Tumemaliza mwaka 2012, tuzingatie haya 2013

Tumemaliza mwaka 2012, tuzingatie haya 2013

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Joined
Feb 3, 2009
Posts
42,872
Reaction score
34,363
NIANZE kwa kumshukuru Mungu kwa kuniwezesha kuumaliza mwaka na kuingia mwingine kwa mafanikio mengi. Sina shaka kuwa wema wake ndiyo ulioniwezesha kupita vikwazo vingi vya kimaisha na hatimaye kuwa mmoja kati ya mamilioni ya waliosherehekea ujio wa mwaka 2013.

Baada ya kusema hayo niingie kwenye mada yangu ya leo kwa kuanza na mifano ya maneno yenye sababu ambazo watu hudhani walikuwa na haja ya kuamua kufanya au kuwafanyia wenzao mabaya. Nililazimika kuwa jambazi kwa sababu ya ugumu wa maisha.

Kwa kuwa maisha yalikuwa magumu na sikuwa na mtu wa kunisaidia, ikabidi nimkubali yule mwanaume, kumbe alikuwa na ugonjwa wa Ukimwi akaniambukiza.

Mara nyingi nilivumilia lakini ukafika wakati na mimi nikaamua kumsaliti ili naye aone uchungu.
Baada ya baba kunifukuza nyumbani nikaingia kwenye vijiwe, nikaanza kutumia dawa za kulevya.

Watu wengi ukiwauliza kwa nini walikosea katika hili na lile watakimbilia kutoa sababu, mara nyingine unaweza kuwapa haki kutokana na uzito wa hoja zao. Lakini ukweli unabaki kuwa maamuzi mabaya yatokanayo na sababu fulani hayabebi uzito wa matukio bali na uelewa mdogo wa mambo wa wahusika wenyewe.

Mpenzi msomaji wangu, hebu jiulize ikiwa sababu ya ugumu wa maisha ndiyo ilikufanya uingie kwenye uhalifu, unadhani shida umekuwa nazo peke yako tu dunia nzima? Kwa nini wengine hawajaamua kuiba pamoja na umaskini walionao?

Jibu ni kwamba wamefikiria vyema zaidi yako ndiyo maana wanavumilia shida zao, wanapambana kutafuta fedha kwa haki, wanajituma katika kazi halali ili waepuke matatizo makubwa zaidi kwenye maisha yao.

Ushauri wangu kwako msomaji wangu ni kwamba ukitaka kuwa mtu mwenye mafanikio kwa mwaka huu, epuka sana kutumia sababu kuamua mambo, badala yake tumia akili yako na uwe tayari kufikiri matokeo kuliko kuhangaika na dalili za tatizo. Ukiona kuna jambo baya limekutokea, jipe muda wa kufikiri na ikiwezekana usiamue chochote mpaka uwashirikishe watu wengine.

Nakushauri pia usitumie sababu kugombana na wenzako kazini, kwenye familia au shuleni. Tambua kuwa ndani ya sababu kuna utashi wako, unaweza kutukanwa ukacheka, unaweza kuwa na dhiki usiibe, unaweza kuwa na tatizo kubwa ukaliona dogo endapo tu utafikiri vyema.

Kinachosikitisha ni kwamba, wengi wetu tumekuwa tayari kuongozwa na nguvu za sababu na kujikuta tunapata matokeo mabaya ambayo hutusababishia kujuta.

Kwa mfano, tunapofanya ugomvi na kujeruhi kisha kupelekwa jela tunakuwa tumepata hasara kubwa ambayo tungeweza kuiepuka kwa kutafakari sababu iliyotusukuma kupigana na hivyo kuamua kuachana na hasira zetu.

Wanasaikolojia wanasema kuwa kinachochochea hamasa za kuitikia sababu ni namna mtu anavyoweza kulichukulia tatizo kwa kulilinganisha na mtazamo wa watu wengine.

Nikinyamaza wakati nimetukanwa matusi ya nguoni, watu si wataniona mimi mnyonge? Ni bora tuonyeshane kazi ili ajue kuwa mimi si mtu wa kuchezewa!

Inaelezwa kwamba, mawazo ya aina hii yakipewa nafasi, sababu huonekana kubwa na isiyovumilika, kumbe sivyo! Busara ni jambo la msingi katika maisha yetu ya siku zote.

Mwisho wa makala hii naomba kuwashukuru sana wasomaji wangu wote ambao wamekuwa nami katika kipindi chote cha mwaka 2012. Niwaombe msiniache mwaka 2013, bali mdumu kuwa nami mkiniombea nami nikiwaombea mema.


MziziMkavu.
 
Back
Top Bottom