Makufuli yaliyoifungia Dowans yaondolewa kinyemela
Mussa Mkama na Patricia Kimelemeta
MAKUFULI yaliyokuwa yamewekwa katika lango kuu la kuingilia katika eneo la mitambo ya Kampuni ya Dowans, inayojihusisha na ufuaji wa umeme wa dharura, yameondolewa kinyemela.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Dowans, Stanley Munai, hatua hiyo imefanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kupitia wakala wake wa kukusanya madeni sugu, Kampuni ya Udalali wa Mahakama ya Majembe Auction Mart.
Munai alisema hata hivyo, hatua hiyo imefanywa bila kuufahamisha ungozi wa kampuni yake.
Mkurugenzi huyo alisema juzi, wakala huyo alikwenda katika ofisi za Kampuni ya Dowans akiwa na kufuli zake na kuzifunga katika lango kuu la kuingilia katika eneo la mitambo, bila kibali chake kusainiwa.
Alisema hata hivyo jana, wakala huyo alirudi katika eneo hilo na kufungua lango hilo, baada ya kubaini kuwa ametenda kosa.
“Wakati hayo yote yanatendeka juzi mimi au sisi hatukuwa na taarifa ya ugeni wa aina yoyote tuliona makufuli katika milango yetu, tukashangaa, kwa sababu hata kibali cha kusaini kufungiwa kwa milango hiyo hatujasaini,�alisema Munai.
Munai pia alielezea kushangazwa kwake na hatua ya TRA kuidai kodi Dowans, wakati ikiwa imeshafungiwa kwa muda mrefu.
“Tumefungiwa kufanya kazi kwa kipindi kirefu sasa, hivi tunauliza kampuni iliyofungiwa inawezaje kudaiwa kodi wakati haizalishi, hicho ni kitu cha kiungwana kweli,� alihoji Munai.
Alisema kwa sasa, Dowans na TRA zinaendelea na mazungumzo ya kuiwezesha kampuni kujua nini inachodaiwa na wapi inapaswa kulipa.
Alisema "mfanyabiashara na mkusanyaji kodi ni mtu na rafiki yake, wanafanya kazi pamoja na kwa kushirikiana, mfanyabiashara kudaiwa kodi si kitu cha ajabu na lazima alipe."
Kuhusu muda wa siku kumi ambazo Majembe Auction Mart imezotoa kwa Dowans kulipa deni vingine mitambo yake itapigwa mnada, mkurugenzi huyo alisema hizo ni porojo ambazo hazina msingi.
“Sisi hatumjui Majembe, hizo fedha anazodai kuwa tunadaiwa ni porojo zake tu, hafanyi kazi na sisi, kwa hiyo wanayosema ni maneno yao,� alisema.
Juzi kampuni hiyo iliweka kufuli katika lango la Dowans, ili kuishinikiza kuilipa TRA Sh 9 bilioni, jambo ambalo lilisababisha usumbufu kwa wafanyakazi.
Kwa mujibu wa habari hizo, deni hilo linalosemekana kuwa ni la muda mrefu, limetokana na Dowans kushindwa kutolipa kodi zake mbalimbali kwa TRA.
Alipotakiwa kuzungumzia suala hilo, Mkurugenzi Mkuu wa TRA, Harry Kittilya, alisema yeye si mhusika katika suala la ukusanyaji wa kodi na kuweka kufuli katika lango kuu la Dowans.
Alisema wahusika wakuu ni idara ya ukusanyaji wa kodi na kwamba ndiyo yenye mamlaka ya kujua kama kampuni hiyo ama imelipa au haijalipa deni.
Katika maelezo yake juzi, Ofisa Masoko wa Majembe Auction Mart, Dickson Kitime, alisema hatua hiyo imechukuliwa kufuatia kampuni hiyo kushindwa kulipa kodi kwa muda mrefu.
http://www.mwananchi.co.tz/newsrids.asp?id=15910