Herbalist Dr MziziMkavu
JF-Expert Member
- Feb 3, 2009
- 42,872
- 34,363
Katuni
Serikali imetangaza kuwa kwa mwaka wa fedha wa 2014/15 inakusudia kutumia Sh. 19,853,331,000 (trilioni 19.853) kwa ajili ya shughuli za kawaida na maendeleo.
Kulingana na mgawanyo wa fedha hizo, Sh. trilioni 6.44 ni kwa ajili ya shughuli za maendeleo wakati fungu la kawaida ni Sh. trilioni 13.408.
Bajeti ya mwaka unaokuja wa fedha imeongezeka kwa Sh. trilioni 1.62 ililinganishwa na Sh. trilioni 18.23 za mwaka wa fedha unafikia ukingoji Juni 30 mwaka huu.
Kwa waliomsikiliza Waziri wa Fedha, Saada Salum Mkuya, jana watakubaliana nasi kwamba bajeti inayokusudiwa mwaka wa fedha unaoanza Julai Mosi mwaka huu, haina tofauti kubwa ya kimsingi na ile ya mwaka 2013/14.
Hoja hii inaweza kupanuliwa zaidi na kuelezwa kwamba bajeti hiyo kwa hakika haina kitu chochote kikubwa kipya mbali na mambo ya kawaida ambayo miaka na miaka ndiyo hasa yamekuwa vyanzo vya mapato ya serikali.
Mathalan, bajeti hii imeendelea kujielekeza kwenye nyongeza ya kodi kwenye soka, bia, sigara, pombe kali na mvinyo kama vyanzo vyake vikuu vya kodi. Ni ada, mwaka baada ya mwaka.
Tumemsikia Waziri akiweka mikakati mbalimbali ya usimamizi wa bajeti ikiwa ni pamoja na malipo ya serikali kulipwa kupitia akaunti moja ya serikali iliyoko Benki Kuu; kutenga fedha za kutosha kukidhi maeneo ya vipaumbele; kuanza kwa mfumo wa ununuzi wa pamoja; matumizi ya mashine za malipo za elekroniki; kupiga marufuku maduhulu kutumiwa na wakusanyaji kabla ya kuwasilishwa hazina; kufuta madaraka ya misamaha ya kodi yaliyokuwa mikononi mwa Waziri wa Fedha, pamoja na nyingine nyingi, bado bajeti hiyo imepokewa na hisia kali za kukata tamaa.
Kwa vyovyote vile, bajeti hii haitazamwi kama mkombozi wa watu wanyonge, wananchi wa kipato cha chini, haionyeshi kuwagusa sawasawa wafanyakazi ambao kwa miaka na miaka wamekuwa ndiyo walipaji wakubwa wa kodi za kuendesha serikali huku wenye mapato makubwa kama wafanyabiashara wakitumia mbinu mbalimbali kukimbia wajibu wa kulipa kodi.
Serikali inataja tu kwamba itapandisha mishahara ya wafanyakazi na hasa kima cha chini, inazungumza kuwa itafanya mabadiliko kulingana na hali ya uchumi ya pensheni ya wazee wastaafu wanaolipwa Sh. 50,000 kwa mwezi; lakini pia serikali imesema kuwa imepunguza kodi ya lipa kadri unavyopata (PAYE) kutoka asilimia 13 hadi 12, hatua zote hizi hazionyeshi kama zitaleta nafuu kubwa kwa maisha ya wananchi.
Baada ya kuitafakari kwa kina bajeti ya serikali ya mwaka 2014/15 tumeshawishika kusema kuwa pengine walioiandaa hata hawakukumbuka kwamba mwaka 2015 ni mwaka wa uchaguzi, licha ya ukweli kwamba miongoni mwa malengo yake ni kuanza kuandaa uchaguzi mkuu mwakani.
Ni kawaida kote duniani serikali yoyote inapokwenda kwenye uchaguzi walau kuwa na sura ya kuwakumbuka wananchi wake; kuibua vipaumbele vya kuwakomboa na kubwa zaidi kupunguza kodi ambazo zimekuwa ni mzigo.
Ni kujidanganya kudhani kwamba punguzo la PAYE kutoka asilimia 13 hadi 12 ni utatuzi wa shida za wafanyakazi kwa sababu kimsingi kikubwa ambacho watafanikiwa kuokoa ni watani wa Sh. 5,000 kwa mwezi.
Tumesikia maelezo mengi sana juu ya suala zima la misamaha ya kodi, tumeambiwa mara kadhaa kwamba taifa hili linapoteza matrilioni ya shilingi mwaka hadi mwaka kutokana na misamaha hii; mingi haisaidii siyo kufufua au kuchangamsha uchumi wala kusaidia wananchi kupata nafuu ya kipato, misamaha mingi ama imetumika vibaya na aghalab kutunisha zaidi nguvu za wenye mitaji ughaibuni, huku taifa hili likiendelea kuwa ombaomba.
Tumemsikia Waziri Mkuya akisema kuwa serikali imewasilisha bungeni muswada wa sheria mpya ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa nia ya kupunguza misamaha ya kodi, kuwasilishwa kwa muswada wa usimamizi wa kodi, bado suala la ulipaji wa kodi kwa kampuni kubwa za uwekezaji limekuwa ni tatizo kubwa ambalo linatishia ustawi wa uchumi wa taifa hili.
Pamoja na hoja hizi, tunapongeza hata hivyo uamuzi wa serikali wa kufuta utaratibu wa sasa wa waagizaji wa mafuta ya petroli kulipa kodi siku 45 baada ya kufanyiwa tathmini, na sasa watakuwa wanalipa kabla ya kuanza kuuza bidhaa hiyo. Kama alivyosema Waziri Mkuya hatua hizi zinalenga kuondoa ukwepaji kodi katika biashara ya mafuta.
Tunaamini bajeti ya mwaka ujao wa fedha siyo rahisi hata kidogo, inaweza kabisa ikawa ngumu kuliko hii inayopita, ni rai yetu kwamba serikali sasa itambue kwamba haina njia nyingine ya kukwamua taifa hili hapa lilipo kiuchumi kama siyo kuamua kwa dhati kabisa kupunguza matumizi yasiyokuwa ya lazima kwa vitendo halisi.
Tujifunze kuishi kwa mfumo wa maisha unaofanana na uwezo wetu. Madeni yakiwa mengi ni hatari.
CHANZO: NIPASHE