SoC01 Tukipende kiswahili lakini tusikipuuze kiingereza

SoC01 Tukipende kiswahili lakini tusikipuuze kiingereza

Stories of Change - 2021 Competition
Joined
Sep 6, 2021
Posts
24
Reaction score
111
Na Elivius Athanas.
0745937016.

Ni kweli kuwa Kiswahili kina umuhimu, ni kweli kuwa Kiswahili ni lugha yetu, ni kweli kuwa Kiswahili kinakua.

Ukiulizwa utaje lugha tano (5) zenye wazungumzaji wengi Barani Afrika, huwezi kuacha kukitaja Kiswahili.

Labda tu, mtu mwenye Shahada ya Ubishi ndiye anayeweza akaacha kukiorodhesha Kiswahili miongoni mwa lugha tano zenye wazungumzaji wengi Barani Afrika.

Inakadiriwa kuwa, Kiswahili ni lugha inayozungumzwa na watu zaidi ya milioni miamoja (100) kote Duniani.

Haya ni mafanikio makubwa sana kwa lugha ya kibantu kama Kiswahili kupenya na kukimbizana na lugha zingine za Ulaya na Amerika. Ingekuwa katika kutafuta maisha tungesema Kiswahili ni mpambanaji.

Pamoja na umuhimu wake, matumizi yake na ukubwa wake, bado tuna sababu muhimu za kutokukipuuza Kiingereza hasa katika karne hii ya utandawazi na ushindani.

Makala hii pendwa inajaribu kuchambua na kutathmini kwa kina, sababu kuntu za kwanini tukipende Kiswahili na kwanini tusikipuuze Kiingereza.

Nitaanza kueleza sababu za kwanini tukipende Kiswahili na baadae nitahitimisha na sababu za kwanini tusikipuuze Kiingereza.

KWANINI TUKIPENDE KISWAHILI?

Tuna sababu milioni za kuendelea kukipenda na kukidumisha Kiswahili.

Moja, tukipende Kiswahili kwa sababu ndiyo lugha yetu mama na lugha yetu ya Taifa.
Lazima tuendelee kukipenda Kiswahili kwasababu, hii ndiyo lugha yetu ya mazungumzo.
Mtaani tunazungumza Kiswahili, kanisani kinatumika Kiswahili, sehemu za biashara kinatumika Kiswahili na kadhalika.
Ni lugha yetu ya Taifa. Kiswahili kinatumika sehemu nyingi za Kiserikali na Kitaifa.
Mfano bungeni,kwenye kampeni za kisiasa na kadhalika.
Tukipende Kiswahili.

Pili, tukipende Kiswahili kwasababu ni utambulisho na utamaduni wa Taifa letu.
Kiswahili ndiyo lugha inayoitambulisha Tanzania na watu wake. Ukienda Nchi za nje ukasikika unaongea Kiswahili, ni utambulisho tosha kuwa wewe ni mtoto au mjukuu wa baba Tanzania.
Tukipende Kiswahili.

Tatu, tukipende Kiswahili kwa sababu ni lugha inayoleta umoja wa Watanzania.
Pamoja na makabila yetu mengi, Kiswahili ni lugha inayotuleta pamoja Watanzania.
Tunaongea lugha moja tunaelewana. Lugha moja Taifa moja.

Tukipende Kiswahili.

KWANINI TUSIKIPUUZE KIINGEREZA?

Pamoja na sababu zote hizo nzuri za kukipenda Kiswahili, pamoja na umuhimu wote huo wa Kiswahili, bado tuna sababu muhimu na zenye mashiko za kutokukipuuza Kiingereza hata kidogo.
Katika ulimwengu huu wa sasa, bado Kiingereza kinaonekana kuwa na umuhimu wake katika nyanja mbalimbali za maisha.
Pamoja na uzalendo wangu mkubwa juu ya Nchi yangu na lugha yangu, bado nauona umuhimu wa lugha ya Kiingereza katika ulimwengu huu wa ushindani.
Viongozi, wanaharakati na watu mbalimbali wanapendekeza matumizi ya lugha ya Kiswahili pekee na kusahau ukweli ulio wazi kuwa, katika Ulimwengu huu wa kidijitali na utandawazi, kuna umuhimu sana wa mtu kufahamu lugha ya Kiingereza japo kidogo.

Zifuatazo ni hoja muhimu zinazoonyesha kwanini tusikipuuze Kiingereza.
(Kwanini kuna umuhimu wa kujifunza Kiingereza)

Moja, tusikipuuze Kiingereza kwasababu maelekezo mengi ya matumizi ya dawa na bidhaa yanaandikwa kwa lugha ya Kiingereza.
Nchi nyingi za Afrika ikiwemo Tanzania, ni watumiaji wazuri sana wa dawa na bidhaa kutoka Ulaya na Amerika. Dawa nyingi za watu na wanyama zinatoka nje.
Bidhaa na malighafi nyingi za biashara na viwanda zinatoka Ulaya na Amerika.
Maelekezo ya matumizi ya dawa za watu na wanyama yanaandikwa kwa lugha ya Kiingereza.
Maelekezo ya matumizi ya vipodozi vingi ambavyo vinawaharibu sura dada zetu, vinaandikwa kwa lugha ya Kiingereza.
Bado tunakipuuza Kiingereza?
Baadhi ya madhara, uharibifu na vifo, vimeripotiwa kwa kutokuelewa maelekezo ya matumizi ya dawa na bidhaa ambavyo vinaandikwa kwa Kiingereza.
Bado tunakipuuza Kiingereza?
Ni ukweli usiopingika kuwa, matumizi ya Kiingereza yapo mpaka kwenye vyakula na vinywaji vya kizungu tunavyokula na kunywa. Kujifunza Kiingereza kutatusaidia kujua na kuelewa maelekezo sahihi ya matumizi yake.
Tusikipuuze Kiingereza.

Pili, Kiingereza ndiyo lugha inayotumika ngazi ya juu ya elimu. Vyuo vikuu vingi vya ndani na nje ya Afrika, vinatumia lugha ya Kiingereza katika kufundisha na shughuli zote za kitaaluma.
Ukisikia Mtanzania ameenda Wingereza kusoma Shahada ya Uzamili au Uzamivu, ujue lugha inayotumika huko ni Kiingereza.
Ukisikia vijana wanaofaulu vizuri mitihani yao ya kidato cha sita na kupata udhamini kwenda kusoma nje, ujue lugha ya Kiingereza ndiyo itakayotumika huko.
Hivyo, hatuna sababu kabisa ya kukipuuza Kiingereza katika ngazi ya msingi na sekondari ili atakayefika ngazi ya juu asipate tabu.
Isitoshe, mikutano, uwasilishaji na midahalo ya kitaaluma katika ngazi hii ya elimu, vinafanyika kwa lugha ya Kiingereza.
Bado tunakipuuza Kiingereza?

Tatu, hojaji (interview) nyingi za kazi zinafanyika kwa lugha ya Kiingereza. Wahitimu wengi wa Vyuo Vikuu na Vyuo vya kawaida ambao hawakuwa na msingi mzuri wa Kiingereza, wanapata tabu sana linapokuja suala la hojaji za kazi.
Wahitimu wengi wanakosa kazi kutokana na changamoto ya Kiingereza wakati wa hojaji.
Matumizi ya Kiingereza bado hayakwepeki katika eneo hili.
Vijana wetu hawana msingi mzuri wa lugha ya Kiingereza. Hii huwafanya vijana kutofanya vizuri katika hojaji za kazi.
Tusikipuuze Kiingereza. Tukiendelea kukipuuza Kiingereza, vijana wetu wa Kitanzania wataendelea kukosa kazi kutokana na changamoto ya lugha.
Tukipende Kiswahili lakini tusikipuuze Kiingereza.

Mwisho, Mtanzania kufahamu lugha ya Kiswahili na Kiingereza siyo kosa wala siyo kukosa uzalendo. Kosa ni kukipa kipaumbele Kiingereza badala ya kukipa kipaumbele Kiswahili.
Tukipende Kiswahili lakini tusikipuuze Kiingereza.

Ahsanteni sana.
 
Upvote 2
Wajukuu wa Mzee Tanganyika, tukipende sana Kiswahili lakini tusikipuuze Kiingereza.
 
Back
Top Bottom