SoC02 Tuhifadhi Mazingira

SoC02 Tuhifadhi Mazingira

Stories of Change - 2022 Competition

Mayonga

New Member
Joined
Sep 11, 2022
Posts
2
Reaction score
2
Habari,

Ninayo heshima kubwa kuchapisha maoni yangu kuhusu kuhifadhi mazingira.

TUHIFADHI MAZINGIRA KWA MAENDELEO ENDELEVU

Dhahania
Nikukaribishe mpenzi msomaji katika makala hii muhimu yenye lengo la kufikisha ujumbe kwa jamii, utakaochochea mabadiliko chanya yatakayosaidia katika kuhifadhi mazingira. Uchambuzi huu unaanza kwa kutoa tafsiri fupi ya mazingira na nafasi yake katika kuwezesha ustawi wa bayoanuai, na kisha kuendelea kwa kuelezea namna na sababu zinazoyaharibu pamoja na athari zitokanazo na uharibifu huo, na hatimae kumalizia kwa maelezo juu ya umuhimu wa kuyahifadhi na njia za kufanya hivyo. Karibu ufuatane name hadi mwisho wa makala hii.

Mazingira na nafasi yake kwenye maisha
Neno ‘mazingira’ linafafanuliwa katika mtandao wa “Wikipedia” kuwa ni “jumla ya mambo yote yanayomzunguka kiumbe katika maisha yake”, na kwamba “Mazingira huweza kuundwa na vitu mbalimbali; yanaweza kuwa ya asili (kama misitu, milima, maziwa, mabonde, mito, bahari, n.k.) au ya kutengenezwa na binadamu (kama majengo, viwanda, n.k.)”. Hivyo ni dhahiri kuwa mazingira yanayo nafasi muhimu sana katika maisha ya binadamu na viumbe vyote kwa ujumla.

Mazingira ‘hubeba’ mifumo anuwai ya kiikolojia, ambapo viumbehai vinakuwa katika mitandao thabiti ya kutegemeana, huku vikijipatia mahitaji ya kuwezesha ustawi wao. Binadamu nasi, kama ilivyo kwa viumbehai vingine, tumo katika mchangamano huo, na tunautegemea moja kwa moja. Mazingira yetu ndio msingi wa ustawi wetu, zikiwemo pia shughuli zetu katika nyanja mbalimbali. Kimsingi, maisha yetu hayawezekani bila ya kuwa na mazingira bora yenye mifumo ya kiikolojia iliyo hai na thabiti muda wote. Namna tunavyoharibu mazingira

Wakati tukiendelea kunufaika kutokana na mazingira, yatupasa pia kutafakari mambo muhimu kuyahusu. Kwani, ukweli ni kwamba, kati ya viumbehai vyote, ni sisi binadamu pekee tuliojaaliwa utashi, ambao, pamoja na mambo mengine, tunaweza utumia katika kuvitawala viumbe vyote vingine na hata mazingira kwa ujumla. Kutokana na utashi huu, tunafanya shughuli mbalimbali kwenye mazingira kujipatia mahitaji. Ila jambo la kusikitisha ni kuwa, karibu muda wote, matokeo ya shughuli zetu hizo huchangia sana katika kuyaharibu mazingira.

Tunayaharibu mazingira kupitia mambo kama: ukataji wa miti kwa ajili ya kupata mbao, kuni na mkaa, nguzo za umeme, malighafi za karatasi, n.k.; uchomaji wa misitu na uoto mwingine wakati wa kupanua maeneo ya uzalishajimali, na uvunaji wa bidhaa za misitu; uchafuzi wa hewa kutokana na moshi unaotolewa kutoka kwenye viwanda, vyombo vya moto na migodi; uchafuzi wa ardhi kutokana na uzalishaji na utupaji mkubwa wa taka ngumu, kuyataja machache.

Athari za uharibifu wa mazingira
Kutokana na uharibifu huo, mazingira na mifumo yake vimeendelea kuathirika sana. Pengine mingongoni mwa athari maarufu zaidi ni ile ya ‘Mabadiliko ya Tabia Nchi’, ambayo inajumuisha mambo kama Mabadiliko ya Hali ya Hewa, Athari ya Kivungulio, kuongezeka kwa Joto Wastani la Eneo na Kupanda kwa Kiwango cha Maji Baharini. Athari nyingine ni Ukame, Mafuriko, Majanga ya Asili kama Vimbunga na Matetemeko ya Ardhi, Mmong’onyoko wa Ardhi, Ardhi kupoteza Rutuba, kutoweka kwa viumbehai, njaa, migogoro, pamoja na kuzuka kwa magonjwa.

Katika kuzungumzia miongoni mwa athari hizi, tovuti ya Shirika la Kimataifa la Kulinda Viumbehai (WWF) inaeleza “Kuongezeka kwa Joto Duniani kuna uwezekano mkubwa wa kuwa sababu kuu ya kutoweka kwa viumbehai zama hizi”, na kwamba “ikiwa Joto la Wastani la Dunia litaongezeka zaidi ya nyuzi 2 basi Mifumo mingi ya Kiikolojia itataabika”. Inaongeza pia kuwa “Vingi kati ya viumbe vilivyo katika hatari ya kutoweka vinapatikana katika maeneo ambayo yataathirika pakubwa na Mabadiliko ya Tabia Nchi”, na, “Mabadiliko hayo yanatokea haraka sana kwa viumbehai vingi kumudu kuendana nayo”.

Tukiangazia suala hili tokea katika kanda zinazotuzunguka (yaani, Pembe ya Afrika, Bode la Ufa, Nchi za Maziwa Makuu na maeneo ya Kusini mwa Jangwa la Sahara), uharibifu wa mazingira umekuwa ukishuhudiwa kutokana na athari zinazojumuisha: Kubadili vipindi, viwango na misimu ya mvua; Kupanda kwa joto wastani, kurefuka kwa vipindi vya ukame na kuongezeka kwa maeneo yenye jangwa; Kuzuka na kujirudia kwa majanga ya uvamizi wa nzige na wadudu wengine waharibifu;Kuzuka kwa magonjwa yanayohusishwa na mabadiliko katika mazingira; pamoja na athari nyingi nyingine.

Kwanini tuhifadhi mazingira
Kama tulivyoona katika utangulizi, mazingira yanayo nafasi muhimu sana kwenye maisha yetu ya kila siku. Maisha hayawezi kuwepo bila ya mazingira bora na mifumo hai ya kiikolojia. Kwani, uwepo wa usawaziko katika mifumo hiyo ndio hupelekea usafishaji wa maji tunayotumia, uchujajiwa hewa tunayovuta, utunzaji wa ardhi tunamoishi na kujipatia rizki, urekebishaji wa majira na hali ya hewa kwa ujumla, na pia kuwezesha mzunguko mzuri wa virutubisho baina ya bayoanuai na mazingira yao. Tunapaswa tuwe makini katika kuhifadhi mazingira kwa sababu shughuli zetu mbalimbali kwa asili huchangia katika kuyaharibu, na kutokana na uharibifu huo, shughuli hizo nazo huathiriwa Hivyo, hatunabudi kuhifadhi mazingira ili nayo yaendelee kuwezesha maisha yetu. Na jambo la kutia moyo ni kuwa, mazingira yenyewe bila ya kuingiliwa na binadamu yanao uwezo wa kipekee wa kujirekebisha yenyewe kupitia mifumo yake!

Tufanye nini kuhifadhi mazingira
Kwa kuzingatia hali halisi ya maisha na aina ya mazingira yapatikanayo katika maeneo yetu tajwa, makala hii inapendekeza kutumia njia zifuatazo katika kuhifadhi. Nazo ni: Kupunguza, kutumia tena na kurejeresha vitu mbalimbali tunavyotumia; Kupanda miti kwa ajili ya chakula, kivuli, kusafisha hewa n.k; Kutunza vyanzo vya maji na kupunguza matumizi yake kadri iwezekanavyo; Kujitolea kushiriki katika kampeni za utunzaji mazingira katika ngazi mbalimbali; Kuunga mkono miongozo ya uhifadhi inayotolewa na mamlaka mbalimbali, kama ule wa kuachana na matumizi ya mifuko ya plastiki; Kuzingatia matumizi ya bidhaa zinazodumu ili kuepuka kuzinunua mara kwa mara; Kuchagua kutumia bidhaa ambazo madhara yake ni madogo kwa kadri iwezekanavyo; Kuepuka matumizi ya usafri binafsi na kutumia usafiri wa umma badala yake; pamoja na nyingine nyingi ambazo makala hii haijaweza kuzigusia.

Hitimisho
Tahmini hii fupi, pamoja na maono ya kujali niliyonayo kuyaelekea mazingira na ustawi wake, ndivyo vilivyonichagiza kuamua kutumia jukwaa hili kufikisha ujumbe huu kwa jamii, ili uweze kuongezea nguvu katika harakati mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa ili kunusuru mazingira, mifumo ya ikolojia, pamoja na bayoanuai. Hivyo, chapisho hili nalitoa liwe changamoto kwa kila mtu kwa nafasi yake pamoja na jamii nzima kwa ujumla, kuchukua hatua stahiki katika kutekeleza wajibu huu.

Nina Imani hadi kufikia hapa utakuwa umeelimika na kuhamasika vya kutosha, na utawajibika na kuwa balozi mzuri wa harakati mbalimbali zilizo na lengo la kuhifadhi mazingira na kunusuru maisha. Shime nikuombe uwe hivyo!

Wako katika kutunza mazingira,
Fadhili Ally Nyamadyaki.
 

Attachments

Upvote 1
Back
Top Bottom