Tuboreshe Utendaji wa Serikali za Mitaa ili kuleta Tija

Tuboreshe Utendaji wa Serikali za Mitaa ili kuleta Tija

idoyo

JF-Expert Member
Joined
Jan 13, 2013
Posts
3,051
Reaction score
1,416
tz-07.png


Kumekuwa na tabia ya kuunda mikoa mipya (na hata wilaya) kwa kigezo cha kusogeza huduma kwa wananchi. Tunafanya hivi kwa sababu hatuzingatii utendaji wa tamisemi. Tamisemi zilianzishwa kwa makusudi ili kusogeza huduma karibu zaidi lakini hazifanyi kazi ipasavyo. Tuboreshe muundo kama ifuatavyo:

1) Mkoa
Tuwe na mikoa 17 + Makao Makuu (kwa Tanganyika) na 2 + Makao Makuu (kwa Zanzibar). Mikoa itakuwa kiunganishi kati ya serikali kuu na tamisemi; katika mikoa hii kuwe eneo la serikali kuu ambapo huduma zote za kiwizara na taasisi zake zitapatikana. Hii itapunguza watu kwenda Makao Makuu, itaokoa gharama na muda, na itaongeza matumizi ya serikali ambayo yatachochea maendeleo kwenye mikoa. Mikoa hii isimamiwe na wakuu ambao watachaguliwa na wananchi, pamoja na viongozi wengine, kwenye uchaguzi wa tamisemi: kwa maana ya Mkuu Wa Mkoa, Diwani, Wenyeviti wa Mashina, na Wajumbe wa Nyumba 10. Mtendaji mkuu wa mkoa ataajiriwa kulingana na vigezo, na atahudumu kwa kipindi kisichopungua uhai wa serikali (kwa sasa miaka mitano).

2) Wilaya
Tuwe na wilaya za kutosha katika mikoa kwa kigezo cha eneo. Wilaya hizi zitasimamiwa na Mkuu wa Wilaya ambaye atateuliwa na Mkuu wa Mkoa kwa kushauriana na waziri mwenye dhamana ya tamisemi. Mtendaji mkuu wa wilaya ataajiriwa kulingana na vigezo, na atahudumu kwa kipindi kisichopungua uhai wa serikali (kwa sasa miaka mitano). Chombo muhimu katika maamuzi kwenye wilaya kiwe ni Baraza la Madiwani ambalo litaunda halmashauri katika wilaya husika. Madiwani wawe ni wasomi na wenye uelewa wa mambo kwa kuwa kuna masuala makubwa ya kujadili kuhusu wilaya zao (hata kama watakuwa na wasaidizi). Huduma muhimu zitapatikana katika wilaya; mwananchi ataenda mkoani endapo tu kuna suala la ulazima. Hivyo kuwe na watendaji wa kutosha kwa ngazi ya wilaya watakaoshughulikia masuala ya wananchi.

3) Kata
Hapa ndipo muhimu maana ni karibu zaidi na wananchi kuliko huko juu. Mfumo wa uendeshaji wa kata uliopo sasa ni mzuri isipokuwa kunakuwa na uingiliaji mkubwa kutoka serikalini, kitendo kinachokwamisha utekelezaji wa majukumu. Kuwe na ofisi ya diwani kwa ajili ya kusikiliza kero za wananchi mara kwa mara (ikumbukwe ofisi ya kudumu ya diwani itakuwa halmashauri). Kuwe na maafisa wafuatao: Afisa Mtendaji ambaye ni mtendaji mkuu wa kata, Afisa Maendeleo ya Jamii kwa ajili ya maswala ya kijamii, Afisa Elimu, Afisa Biashara na Kodi kwa ajili ya usajili na ufuatiliaji wa biashara, Afisa Mipango Miji kwa ajili ya ardhi, ujenzi na miundombinu, na Afisa Kilimo (kwenye kata za kilimo, ufugaji, misitu, au uvuvi), n.k. Kwa sasa kata zina baadhi ya hawa maofisa lakini hawafanyi kazi kwa kuwa wananchi wengi wanalundikana wilayani/halmashauri kwa maswala madogo ambayo yangemaliziwa kwenye kata. Wananchi wamalize kero zao kwenye kata kadiri inavyowezekana, na kata ziwe na watendaji full time. Kata zikifanya kazi vizuri hatutaangaishwa na idadi ya watu katika uundaji wa mikoa au wilaya.

4) Mtaa
Hiki ni kiungo muhimu kutoka ngazi ya chini kwenda juu. Mitaa itasimamiwa na wenyeviti na/au watendaji. Watakuwa ni watu muhimu katika kusikiliza wananchi, kukusanya kero, kukagua maendeleo, na kutambua masuala muhimu ya kufanyia kazi. Watafanya kazi kwa karibu na wajumbe wa (5) Shina (nyumba 10) ambao wanawajua vizuri watu wao, makazi, na mitaa wanayoishi.

Nchi nyingi zilizoendela zina muundo thabiti wa serikali za mitaa. Serikali kuu inazitegemea sana katika kutekeleza miradi ya maendeleo. Hapa kwetu tunalalamika sana maana kila kitu ni mpaka "rais au waziri aseme", yani mpaka mbunge anaililia serikali kuu anasahau majukumu yake. Halafu wananchi waache kutengeneza "miji mipya" maporini na kuachi miji inliyojengeka, hii inasababisha utoaji wa huduma kuwa mgumu.
 
Back
Top Bottom