Tume Haki Binadamu(THBUB)
Member
- Sep 17, 2024
- 21
- 16
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Tamko la THBUB kulaani mauaji ya Bw. Jumanne Juma
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Bw. Jumanne Juma (28), aliyekuwa mkazi wa Mtaa wa Kimara B, Wilaya ya Ubungo Jijini Dar es salaam aliyeuawa kwa kuchomwa na mafuta ya petroli na watu aliokuwa akiwafanyia kazi za nyumbani kwa madai ya kuwaibia kiasi cha Shilingi 200,000.
Taarifa kutoka Jeshi la Polisi na vyombo vya habari zinaeleza kuwa watu waliomuua Bw. Jumanne walimfuata nyumbani kwake majira ya saa 4 usiku kumtaka waondoke naye wakamlipe malipo yake pamoja na kumpatia kazi nyingine. Hata hivyo, baada ya kuondoka naye walimpeleka mahali, wakanunua mafuta ya petroli na kumchoma moto.
Katika ufuatiliaji wake THBUB imebaini yafuatayo:-
i) Baadhi ya wananchi bado hawaheshimu Katiba ya nchi kama inavyoelekezwa katika Ibara ya 26 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 pamoja na sheria za nchi na hivyo kujichukulia sheria mikononi;
ii) Vitendo vya mauaji vinavyotokea hivi karibuni vimeambatana na ukatili dhidi ya ubinadamu; na
iii) Kuna viashiria vya wananchi kutokuwa na imani na vyombo vya usimamizi wa haki.
Kutokana na tukio hilo ambalo limesababisha kifo cha Bwana Jumanne Juma, THBUB inapenda kutamka kuwa kitendo hicho ni:
i) Ukiukwaji wa haki ya kuishi kama ilivyotamkwa katika Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na hivyo inalaani vikali vitendo hivyo; na
ii) Ukatili dhidi ya binadamu ambao ni kinyume na Ibara ya 13(6)(e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
THBUB inapenda kuwafahamisha wananchi kuwa madhumuni ya kuwepo kwa utawala wa sheria ni ili kulinda utu wa binadamu na kujenga jamii iliyostaarabika inayothamini haki ya kuishi na haki nyinginezo. Ndio maana nchi imeweka vyombo na mifumo mbalimbali ya kuhakikisha kuwa migogoro yote ambayo haiwezi kusuluhishwa kwa mapatano basi inatatuliwa kwa kufikishwa katika vyombo vya kutoa haki.
THBUB inatambua jitihada zilizofanywa na Jeshi la Polisi kwa kuwakamata watuhumiwa. Pamoja na hayo, THBUB inapendekeza yafuatayo:
1. Jeshi la Polisi Tanzania
■ Liendelee kuchukua hatua mahsusi kuimarisha ulinzi katika maeneo ya wananchi na kuwezesha kupata taarifa za mapema kuhusu kuwepo kwa viashiria vya uvunjifu wa sheria ikiwa ni pamoja na mauaji na vitendo vya ukatili.
Liimarishe ulinzi shirikishi kupitia vituo vya polisi kata kwa kuongeza idadi ya vituo na idadi ya askari ili kuongeza ufanisi.
2. Serikali za Mitaa
Mamlaka za Serikali za Mitaa katika ngazi zote ziwe na mipango madhubuti ya kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo yao.
3. Viongozi wa Dini
Waongeze nguvu katika utoaji wa elimu ya dini na maadili na kukemea uovu unaotokea nchini.
4. Wananchi
Wajenge utamaduni wa kuheshimu sheria za nchi, haki za binadamu, kutafuta namna bora ya kupata suluhu ya migogoro na kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi;
• Washirikiane na vyombo vya dola kufichua maovu kwa kutoa taarifa kwa mamlaka husika ili kuzuia matukio kama hayo kutokea.
5. Asasi za Kiraia na Vyombo vya Habari
Kuendelea kutoa taarifa za matukio ya uhalifu kwa wakati na kushiriki kwa ukamilifu katika kutoa elimu kwa umma kuhusu taratibu zilizopo za namna ya kushughulikia masuala mbalimbali ya kijamii kupitia sheria na hivyo kulinda haki za binadamu na utu wa mtu.
THBUB inatoa pole kwa ndugu, jamaa na wanafamilia waliopoteza mpendwa wao katika tukio hili na inaahidi kuendelea kutoa ushirikiano katika jitihada za kukomesha na kulinda haki za binadamu na misingi ya utawala bora.
Jukumu la ulinzi na utetezi wa haki za binadamu ni letu sote!
Imetolewa na:
Mathew P. M. Mwaimu (Jaji Mstaafu)
MWENYEKITI TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA