SoC02 Tozo

Stories of Change - 2022 Competition

HARIDI KORONGO

New Member
Joined
Sep 13, 2022
Posts
1
Reaction score
0
MTUNZI: HARIDI KORONGO
JINA LA SHAIRI TOZO

1.Tunamshukuru muumba, alie tupa pumzi.
Tanzania yetu nyumba, anailinda mwenyezi.
Twapaswa kua sambamba, amani kwa kuienzi.
Asanteni jamii, kutupa fursa hii.

2.Uchumi wetu kupanda, lazima tushikamane.
Tujenge chetu kibanda, wageni watazamane.
Hata kwa kula mrenda, tozo tushirikiane.
Ahsanteni jamii, kutupa fursa hii.

3.Kweli tozo ni ujenzi, hakuna aliepinga.
Ila tusipigwe konzi, tukageushwa mandonga.
Wakusanya kwa mapenzi, matokeo ndio chenga.
Asanteni jamii, kutupa fursa hii.

4.Tozo isiwe mzigo, haswa usiobebeka.
Uraiani ni zogo, tena mengi husemeka.
Wapo kimya vigogo, raia tunachomeka.
Asanteni jamii, kutupa fursa hii.

5.Raia wanalalama, wala hamtii shaka.
Sisi sote ni wa mama, uchumi kuusimika.
Na tozo isije kwama, elimu yahitajika.
Asanteni jamii, kutupa fursa hii.

6.Mkuu wetu Mwigulu, mtoto wake Nchemba.
Sisi sio wakabulu, ubaguzi kwa viremba.
Wajuu sukari gulu, wachini mwatuperemba.
Asanteni jamii, kutupa fursa hii.

7.Usingoje taharuki, alafu muunde tume.
Kabla kushika maiki, jitasimini jiseme.
Maisha yetu mkuki, tozo kwetu tezi dume.
Asanteni jamii, kutupa fursa hii.

8.Tazama maisha yetu, kwa mbali unayaona.
Hili ni taifa letu, hatupaswi kupishana.
Maendeleo ni yetu, sio kwa kuandamana.
Asanteni jamii, kutupa, fursa hii.

9.Kwanini iwe mzozo, tozo ni maendeleo.
Sisi sio bongo zozo, maisha ni kesho na leo.
Irekebisheni tozo, isiwe yapanda cheo.
Asanteni jamii, kutupa fursa hii.

10.Tozo ya kila pahala, punguzeni tupumue.
Maisha yetu yanalala, usiombe usikie.
Mambo mpela mpela, sisi wezangu na mie.
Asanteni jamii, kutupa fursa hii.

11.Serikali ya utulivu, sikio kwa watu wake.
Kiongozi si mvivu, tetea usibweteke.
Tuta ambulia jivu, tukiyaweka makeke.
Asanteni jamii, kutupa fursa hii.

12.Kwanza tupeni elimu, kufahamu vilivyomo.
Ni kweli tuna nidhamu, tozo imezidi kimo.
Weka wazi tufahamu, si kutupa kwenye shimo.
Asanteni jamii, kutupa fursa hii.

13.Kumbukumbu ni kwa baba, sio baba wa taifa.
Kawezaje msalaba, na kuziba zile nyufa.
Hofu yetu mwatukaba, hadi sisi tutakufa.
Asanteni jamii, kutupa fursa hii.

14.Tozo si kukomoana, lazima tuumizane.
Mwishoe twasakamana, hii tozo ya karne.
Mawazo yakikutana, umoja upatikane.
Asanteni jamii, kutupa fursa hii.

15.Wala sio la waganga, eti tukapige ndumba.
Hapa hatutaki chenga, yapaswa tuwe sambamba.
Mpaka kipigwe kipyenga, utamu wote kuramba.
Asanteni jamii, kutupa fursa hii.
 
Upvote 1
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…