`Shehena ya Barrick ilikuwa na mabomu`
2008-12-20 14:41:55
Na Grace Chilongola, Mwanza
Ukaguzi uliofanywa kwenye shehena ya kampuni ya dhahabu ya Barrick Tanzania, iliyozuiliwa kwa muda katika uwanja ndege wa Mwanza imebainika kuwa ni mabomu ya kurushwa kwa mkono na yale ya kutoa machozi pamoja na risasi.
Ukaguzi huo ulifanywa kwa kushirikisha Jeshi la Polisi, Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Usalama wa Taifa pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Katika mahojiano na waandishi wa habari ofisini kwake, Meneja Forodha wa TRA Mwanza, Leopold Kihumo alisema wao kama TRA baada ya kupata taarifa ya shehena hiyo waliikabidhi polisi kwa ajili ya utaratibu wa ukaguzi.
``Shehena kama hizo zikiingia TRA (forodha) huwa hatujiridhishi peke yetu na badala yake tunashirikiana na taasisi nyingine kama za jeshi la Polisi, JWTZ na Usalama wa Taifa,`` alisema.
Kwa mujibu wa Kihumo shehena hiyo iliyokuwa ifike Desemba 5, ilichelewa kuondoka kwa ajili ya kuvipa nafasi vyombo vingine kufanya ukaguzi na kwamba ilikuwa na uzito wa tani 1.4 ambapo ililipiwa kodi inayofikia Sh. Mil 144.
Kihumo alisema shehena hiyo ilitumia taratibu zote za kuombewa kibali na ndio maana baada ya kujiridhisha na ukaguzi iliruhusiwa kuendelea na safari.
``Shehena kama hii huwezi kuiacha ikaingia mtaani bila kukaguliwa na ndio maana walishirikisha vyombo vingine na walipojiridhisha Kamanda wa Polisi aliruhusu viendelee na safari na kutoa polisi wanne kwa ajili ya kusindikiza,`` alisema.
Hata hivyo, alisema baada ya ukaguzi walipendekeza shehena kama hizo ziwe zinaagizwa na wakala wa serikali wanaojihusisha na silaha na sio mwekezaji.
Naye Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Khamis Bhai alisema taarifa aliyopewa asubuhi na Afisa Upelelezi wa Mkoa, Agustine Olomi alimweleza shehena hiyo ilikuwa na baruti za kulipulia miamba.
Gazeti hili liliripoti kuwepo kwa shehena inayosadikiwa kuwa na baruti za kupasulia miamba, risasi na mabomu ya kurusha kwa mikono na yale ya kutoa machozi mali ya kampuni ya Barrick imezuiliwa kwa muda katika uwanja wa ndege jijini Mwanza kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa kina kubaini vitu vilivyomo.
Wakati huohuo, Simon Mhina anaripoti kuwa kampuni ya Barrick imesema mzigo wake uliodaiwa kukamatwa mjini Mwanza haukuwa na silaha.
Akizungumza na Nipashe jijini Dar es Salaam jana, Meneja Uhusiano wa kampuni hiyo, Teweli Teweli, alisema Barrick haina sababu zo zote za kusafirisha shehena kama hizo kwa vile hazitumii katika shughuli zake za uchimbaji madini.
Akifafanua, alisema hivi sasa walinzi wake hawaruhusiwi kabisa kutumia risasi za moto, na ndio maana hata mgodi wake ulipovamiwa hivi karibuni na wakazi wa Tarime walilazimika kukimbia.
``Shehena yetu haikuwa na mabomu wala risasi, hatuna sababu yo yote ya kuagiza vitu hivyo,`` alisema.