sheria. Hali hii imezua hofu kubwa miongoni mwa wananchi na imeathiri mazingira ya uhuru wa kujieleza, uhuru wa kukusanyika, na haki ya kushiriki katika masuala ya kisiasa kwa uhuru na usalama. Baadhi ya waandishi wa habari wamechukuliwa vifaa vyao na hadi leo tarehe nne zoezi la kuendelea kukamata waandishi wa habari linaendelea katika maeneo mbalimbali ya nchi. Hali hii ya msako na ukamataji inaendelea hadi sasa na kuendelea kuwaweka wananchi katika hofu kubwa bila sababu ya msingi. Vijana wengi wanashikiliwa katika vituo vya polisi na maeneo mengine bila msaada wowote wa ndugu au wanasheria.
Kwa ujumla, matukio haya yameacha athari kubwa katika mustakabali wa haki za binadamu, utawala wa sheria, na demokrasia nchini Tanzania, na yanahitaji hatua za haraka za uchunguzi huru, uwajibikaji, na urejeshwaji wa haki kwa wahanga.

3.0 Jitihada ambazo THRDC na TLS imewahi Kuzichukua Kabla ya Madhara yaliyotokea

THRDC na TLS mara kadhaa tumetoa mapendekezo huko nyuma, tumetoa ushauri na nasaha kwa Serikali, Chama Tawala ikiwemo kutaka mwafaka wa kitaifa kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 lakini sauti zetu zilipuuzwa na hakuna aliyekuwa tayari kuliponya taifa kabla ya kuelekea kwenye uchaguzi. Sisi tuliamini kabisa njia iiyokuwa bora ya kuzuia wananchi kusimama kudai haki zao barabarani ilikuwa ni mazungumzo na maridhiano ya kitaifa ambapo malalamiko ya muda mrefu ya watanzania yangefanyiwa kazi kabla ya uchaguzi. Tunaamini kwamba ukweli na uadilifu havipotei kwa kupuuzwa, wala dhamiri haifi katika ukimya.

Hatujachagua kufika katika kipindi hiki cha giza na maafa kwa Taifa, tumefikishwa hapa kwa kulazimishwa na wachache ambao hawakuwa tayari kusikiliza sauti za wananchi na kuzifanyia kazi. Wakati ukweli na ushauri unadharauliwa, taifa huzama katika giza. Lakini giza haliwezi kushinda mwanga wa dhamiri iliyo ya haki. Mwanga wa ukweli unaweza kukandamizwa kwa muda, lakini daima hurudi ukiwa mkali zaidi, wenye nguvu zaidi, na usioweza kuzuilika.

Tunamsihi kila mmoja wetu na mpenda haki kupinga ukandamizaji kwasababu kupinga ukandamizaji siyo uasi ni uzalendo na ndio njia bora ya kulinda amani, umoja na mshakamano nchini. Ni wajibu mtakatifu wa kila raia anayeamini kwamba uhuru, haki, na heshima ya binadamu si zawadi kutoka kwa wenye nguvu, bali ni haki alizopewa kila mmoja na dhamiri na Mungu. Watanzania wana haki ya kulinda na kutetea haki zao, na wanapofanya hivyo vyombo vya dola kamwe visiwazuie wala kuwaumiza au kuwaua.

4.0 Wito wa THRDC na TLS

a) Tunatoa wito kwa wale ambao hawajui walipo watoto wao au ndugu zao kutoa taarifa kwa mamlaka husika na kwa mashirika wanachama wa haki za binadamu pamoja na ofisi za TLS zilizopo makao makuu na kila mkoa ili kusaidia juhudi za ufuatiliaji.
b) Tunatoa wito kwa Jeshi la Polisi kuacha kupita kwenye nyumba za watu kukamata waandishi wa habari, wananchi, wanasiasa, na watetezi wa haki za binadamu na wasitishe nia ya kutaka kuwafungulia makosa ya ugaidi.
c) Tunatoa wito kwa Jeshi la Polisi kusitisha ukamataji unaoendelea nchini dhidi ya wale wanaoshutumiwa kwa kuhamasisha maandamano au kutoa maoni yao kwa amani.
d) Tunatoa wito kwa mashirika wanachama wa THRDC na TLS kutoa msaada wa kisheria bure kwa familia zilizopoteza wapendwa wao, waliopoteza watoto, au waliokamatwa kinyume cha sheria na waliofunguliwa au watakaofunguliwa mashtaka.

5.0 Hitimisho

THRDC na TLS tunasisitiza kuwa amani ya kweli na demokrasia haviwezi kujengwa kwa kukandamiza uhuru wa kujieleza, kukandamiza haki za kiraia, kukamata watu kiholela, au kuzima njia za mawasiliano. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ichukue hatua za haraka kurejesha hali ya utulivu, umoja, demokrasia ya kweli, uwazi, na ulinzi haki za binadamu kwa mujibu wa Katiba, Sheria za nchi na Mikataba ya Kikanda na Kimataifa ambayo Tanzania imeridhia.

Tunabaki na dhamira thabiti ya kulinda haki, uhai, na utu wa kila Mtanzania ili kujenga taifa lenye amani, upendo na mshikamano.

Imetolewa leo Novemba, 4 Mwaka 2025:
 

Attachments

Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…