- Source #1
- View Source #1
Nmeona tangazo kwenye baadhi ya makundi huko mtandaoni kuwa Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi imetangaza nafasi za kazi kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa.
- Tunachokijua
- Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imeanzishwa kwa mujibu wa ibara ya 74(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Kwa kuzingatia masharti ya ibara ya 74(7) na (11) ya Katiba na kifungu cha 6(1) cha Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 2 ya Mwaka 2024, Tume ni idara huru inayojitegemea na inafanya maamuzi yake rasmi kuhusu utekelezaji wa majukumu yake kwa vikao.
Katika kutekeleza majukumu yake ya kikatiba, Tume haitalazimika kufuata amri au maagizo ya mtu yeyote au idara yoyote ya Serikali au maoni ya chama chochote cha siasa.
Tarehe 27-11-2024 kumepangwa kufanyika uchaguzi wa serikali za mitaa Tanzania bara ambao utahusisha kuchagua viongozi wa serikali za mtaa, vijiji na vitongoji.
Imekuwepo taarifa inayosambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii ikionesha kuwa Tume huru ya taifa ya uchaguzi imetangaza nafasi za kazi kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa
Ukweli upoje kuhusu nafasi hizo za kazi?
JamiiCheck imefuatilia uhalisia wa taarifa hiyo na kubaini kuwa taarifa hiyo si ya kweli, tume huru ya Taifa ya uchaguzi haijatoa tangazo hilo. Utafutaji wa kimtandao umebaini kuwa link inayotumika kuchukua taarifa za watu wanatuma maombi siyo link halisi ya tume huru ya taifa ya uchaguzi kwani haina kikoa (domain) kinachotumika na taasisi za serikali yani .go.tz mathalani link ya taarifa potofu ni https//:cutt.ly wakati kiungo (link) ya Tume huru ya Taifa ya uchaguzi inec.go.tz ikiwa na kikoa (domain) ya .go.tz kuonesha kuwa ni tovuti halisi ya taasisi ya serikali ya Tanzania.
JamiiCheck imebaini pia kuwa tovuti inayotumiwa na wapotoshaji inafanana kimuonekano katika baadhi ya maeneo na tovuti rasmi ya Tume huru ya Taifa ya uchaguzi. Utofauti ni kuwa tovuti ya wapotoshaji ikifunguka moja kwa moja inahitaji kuchukua taarifa binafsi za mtu ambazo wanadai ndiyo maombi ya kazi, lakini pia mahali walipoweka viungo kwa ajili ya taarifa nyingine ukibonyeza hazifunguki ukilinganisha na tovuti rasmi ya Tume huru ya Taifa ya uchaguzi.
Muonekano wa tovuti rasmi ya Tume huru ya Taifa ya uchaguzi, na sehemu ya link ikionesha https://www.inec.go.tz kuthibitisha ni tovuti rasmi ya taasisi ya serikali.
Muonekano wa tovuti isiyo rasmi yenye lengo la kupotosha link yake ikionesha https://tume-huru-ya-uchaguzii.pages/
Tovuti rasmi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi upande wa kulia chini ina logo yao chini kukiwa na maneno yanayosomeka ‘ Kujiandikisha kuwa mpiga kura ni msingi wa uchaguzi bora’, ambapo ni tofauti na tovuti inayofanya upotoshaji.
Muonekano wa tovuti rasmi ya Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi
Muonekano wa tovuti isiyo rasmi ya Tume huru ya Taifa ya uchaguzi
JamiiCheck imefuatilia pia taarifa hiyo katika kurasa rasmi za mitandao ya kijamii ya tume huru ya Taifa ya uchaguzi na kukuta imekanusha taarifa hiyo hapa.