Tukatae uhuni kama wa Operesheni Snow White!

Tukatae uhuni kama wa Operesheni Snow White!

kalulukalunde

JF-Expert Member
Joined
May 27, 2016
Posts
1,056
Reaction score
1,083
TUKUMBUSHANE kuhusu kile kilichoitwa Operation Snow White ndani ya Kanisa la Scientology. Kanisa la Scientology lilifanya uamuzi wa siri wa kuunda mtandao duniani ili kujihami na kashfa zilizokuwa zikilielemea miaka ya 1970.

Operesheni hii ilihusisha mbinu za uhalifu ili tu kulinusuru kanisa hilo pamoja na mwasisi wake Ron Hubbard. Ni operesheni iliyohusisha mtandao wa kanisa hilo kujipenyeza katika taasisi 136 binafsi na za serikali ya Marekani na ofisi za balozi nje ya nchi hiyo. Taasisi yoyote iliyobainika kuwa hatari kwa kanisa hilo ilipenyezewa wanamtandao. Nchi zaidi ya 30 duniani ziliguswa katika njama hiyo kubwa kuwahi kutokea duniani.

Wizi wa nyaraka mbalimbali ulifanywa, unasaji wa sauti na hata utengenezaji wa nyaraka feki ulifanyika ili kukidhi malengo ya mtandao huo.

Kazi hiyo ilianza mwanzoni mwa miaka ya 1960 na Ron Hubbard, mwanzilishi wa kanisa la Scientology ndiye aliyependekeza kuundwa kwa mtandao wa kuhami kanisa lake – mtandao ulijipenyeza kupitia kazi mbalimbali za kitaaluma serikalini au popote, kazi kama za ukatibu muhtasi, ulinzi wa viongozi na nyinginezo.

Ofisi maalumu katika kufanikisha mpango huo zilifunguliwa maeneo mbalimbali Marekani na Uingereza.

Mwishoni mwa mwaka 1973, mtandao wa kanisa hilo ulianza kujipenyeza katika serikali mbalimbali duniani, japokuwa lengo kuu la uamuzi huo ilikuwa kujipenyeza ndani ya Marekani. Na zaidi, katika kuhofia kuporomoka kwa hadhi ya kanisa hilo, ilibidi mtandao ujipenyeze katika polisi wa kimataifa, Interpol, ili kunasa na kudhibiti nyaraka zilizohusu maovu yao.

Kati ya mlengwa namba moja wa operesheni Snow White ni mwanahabari Paulette Cooper. Operesheni hii ilimlenga kiasi cha kuibuka kwa operesheni nyingine kama Operation Freakout dhidi yake. Kilele cha operesheni hiyo dhidi ya Paulette kilikuwa ni kuibua matokeo kwamba mwanadada huyo aonekane kichaa na kutunzwa kwenye hospitali maalumu za vichaa au anafungwa jela. Operesheni ilitakiwa kutengeneza mazingira yatakayotoa matokeo hayo.

Kwa nini Pauelette Cooper? Kilichomponza ni kufichua uhalifu wa kanisa hilo. Cooper alianza uchunguzi wake mwaka 1968 na kuandika makala iliyofichua uchafu wa kanisa hilo mwaka 1969.

Mbinu mbalimbali zilitekelezwa kumshughulikia Paulette ikiwamo ile ya kutumia asili yake ya Uyahudi kumchonganisha na nchi za Kiarabu na kumchonganisha na aliyekuwa rais wa Marekani wakati huo, Gerald Ford, sambamba na aliyekuwa waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Henry Kissinger ambaye naye ana asili ya Uyahudi.

Kama ilivyoeleza juu, operesheni Snow White katika utekelezaji wake ikazaa Operation Freakout. Operation Freakout ikamuibua mwanamke aliyeigiza sauti ya Paulette Cooper, akapiga simu ubalozi mdogo wa uarabuni New York na kutoa vitisho huku mazingira mahsusi yakitengenezwa kwamba aliyetoa vitisho hivyo ni myahudi.

Na katika mpango mwingine wa kuonyesha Paulette Cooper ametoa vitisho kwa Ford na Kissinger, mpango wa ziada ukafanywa kuhakikisha Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) linapokea taarifa iliyokusudiwa na wana-operesheni – kwamba Cooper ni hatari.

Nifupishe maelezo kwamba Operation Freakout haikufanikiwa. FBI walifanya kazi yao kwa umakini na Julai 8, 1977 walivamia ofisi za kanisa hilo zilizoko Los Angeles na Washington D.C. na kuzoa nyaraka zaidi ya 48,000 zilizokuwa zikieleza namna kanisa hilo lilivyokuwa likiendesha shughuli zake hizo za kihalifu.

Nimerejea mfano huu kwa sababu Rais John Magufuli anapambana na uhalifu na wahalifu waliojificha serikalini na sekta binafsi na taifa linashuhudia kuanza rasmi Mahakama Maalumu ya Uhujumu Uchumi na Ufisadi.

Kama ambavyo operesheni Snow White ilivyokuwa ngumu kuikabili ni vigumu kwa Magufuli kuvunja mtandao wa hujuma za kifisadi utakaotumia mbinu pengine zaidi ya zile za Snow White.

Ili kufikia mafanikio ni lazima mahakama hiyo mpya iundwe sambamba na kikosi kazi maalumu katika ukamataji, upelelezi na uendeshaji wa kesi husika. Kama ilivyokuwa kwa operesheni Snow White kuzaliwa katika sura ya ‘utumishi’ wa Mungu ndani ya kanisa la Scientology ndivyo hivyo ambavyo mitandao ya hujuma inavyoweza kuzaliwa ndani ya mwavuli wa shughuli mbalimbali za kitaasisi katika jamii.

Jambo la kuzingatia hapa ni kwamba, nguvu za hujuma wakati wote huhusisha mtandao mpana na kwa hiyo, vita ya kusafisha nchi si kazi ndogo. Wakati mwingine ni vita yenye kuibua kelele za udikteta. Hii ni vita inayochora mstari kati ya wapambanaji na maadui wa mapambano. Ni vita inayolazimisha mzalendo mmoja kumtafuta mwenzake na kisha wote hao kutafuta wenzao kupigania nchi yao.
 
Back
Top Bottom