kumbe kweli?????????
TID afungwa jela mwaka mmoja
Na Rehema Maigala
MSANII mahiri wa muziki wa kizazi kipya nchini Khalid Mohammed a.k.a TID (26), mkazi wa Kinondoni, Dar es Salaam, amehukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela kwa kosa la shambulio.
Msanii huyo maarufu nchini alijikuta akishika kichwa ghafla jana baada ya kumsikia Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, Hamisa Kalombola akisoma hukumu hiyo ambayo haikuwa na faini wala fidia.
Baada ya hukumu hiyo, msanii huyo alishikwa kwa umakini na askari magereza kwa ajili ya kupelekwa chumba cha mahabusu ili kusubiri safari ya kwenda gerezani.
Muda mfupi baadaye TID, alitolewa nje ya chumba cha mahabusu, huku akiwa ameshikwa mkono na ndugu zake wakisaidiana kumvua shati, kwani ilionekana kama amepata presha ya ghafla kutokana na hukumu hiyo, ambapo ndugu zake pamoja na marafiki walionekana na nyuso za huzuni.
Mlalamikaji katika kesi hiyo, Ben Mashibe alileta mashahidi wanne katika Mahakama hiyo, ambao wote kwa pamoja walielezea jinsi mshitakiwa alivyompiga mlalamikaji na kumsababishia maumivu makali kichwani.
Mshitakiwa alidai yeye ana shahidi mmoja, hata hivyo alishindwa kumleta mahakamani kwa kuwa alikuwa safari, ambapo jana kabla ya kutoa hukumu, Hakimu Kalombola alimtaka mshitakiwa ajitetee ili mahakama impunguzie adhabu na katika utetezi wake alidai ana familia inayomtegemea hasa mama yake mzazi.
Awali ilidaiwa mahakamani hapo kuwa Julai mwaka jana, mshitakiwa alimshambulia mlalamikaji kwa kumpiga na trei ya bia kichwani walipokuwa Masaki Slip Way jijini Dar es Salaam na kumsababishia maumivu makali.