SoC02 Tozo ndiyo kipimo cha uzalendo?

Stories of Change - 2022 Competition

Chebu

New Member
Joined
Sep 4, 2022
Posts
2
Reaction score
0
Tozo ni msamiati ambao kwa lugha ya mtaani tunaweza kusema watanzania 'waliuchukulia poa' lakini ndani ya it is itmiezi 18 umejizolea umaarufu wenye kuibua hisia tofauti miongoni mwa Watanzania.

Mjadala kuhusu tozo ni mkubwa, na kwa hakika bado kuna mengi yanahitaji kuhojiwa na kufafanuliwa ili mwafaka upatikane na ujenzi wa taifa uendelee.

Swali la msingi, je tozo ni halali?

Katika maandiko matakatifu ya Biblia Yesu aliwahi kuulizwa, je ni halali kulipa kodi kwa Kaisari (mtawala/serikali)?

Kwa kifupi sana jibu la Yesu lilikuwa ni ndiyo. Kulipa kodi siyo dhambi bali ni wajibu. Kwa mujibu wa katiba muundo wa serikali kimamlaka umegawanyika mara mbili; serikali kuu na serikali za mitaa. Serikali kuu inapata mapato yake kwa KUTOZA KODI za viwango tofauti kwa mujibu wa sheria zilizopitishwa na Bunge na walipa kodi wamegawanywa katika mafungu mbali mbali kulingana na viwango husika. Mapato ya serikali za mitaa yanapatikana kwa KUTOZA USHURU kwa mujibu wa sheria ndogo, kanuni na taratibu zilizopitishwa na halmashauri za mamlaka husika.

Hata kwa maandishi tu KUTOZA TOZO ni kitendo kinachojirudia; ni kudai kodi/ushuru kwa mara ya pili.

Kwa mujibu wa serikali tozo ni KODI YA UZALENDO na ni juhudi za serikali kupanua wigo wa kodi ili kuiwezesha nchi kugharamia utekelezaji wa miradi ya kimkamkati.

Inawezekana kwa makusudi au kwa bahati mbaya kodi halali ambayo mamlaka husika zilikuwa zimeshindwa kuweka mikakati na mfumo unaoeleweka wa kuwatoza wafanyabiashara wa nyumba/vyumba vya kupangisha nayo pia imekuja kwa kivuli cha tozo. Hili ni kosa ambalo gharama yake anailipa mpangaji kwa sababu ya hisia hasi kuhusu tozo baadhi wafanyabiashara wa nyumba za kupangisha hawatakubali kupoteza kipato chao kwa hiyo watapandisha kodi ya upangishaji ili mzigo wa tozo ubebwe na mpangaji, tofauti na kama kodi hii ingekuja kwenye mfumo rasmi wa kodi za mapato ikiambatana na mwongozo wa serikali kuhusu viwango elekezi vya gharama za upangishaji nyumba/vyumba.

Wanasiasa wanapotumia kodi hii, ambayo serikali imeshindwa kuweka mfumo bora wa kuikusanya na kuipatia nchi mapato, kuhalalisha tozo za miamala kwa simu ni kuwatapeli wananchi.

UHARAMU WA TOZO ZA SERIKALI MIAMALA KWA SIMU
Mageuzi makubwa ya kitekinolojia mwanzoni mwa karne ya 21 yamebadilisha kwa kiasi kikubwa sekta ya habari na mawasiliano. Miongoni mwa athari chanya za mabadiliko hayo ni urahisi wa kutuma na kupokea taarifa za kibenki (banking information) kupitia simu za mkononi. Kuna uwekezaji unaoambatana na gharama kubwa za uendeshaji wa mifumo hii inayoturahisishia maisha kwa hiyo si jambo la ajabu kulipia TOZO KWA WATOA HUDUMA.

Watoa huduma (kampuni za simu na mabenki) ni wafanyabiashara wanaotozwa kodi na serikali kwa viwango walivyokubaliana ambavyo serikali imeridhika navyo.

Tozo zilizowekwa na mtoa huduma zimezingatia hali ya ushindani wa soko, gharama za uendeshaji zitakazomwezesha kuendelea kutoa bora huduma kwa mteja na kulipa kodi ya serikali. Je tozo ya serikali imezingatia vigezo gani?

Inawezekanaje serikali kumtoza tozo mwananchi kwa huduma ambayo ameishailipia kwa mtoa huduma ambae pia ameshatozwa kodi na serikali hiyo hiyo? Huyu mwananchi anaekamuliwa maziwa na watoa huduma na kunyonywa damu na serikali yake ataishi maisha ya namna gani?

Kumtoza tozo mwananchi ni kumnyang'anya fedha zake bila kujali kazipataje na ana changamoto za mahitaji gani. Serikali isiyojali ni ajali kwa wananchi wake, hasa wenye kipato cha chini. Chukulia mfano wa mfanyakazi anaepokea mshahara wa laki 3 kupitia benki, anakatwa kodi ya serikali na makato mengine halali zikiwemo gharama za kibenki.

Mtanzania huyu, kama asilimia kubwa ya Watanzania wengine, ana majukumu lukuki ya kifamilia, miongoni mwa majukumu hayo kuna mzazi mgonjwa kijijini anahitaji fedha ya matibabu. Mfanyakazi huyu akihamisha kiasi kutoka benki kwenda kwenye mtandao wa simu anakutana na tozo ya serikali na tozo ya mtoa huduma, akimtumia mzazi fedha vivyo hivyo serikali inachukua tozo na mtoa huduma pia, mzazi akitoa anunue dawa hadithi ni hiyo hiyo ya tozo.

Kama ubunifu wa wataalamu wa uchumi wizara ya fedha kupanua wigo wa mapato umekomea kwenye tozo ya miamala ya simu suluhisho ni serikali kuongea na watoa huduma (kampuni za simu na mabenki) wafanye marekebisho kwenye viwango vya kodi wapate kiasi wanachokitaka ili sasa watoa huduma washindane wao kwa wao kwenye viwango vya tozo. Serikali kuingiza mkono kwenye akaunti za watu ni unyang'anyi usioweza kuhalalishwa kwa propaganda yoyote ya kisiasa.

Wananchi wanapohoji uhalali wa tozo wanaonyesha uzalendo wao na si kinyume chake. Serikali inapowahoji Wananchi wanaotumia haki yao ya kikatiba kutoa maoni kuhusu uhalali wa tozo inaashiria siyo tu matumizi mabaya ya mamlaka lakini pia uoga wa serikali kwa sauti za wananchi pale wanapodai haki.

Kama tozo si unyang'anyi kwa nini kuzima sauti za wananchi wanapohoji matumizi yake?

Kama miradi ya kimkamkati inayohitaji kugharamiwa na tozo ilianzishwa, ikaendelezwa bila tozo imeshindikanaje kumalizika bila tozo?

Vyanzo vya mapato ya fedha ya kumalizia miradi hiyo vimekumbwa na dhahama gani ya ghafla kiasi hiki?

Kwa nini Wananchi wasiambiwe kama miradi ilikuwa inategemea mikopo au misaada ya wafadhili ambao wamejitoa ghafla na sasa inabidi Watanzania wabebe mzigo migongoni mwao badala ya kudandia lifti ya misaada au miikopo?

Au kwanini wananchi wasiambiwe kuwa miradi hiyo ilikuwa inagharamiwa na mapato ya kodi ya ndani ambayo sasa imepunguzwa au imesamehewa kabisa kwa hiyo bila tozo miradi itakwama?

Kama yote hayo siyo basi tuambiwe miradi hii ilianzishwa bila mikakati maalumu ya kuigharamia kwa hiyo kila anaeingia 'anajiongeza' ili ikamilike.

Unaanzaje kuhoji uzalendo wa Watanzania wanaouliza maswali kuhusu uhalali wa tozo na matumizi yake wakati serikali inatoa ufafanuzi kuwa tozo imetumika kujenga vyumba vya madarasa na zahanati wakati majengo hayo hayo yanajieleza kwa mabango kuwa yamejengwa kwa fedha za uviko 19? Unawaeleweshaje wananchi wazalendo walipa kodi na ushuru ambao wameshuhudia vyumba vya madarasa na majengo ya vituo vya afya yakijengwa bila tozo wala fedha za uviko 19?

Machungu ya Watanzania wengi siyo tu uharamu wa tozo inayozidi kuwazamisha kwenye lindi la umasikini bali pia kukosekana kwa maelezo yaliyonyooka kuhusu matumizi halisi ya tozo. Watanzania wanahisi 'wanapigwa' serikali yao wenyewe. Minong'ono ya 'upigaji umerudi' inaanza kuzoeleka mitaani ila itachukua muda kwa maumivu ya masikini kunyang'anywa hata kidogo walichonacho na wenye nacho kuongezewa kuzoelezeka.

Tanzania inayojengwa na wenye moyo na kuliwa na wenye meno iko kwenye hatari ya kupasuka mikononi mwa watawala wanaobeza kilio cha wananchi kuhusu ugumu wa maisha wanaokabiliana nao. Tunaposema Tanzania ni yetu sote tuseme kwa moyo wa dhati na tuthibitishe kauli zetu kwa vitendo dhahiri visivyotia shaka nia na dhamira zetu.

Tanzania haiwezi kuwa yetu wote ikiwa wakulima, wafanyakazi na wachuuzi wa Tanzania wanakamuliwa tozo wakati wenye mamlaka wanakula kwa urefu wa kamba, angalizo pekee likiwa "wasivimbiwe" Kiuhalisia ni kuwa kadri watu wachache wenye kamba zao ndefu wanapotafuta malisho bora zaidi ndivyo kamba hizo zinavyozidi kukaza kwenye shingo za Watanzania walio wengi wanaoishi maisha ya bora mkono uende kinywani.

Hawa unapowaambia hii nchi ni yetu wote unawadhihaki na inapowatoza tozo unawanyang'anya hata hicho kidogo walichonacho.

Tuendelee kusalimiana kwa jina la jamhuri yetu.
 
Upvote 0
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…