bonge la story bonge la motivation and insiparation, walio isoma hii hadithi watakubaliana na mimi. Ni mtu aliyetoka maisha ya chini sana familia masikini sana, mambo ya vibarua vya kulima, kuuza sigara mtaani, hadi sasa kufikia level ya kuheshimika katika jamii na kuwa millionaire. Kama bado hujaisoma itafute. Lazima itakufanya usongeee mbele zaidi.
Memories of my life
[Kumbukumbu za maisha
yangu]
by GLOBAL
Oct 22, 2012
SITAKI kuyafanya maisha yangu siri,
nataka watu wote wanifahamu, ndiyo
maana nimeamua kuanzisha ukurasa
huu ili kuelezea yale ninayoyakumbuka
maishani mwangu, tangu nilipozaliwa
mpaka siku nitakapokoma kuandika.
Ninaamini yatakuwepo mengi ya
kujifunza, kutia moyo na pengine
kuonya mtu mwingine asiyafanye kwani
nimefanya makosa mengi sana maishani
mwangu, mengine ni ya aibu lakini
nitayasema hadharani na ninapotakiwa
kuomba msamaha nitafanya hivyo.
Nawakaribisheni kwenye kumbukumbu
zangu za maisha ambazo nimezitunza
kwa muda mrefu, kwa lengo la kuandika
kitabu. Najua yatakuwepo ya
kuchekesha, kutoa machozi na kuinua
mioyo ya waliokata tamaa. Hivyo usikose
kusoma kumbukumbu hizi kila siku ya
Jumatatu kwenye Ijumaa Wikienda.
Nina miaka mitano, ni asubuhi ya siku
na mwezi nisioukumbuka, mwaka 1976.
Kuna ukungu kila mahali, umande
umetapakaa kwenye nyasi. Baba yangu
amenishika mkono, ananipeleka Kijiji cha
Ishigwandama kilichokuwa kama
kilometa mbili kutoka kijijini kwetu
Mwangika.
Ingawa natetemeka kwa baridi kali na
meno yakigongana, kwani sina sweta
mwilini mwangu na manyunyu ya mvua
yanadondoka, bado moyo wangu una
furaha kwa sababu ni siku ya kwanza
napelekwa shuleni kuanza darasa la
kwanza kwenye Shule ya TAPA, sielewi
maana ya neno hili, lakini ndivyo
ninavyosikia linatamkwa.
Tunatembea kidogo, nachoka, baba
anaamua kunibeba begani. Ni mzee
masikini ambaye hakusoma hata darasa
moja lakini anapenda elimu na anaamini
ndiyo itakayowasaidia watoto wake
maishani.
Ngwanone, yaya eligusha, ukasome
getegete! Uligwa?
(Mwanangu, usiendekeze michezo
shuleni, usome kabisa, unasikia?)
anasema baba yangu kwa lugha ya
Kisukuma tukiwa tumekaribia kufika
shuleni.
Nali
gwa! (Nasi
kia) naitikia huku
meno yakigongana.
Shuleni ananishusha mabegani kwake
na kuanza kutembea, kinachoonekana
mbele yangu ni majengo
madogomadogo ya nyasi, ni kama
mabanda ya kuku, nje kuna watoto
wengi, wote wakiwa hawana viatu kama
nilivyo mimi baadhi hawana hata
mashati, pamoja na baridi hiyo wapo
vifua wazi. Wamepauka kama vile
hawakuoga jana yake huku wengine
wakiwa na vipande vya vyakula
mikononi, nilipoangalia vizuri
nikagundua ni viporo vya ugali.
Namwona mtoto mmoja jirani yetu,
ambaye huwa nacheza naye siku zote,
najichomoa kwenye mkono wa baba na
kumkimbilia. Tunasimama pamoja
tukiwa na furaha, ni siku ya kwanza
shuleni. Huyu anaitwa Joki (hivi sasa ni
marehemu, alifariki miaka michache
iliyopita), haukupita muda mrefu sana
akaja mtoto mwingine, pia namfahamu
anaitwa Malila (huyu yupo kijijini mpaka
leo, ni rafiki yangu mkubwa).
Muda mfupi baadaye mwalimu
anajitokeza, simkumbuki jina na
tunamsalimia kwa Kisukuma lakini
anakataa na kututaka tuseme:
Shikamoo Mwalimu. Ni neno geni
kwangu kwani sijazoea kulitumia
nyumbani. Kwangu ni kama neno la
Kichina, nalazimika kulizoea kwani ndilo
litakalokuwa likitumika shuleni kila siku.
Furaha niliyonayo moyoni haina kipimo
kwani nilitamani sana kusoma na siku
zote nilipowaona watoto wakipita
nyumbani kwetu wakielekea shuleni
moyo uliniuma, hakika siku hii ya leo
niliisubiri kwa muda mrefu.
Sasa tutawapima, waliotimiza umri tu
ndiyo watakaoanza shule! Ilikuwa ni
sauti ya mwalimu baada ya salamu,
moyo wangu ukashtuka kugundua
kuwa kumbe kuna watu wasingeanza
darasa la kwanza sababu ya umri wao.
Wote tukapangwa kwenye mstari mrefu
na mwalimu akawa anapita na
kumwambia mwanafunzi mmoja mmoja
anyanyue mkono wake wa kuume na
kuupitisha juu ya kichwa na kugusa
sikio la upande wa kushoto, waliogusa
waliwekwa upande mmoja na ambao
hawakugusa waliwekwa upande wa pili.
Wewe mtoto wa James, acha ujanja
weka mkono wako vizuri, weka katikati
ya kichwa, usiweke kichogoni!
mwalimu alisema kwani mkono wangu
ulikuwa haugusi sikio, ili kulifikia ilibidi
niusogeze kwa nyuma ndipo
nikafanikiwa kuligusa.
Nikajaribu weeee, lakini sikuweza, bila
huruma mwalimu akanisukumizia
upande wa watu ambao walishindwa
kugusa sikio.
Hawa warudi nyumbani mpaka mwaka
kesho, wakue kidogo.
Haikuwa shule tena, iligeuka kuwa
hospitali au kliniki kwani mimi ndiye
niliyeongoza vilio vya wanafunzi wote
waliokataliwa kuingia darasa la kwanza,
nikagalagala chini huku nikimwita baba
ambaye alifika na kuninyanyua. Akaanza
kunibembeleza ninyamaze huku
akiniambia nivumilie tu mwaka kesho si
mbali, sikukubali niliendelea kulia kwa
nguvu nikiamini mwalimu angebadilisha
mawazo lakini haikusaidia, wenzangu
wakaingia darasani nami nikabebwa na
baba begani na kuanza kurejea
nyumbani, njia nzima nililia mpaka
nilipofika nyumbani macho mekundu na
yakiwa yamevimba na sauti imepotea,
inawezekana kabisa nilikuwa na deko.
Nyamaza mwanangu utasoma tu!
ilikuwa ni sauti ya mama yangu.
Labda jaribu wewe, mimi nimeshindwa,
mtoto hasikii! baba aliitikia.
Kubembelezwa na mama
kulininyamazisha, nikaendelea na
mchezo, kumbukumbu ilinirejea
nilipowaona baadaye Joki na Malila
wakirejea kutoka shuleni, roho iliniuma
mno lakini nikajipa moyo na kuamini
mwaka kesho na mimi ningeanza shule
ingawa wao wangekuwa tayari darasa
la pili.
***
Mwaka huohuo 1976, nikawa
nimeshasahau habari za shule, mama
yangu alileta mtoto mwingine nyumbani,
mdogo, mzuri, anafanana na padri Paulo
(huyo alikuwa ni Padri Mzungu wa
Parokiani kwetu Mwangika)
Mama mtoto umemtoa wapi?
Itaendelea