SoC01 Tubadili mtazamo ili kumaliza maovu yanayoumiza jamii zetu

SoC01 Tubadili mtazamo ili kumaliza maovu yanayoumiza jamii zetu

Stories of Change - 2021 Competition
Joined
Jul 22, 2021
Posts
7
Reaction score
5
Na Nkuruma wa Karne ya 21.

Maisha ya Mwanadamu yamesimama katika misingi ya Sheria ambazo zinakuwa kama kanuni ya matendo na kauli za kila mwanajamii wa jamii husika.

Sheria ndiyo huweka misingi ya jinsi gani watu wa jamii husika waishi, ikiwa Sheria zitakuwa mbaya basi watu wa jamii hiyo huishi vibaya Sana na ikiwa Sheria zitakuwa nzuri basi jamii huishi vizuri Sana ikiwa sheria hizo zitazingatiwa kama zinavyoagiza.

Viongozi wa jamii yoyote duniani Mara nyingi hutokana na watu wa jamii za eneo husika na hivyo huongoza ndugu zao na matendo ama maamzi yao kugusa maisha ya jamii husika moja kwa moja, hii inadokeza kuwa ikiwa jamii inao watu wengi wenye fikra pevu basi hata watakaopata nafasi za kuwaongoza kwa kuwa watatokana na jamii hiyo na jamii yenyewe ndiyo itakayowaamini na kuona wanasifa basi Uongozi bora utapatikana na kufanya jamii hiyo iishi vema pia.

Heinrik Ibsen, Maandishi mashuhuri wa riwaya na tamthiliya wa Karne ya 20 kutoka Norway aliamini kuwa maisha ya jamii husika unatokana na fikra za waliowengi katika jamii hiyo. Aliamini kuwa ikiwa jamii inao watu wengi wenye mitazamo chanya juu ya maisha ya kijamii basi maisha ya jamii hiyo yatakuwa shwari kabisa lakini ikiwa waliowengi watakuwa na fikra zisizofaa basi jamii hiyo itaishi kwa madhila makubwa na asiwepo wa kukema na akitokea ndiye atakayeonekana kuwa hana fikra njema.

"Mtazamo mbaya wa waliowengi katika jamii ndio ulinzi wa maovu na wanaotekeleza maovu hayo katika jamii yao" ni maneno aliyoyaandika Ibsen katika tamthiliya yake maarufu ya 'Adui wa watu' ambayo aliitumia kukosoa vikali tabia mbaya za baadhi ya viongozi wa umma na jamii zao kama vile Unafiki, mwamko duni wa jamii katika masuala yanayowahusu, usaliti na ubinafsi aliyoyataja kama nyenzo zinazolea maovu yanayoathiri jamii za watu.

Heinrik Ibsen anatoa somo kwa jamii kuwa, mtazamo wa jamii ndio unabeba maisha ya jamii husika, yaani matendo ya viongozi, uhusiano kati ya makundi mbalimbali ya kijamii na hata mtu mmojammoja unatafsiri mtazamo wa waliowengi katika jamii hiyo.

Hii inamaanisha kuwa, ikiwa jamii inawatu wengi wanaoona mambo fulani kuwa hayafai basi mambo hayo hayawezi kushamiri ama kutekelezeka katika jamii hiyo na ikiwa wengi katika mtazamo wao wanayaona mambo hayo kuwa yanafaa ama hawana uelewa juu ya athari za mambo hayo, uwezekano wa kushamiri kwa mambo hayo katika jamii hiyo unakuwa mkubwa na hata wachache watakaojaribu kuyapinga hawatapata uungwaji mkono wa kutosha na jamii yao.

Hii inakuwa dhahiri katika jamii mbalimbali kwani kushamiri kwa jambo lolote kunahitaji watu wa kulitekeleza na ikiwa watalipinga basi halitaweza kuwepo.

Changamoto za kisiasa, kijamii na kiuchumi ambazo Tanzania tunazipotia kwa Sasa zikiwemo Madai ya marekebisho ya katiba, kero za tume na madai ya tume huru ya uchaguzi pamoja na mahusiano mabaya baina ya wanasiasa wa vyama vya siasa, ambayo mimsingi yamekuwa tishio kwa amani yameendelea kudumu kutokana na mtazamo hasi miongoni mwa wanajamii dhidi ya mambo hayo.

Kwani ikiwa lipo hitaji la katiba, kuna tatizo gani kulikamilisha? ama kama halipo hitaji la katiba hiyo kwanini suala hili liendelee kuwa mjadala kwa taifa? au kama kazi za mahakama zetu na tume zetu za uchaguzi ziko huru na zinatenda haki kwanini kuendee kuwa na madai ya vyombo hivyo kuhusishwa na Michuano ya walio katika vyama vya siasa? na kama hayo madai ni ukweli, kwanini marekebisho ya kasoro hizo yasifanyike?

Jamii ikiamua vema na ikashikilia inachokiamini katika kweli ya fikra zao wakiwa huru dhidi ya mihemko ya kisiasa kwa milengo ya vyama vyao, ama maslahi yoyote binafsi wakapaza sauti dhidi ya mambo yasiyofaa na wakataka yanayohitajika kwa njia ya kisheria, hakuna maovu yanayoweza kudumu katika jamii hiyo.

Kudumu kwa matatizo ama maovu yoyote katika jamii ni ushahidi tu kuwa katika jamii hiyo wapo watu wanayaunga mkono aidha wanamanufaa na maovu hayo kwa namna hii ama ile na pengine jamii wanakuwa wameshaiandaa kutokutilia mkazo mambo muhimu yanayowagusa ili wale wanayonufaika nayo waendelee kutimiza yale wanayoyakusudia.

Paulo Freire, Mwanafilosofia wa zamani wa Ulaya ya Magharibi, mbobezi na Mwanaharakati aliyekuwa mhamasishaji wa ubora wa elimu aliamini kuwa mfumo wa elimu ndio unaoandaa jamii iwe ya namna gani na kwamba mtu akitaka kuharibu ama kutengeneza jamii anashughulika na mfumo wa elimu ili iendane na namna anavyotaka jamii iwe.

Freire, katika falsafa yake ya elimu alibainisha kuwa, Elimu ya ukombozi wa jamii ni ile inayotakiwa kuwaandaa wale anaoipata wawe watu wa kujiamini, kudadisi mambo muhimu yanayowagusa na kukataa yale yasiyofaa na si ile inayowandaa watu kuwa watu wasio hoji, wafuasi wa waliofanikiwa wasioweza kudadisi wala kukosoa Mambo yanayoathiri maisha yao wenyewe.

Mwanafilosofia huyo alilaani tabia ya watawala wabinafsi wanaoangamiza mataifa yao kwa kuandaa jamii kuwa ya watu waliokufa kifikra kupitia mifumo ya elimu inayowaandaa kutii kila Jambo na kuendelea kuwa wafuasi tu wa walio na mamlaka ili wao waendelee kutawala na kufanya watakavyo kwa jamii hiyo na isiwape usumbufu kwakuwa wameshaiandaa.

Freire aliyataja masomo ya sayansi ya jamii kama historia, uraia, siasa na fasisi kuwa masomo muhimu katika kuandaa jamii yenye kutambua mifumo ya maisha yao na kuweza kuwa wadadisi.

Kwa mawazo ya Mwanafilosofia huyu tunajifunza kuwa Watawala wabinafsi, wasioangalia Kesho bali wanatazama kipindi chao na nafasi zao pekee huandaa mfumo wa elimu ambao unaifanya jamii iwe ya kuwatii pekee na kutokudadisi mambo wakati watawala wazalendo wanaotazama kesho ya Taifa lao hutumia mfumo wa elimu kutengeneza kizazi Cha watu jasiri, waelewa wa mambo wenye uwezo wa kuhoji, kudadisi na kuibua fikra kinzani dhidi ya maovu yaliyopo katika jamii na kichagiza mabadiliko ya maisha ya jamii za watu.

Kutokana na kudumu kwa madhila yanayoumiza jamii, pengine tunapaswa kuitazama mitaala ya elimu yetu pia na kuona kama inabeba dhamira ya kweli ya ukombozi wa kifikra kwa jamii zetu, na njia rahisi ya kuitazama elimu yetu ni kuwatazama wale walioipata jinsi wanavyotoa majawabu na misimamo katika maswala yanayoibua utata katika jamii zao.

Nami naamini, ikiwa jamii itaacha Unafiki, kila mmoja kwa nafasi yake akaukana ubinafsi, akakataa kununuliwa na akasimama na kweli anayoiamini kadiri ya ufahamu wake, walio mamlakani vivyo hivyo kwa nafasi zao wakatenda na elimu yetu ikatazamwa kwa namna hiyohiyo, maovu hayawezi kudumu bali tutakuwa tukiyatatua kadiri yanavyotokea na si kudumu na tatizo moja miongo kadhaa kwani kudumu kwa tatizo ni tishio kwa amani ya Kesho kwani ipo siku wale wanaoumizwa watatumia nguvu kama wanayoitumia wale wanaowaumiza katika kutafuta ahueni.
 
Upvote 1
Back
Top Bottom