BARD AI
JF-Expert Member
- Jul 24, 2018
- 3,591
- 8,826
Serikali inatarajia kuongeza 7% sawa na Tsh. Trilioni 2.9 ya Makusanyo kwenye Matumizi ya Fedha za Bajeti ya mwaka 2023/24 ili kufikia Tsh. Trilioni 44.38 kutoka Tsh. Trilioni 41.48 ya mwaka 2022/23.
Tsh. Trilioni 26.72 zitakusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kupitia Kodi na kiasi kingine kitatoka kwenye vyanzo vingine visivyo vya Kikodi ikiwemo Misaada, Mikopo Nafuu na Mikopo ya Kibiashara.
Vipi Mdau, Una maoni gani kuhusu Bajeti na Je, inagusa maisha yako?
================
Serikali inatarajia kukusanya na kutumia Sh44.38 trilioni kwa mwaka 2023/2024 ikiwa ni ongezeko la asilimia 7.0 ya bajeti ya mwaka 2022/2023.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba ameyasema hayo leo Jumatatu Machi 13, 2023 wakati akiwasilisha kwa wabunge mapendekezo ya mpango wa Maendeleo wa Taifa na Ukomo wa Bajeti kwa mwaka 2023/2024.
Bunge mwaka jana lilipitisha Sh41.48 trilioni kwa ajili ya bajeti ya mwaka 2022/2023 kwa ajili ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka huo wa fedha.
Amesema katika mwaka wa 2023/2024 mapato ya ndani yanatarajiwa kuwa Sh31.38 trilioni sawa na asilimia 70.7 ya bajeti yote.
“Kati ya mapato hayo, mapato yanayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yanakadiriwa kuongezeka kwa asilimia 13.0 hadi Sh26.72 trilioni kutoka makadirio ya Sh23.65 trilioni mwaka 2022/23,”amesema.
Amesema misaada na mikopo nafuu kutoka kwa washirika wa maendeleo inatarajiwa kufikia Sh5.46 trilioni sawa na asilimia 12.3 ya bajeti yote.
Aidha, Dk Mwigulu amesema Serikali inatarajia kukopa Sh5.44 trilioni kutoka soko la ndani ambapo Sh3.54 trilioni ni kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za Serikali zinazoiva.
Amesema pia Sh1.89 trilioni kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo na kwamba Serikali inatarajia kukopa Sh2.1 trilioni kutoka soko la nje kwa masharti ya kibiashara ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya miundombinu.
MWANANCHI