Vilio mgomo NMB
na Mwandishi Wetu
Tanzania Daima~Sauti ya Watu
WAFANYAKAZI wa Benki ya Makabwela (NMB) wa nchi nzima jana walianza kufanya mgomo wao uliosababisha kusitishwa kwa huduma zote za kibenki.
Hatua hiyo ya wafanyakazi wa benki hiyo kubwa kimtaji na kimtandao kuliko benki nyingine zote, ikiwa na jumla ya matawi 121 nchi nzima, ilisababisha mtikisiko mkubwa ndani ya uongozi wa taasisi hiyo.
Mgomo huo wa kwanza wa kihistoria nchini, ulisababisha matatizo makubwa miongoni mwa wateja wa benki hiyo ambao wengi wao ni wafanyakazi wa kada ya chini na ya kati katika taasisi za umma na sekta binafsi.
Aidha, hatua hiyo ya wafanyakazi hao kugoma ambayo inaweza ikawa imesababisha hasara ya mamilioni ya shilingi kwa benki hiyo, imewasababishia matatizo makubwa ya kifedha wafanyabiashara wa maeneo mbalimbali nchini.
Katika maeneo mbalimbali nchini, makundi ya wateja yalionekana kuwapo kwenye foleni kuanzia mapema asubuhi, huku baadhi yao wakiwa hawana taarifa za kuwapo kwa mgomo huo.
Wakati huo wote wateja hao walishikwa na butwaa wakati wakiwaona wafanyakazi wachache walikuwamo ndani ya matawi hayo, wakiwa wamekaa pasipo kutoa huduma, huku wengine wakisoma magazeti.
Hata mashine maalumu za kutolea pesa (ATM) kwenye matawi mengi nchini, hazikufanya kazi, wakati katika matawi mawili ya Bank House na Mtaa wa Samora ya jijini Dar es Salaam, mashine hizo zilianza kufanya kazi kuanzia saa 10:58 asubuhi.
Tangu asubuhi mashine hizo zilionekana zikiwa na maandishi yaliyosomeka: "Samahani, mashine hii haitumiki kwa sasa, tafadhali jaribu tena baadaye."
Wakizungumza na Tanzania Daima, kwa nyakati tofauti, wateja waliofika katika matawi hayo walieleza kusikitishwa na kitendo kilichofanywa na serikali kutomaliza tatizo hilo mapema.
Miongoni mwa wateja walioeleza wasiwasi wao kuhusu hali hiyo ni wafanyakazi wa serikali na taasisi za umma ambao wanachukua mishahara yao kupitia katika benki hiyo.
Mmoja wa wateja wa benki hiyo wa jijini Dar es Salaam alisema tukio hilo linapaswa kuwa fundisho kwa serikali ambayo inapaswa kuanza kugawa mishahara ya wafanyakazi kupitia katika benki nyingine mbali ya NMB.
Mteja mwingine aliyejitambulisha kwa jina moja la Mama Rose, akiwa nje ya makao makuu ya benki hiyo jijini Dar es Salaam, aliiambia Tanzania Daima kuwa yeye ameathirika kwa mgomo huo, kwani alikuwa na shida muhimu iliyohitaji fedha alizotarajia kuzitoa katika tawi hilo.
Katika Tawi la Barabara ya Morogoro jijini, watu kadhaa walionekana kuchanganyikiwa, wasijue la kufanya walipoona milango ya benki hiyo ikiwa imefungwa.
Bakari Msele, mmoja wa wateja wa benki hiyo, aliitaka serikali iharakishe kutatua mgogoro huo, kabla hali haijabadilika na kuwa mbaya zaidi.
Kizaazaa cha mgomo huo, hakikuishia jijini Dar es Salaam pekee, kwani huko Arusha, wateja wengi walishinda kwenye matawi ya NMB wakisubiri huduma bila mafanikio.
Katika tawi la NMB la Clock Tower, milango ilikuwa imefungwa huku kukiwa na bango lenye maandishi yasemayo:
"Tunasikitika kuwaarifu wateja wetu kwamba tawi letu limefungwa leo, tunaomba radhi kwa usumbufu wowote utakaojitokeza, asanteni."
Kutokana na hali hiyo, wateja wengi walijikuta wakirejea majumbani mwao bila kupata huduma huku ATM zikiwa haina fedha.
Mteja John Simon, baada ya kuona hali hiyo, aliangua kilio huku akisema ana matatizo makubwa kutokana na mtoto wake kulazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha na alikuwa anahitaji fedha kwa ajili ya matibabu yake.
Huko Babati inaripotiwa kuwa, Jeshi la Polisi liliweka ulinzi mkali katika maeneo yanayolizunguka jengo la Benki ya NMB ili kuzuia vurugu kutoka kwa wananchi waliokuwa na hasira baada ya kushindwa kupata huduma za kibenki katika tawi hilo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Luther Mbuttu, alisema jeshi hilo limelazimika kuimarisha ulinzi kutokana na wananchi wengi kuwa na hasira na kuamua kulizunguka jengo la benki hiyo.
"Ni kweli polisi imethibitisha kuwepo kwa mgomo ila tumeimarisha ulinzi ili kuhakikisha hakuna vurugu yoyote itakayotokea," alisema Mbuttu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa TUICO, Boniface Nkakatisi, alisema chama hicho kiko tayari kuwalipa mishahara wafanyakazi wote wa NMB kama serikali itashindwa kufanya hivyo.
Alisema hatua hiyo imefikiwa baada ya serikali kushindwa kukubaliana na masharti waliyowekeana na wafanyakazi kabla ya benki hiyo kuuzwa.
"Sisi tunasema kwamba, hatushindwi kuwalipa mishahara kama serikali ikishindwa kusaini mkataba wetu. Haya tulikubaliana lazima tuone haki inatendeka," alisema Nkakatisi.
Alisema wakati wote wa majadiliano, serikali iliwakilishwa na wanasheria wake ambao waliafikiana na kila kipengele kilichokuwa kwenye mkataba huo.
"Napenda kuwaambia hapa serikali imejaribu kuvuta kamba, sasa hatuachi mpaka kieleweke… lazima tuhakikishe kwamba tunapata haki zetu za msingi kama tulivyokubaliana kwenye mkataba wetu,"alisema Nkakatisi.
Alisema jambo kubwa linalozusha hofu kwa wafanyakazi ni kitendo cha kuuzwa kwa benki hiyo kwa mwekezaji mpya ambaye wanaamini kama hawatalipwa mafao yao sasa, wanaweza kuyakosa baada ya kuingia.
"Hatuwezi kukubali huyo mwekezaji aingie kabla hatujalipwa mafao yetu, tunaweza kuyakosa kwa sababu kila mwekezaji anakuja na sera zake. Hapa kuna hatari wafanyakazi wenzetu wakapoteza kazi," alisema Nkakatisi.
Alisema mgomo wa wafanyakazi katika benki hiyo umesababishwa na kundi fulani la watu ndani ya serikalini ambao wana ajenda ya siri juu ya wafanyakazi hao.
Hali hiyo ya mambo ilisababisha Mkurugenzi Mtendaji wa NMB, Ben Christiaanse, kuitisha mkutano wa dharura na waandishi wa habari na kueleza namna hatua hiyo ya wafanyakazi ilivyosababisha, na itakavyosababisha madhara makubwa.
Christiaanse alisema mbali ya kuitia hasara kubwa benki hiyo ambayo hakuitaja, mgomo huo unaweza kusababisha matatizo makubwa kwa wafanyakazi wanaopokea mishahara yao kupitia NMB.
"Tumepata hasara kubwa kifedha, lakini hasara kubwa zaidi ni ya kupoteza imani kwa wateja wetu.
'‘Maelfu ya Watanzania leo wanahangaika kupata huduma zetu kwa sababu ya mgomo huo. Hiyo ni hasara kubwa zaidi," alisema.
Hata hivyo mkurugenzi huyo alisema hatua hiyo ya wafanyakazi imesababisha hali ya ulinzi na usalama katika benki hiyo kwa matawi yake yote nchini kuimarishwa.
Mkurugenzi huyo alisisitiza kuwa uongozi wa benki hiyo umeshtushwa na mgomo huo kwa madai kuwa, njia waliyotumia wafanyakazi hao kushinikiza madai yao ni kubwa na athari zake ni mzigo kwa NMB.
"Sijui mgomo huo utaisha lini, lakini binafsi napenda uishe hata sasa ila inategemea jinsi serikali itakavyoharakisha kumaliza malalamiko yao," alisema.
Mkurugenzi huyo alifafanua kuwa, wafanyakazi hao hawajagoma kutokana na mishahara midogo, bali mafao yao waliyoahidiwa na serikali kwa mujibu wa mikataba yao.
Alisema kwa nyakati tofauti, kwa siku nzima ya jana alikuwa na mazungumzo na uongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO), pamoja na serikali kwa nyakati tofauti na kwamba wafanyakazi wameonyesha msimamo wa kutorejea kazini.
Katika hatua nyingine, uongozi wa NMB umekwenda mahakamani kutaka viongozi wa TUICO waliochochea mgomo huo, wachukuliwe hatua kwa madai ya kukiuka amri halali ya mahakama.
Uongozi huo kupitia wakili wao, Rosan Mbwambo, uliwasilisha ombi hilo katika Mahakama Kuu jana la kutaka viongozi wa TUICO wakamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria kwa madai kuwa kuna ombi la mahakama lililozuia kufanyika kwa mgomo huo hadi hapo litakapotolewa uamuzi.
Mwanasheria huyo aliwaambia waandishi wa habari kuwa, ombi hilo lipo mahakamani hapo kuanzia Januari mwaka huu na hadi sasa halijatolewa uamuzi, hivyo kitendo cha TUICO kutaka wafanyakazi wa NMB wagome ni cha kuvunja amri ya mahakama.
Aliwataja viongozi wa TUICO ambao leo wanatakiwa mahakamani kutoa utetezi wao kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria kuwa ni Katibu Mkuu, Boniface Nkakatisi, Naibu Katibu Mkuu, Alquine Senga, Mwenyekiti wa NMB tawi la TUICO, Kamati ya Majadiliano na Abdallah Kinenekejo.
Kwa mujibu wa amri ya Mahakama Kuu iliyotolewa na Jaji Mwipopo, ilisema amri hiyo inawataka wahusika wafike mahakamani na kujieleza kwanini wasichukuliwe hatua.
Samansi ya amri hiyo, ilitolewa kidharura na kwa faragha bila upande wowote kuwapo mahakamani hapo na wahusika pia walipewa kidharura.
Habari hii imeandaliwa na Daniel Misheto, Kulwa Karedia, Happy Katabazi, Hamida Khalid, Richard Mwangulube na Deogratius Temba.