SoC02 Tunaishi ili kula au tunakula ili kuishi?

SoC02 Tunaishi ili kula au tunakula ili kuishi?

Stories of Change - 2022 Competition

Laban255

Member
Joined
Jul 20, 2022
Posts
6
Reaction score
1
Wahenga walisema"Kila nabii na zama zake" kila jambo na wakati wake na katika kila zama kuna namna tofauti ya maisha, na namna tofauti ya utafutaji wa mahitaji muhimu ya binadamu. Kila jua linapochomoza asubuhi ni ishara kuwa jambo jipya limezaliwa duniani na kila linapokuchwa binadamu hurejea katika pango lake ambapo mawazo mapya na fikra mpya huzaliwa. Nakumbuka nikiwa darasa la sita mwalimu wa sayansi aliwahi kuuliza kwa nini tunakula? Jibu kubwa lilikuwa ni tunakula ili tuishi bila shaka unajua swali doto ni lipi, ambalo pia mwalimu aliuliza kwa nini tunaishi?. Kwa urahisi kabisa lilijibiwa na mwanafunzi mmoja nyuma ya darasa "tunaishi ili tule". Umewahi kupata majibu ya maswali haya?.

Hivi ni kweli tunaishi ili kula? Yaani maisha maana yake ni kula na kama si hivyo, nini kingine unafaidika au jamii inayokuzunguka inafaidi kupitia uwepo wako katika sayari hii? Suala la kula ili kuishi na kuishi ili kula sikulipatia majibu mapema hadi nilipofanikiwa kupata nafasi ya kujiunga na elimu ya sekondari ambapo nilisoma baiolojia na kujua kuwa kula ni mojawapo tu ya viashiria au sifa za kiumbe anayeishi, sanjari na kula binadamu kama viumbe wengine hujongea, hutoa taka mwili, hukua, huzaliana na kuhisi hivi vinaonesha kuwa binadamu anaishi. Hivyo basi swali sio moja tena, Tunapumua ili?, tunajongea ili? Tunakua ili?, tunazaliana ili? Tunahisi ili? Tunatoa taka mwili ili? kwa majibu yaleyale na mtazamo uleule tungejibu yote haya yapo ili tuishi, ila swali linakuwa upuuzi zaidi likigeuzwa tena mfano; tunaishi ili? Kwa majibu yaleyale itakuwa tunaishi ili kula, tunaishi ili kujongea, tunaishi ili kuhisi, tunaishi ili kuzaliana.

Hivi utamfikiriaje mtu endapo utamwuliza kwa nini tunaishi na akakujibu "tunaishi ili kutoa takamwili"?. Bila shaka Utakuwa ni mzaha huu japo jibu lake ni sahihi kwa mtazamo uleule wa tunaishi ili kula maana vyote ama kula ama kutoa taka mwili ni viashiria au sifa zinazoonesha kuwa kiumbe anaishi. Asha kum si matusi, ni kweli unaishi ili kutoa takamwili? na kama ndiyo ni jibu kwa swali hili, takamwili unalotoa lina faida gani kwa jamii na taifa? Na kama jibu siyo ni jibu kwa swali hili maisha yaana maana kubwa zaidi ya kula, kukua na kuzaliana. Watu huzaliwa, huishi na hufa na historia pamoja na urithi hubakia kwa vizazi, baada ya uhai kuna watu huacha historia na urithi lakini wapo huacha visa, visasi, chuki, lawama pamoja na migogoro kwa wanaobaki.

Maisha yana maana zaidi ya kula tu na kuzaliana na hata kula na kuzaliana kuna maana zaidi ya maisha na ndiyo sababu kuna watu hawaishi leo lakini wanaonekana kupitia maisha ya watu wengine na wanaishi kupitia kazi walizofanya kipindi cha uhai wao. Unakumbuka kisa cha mtu aliyegundua moto kwa kutumia vijiti vya ulimbombo na ulindi? Unajua ni kwa namna gani uvumbuzi wake ulikuwa na manufaa kwa binadamu? Kabla ya uvumbuzi huo watu waliishi kwa kula mizizi, matunda na vyakula ambavyo havikupikwa lakini baada ya uvumbuzi huo na ubunifu ukaendelea katika kutengeneza moto yaliyofuata ni historia.

Profesa mmoja aliyewahi kuwa mhadhiri katika chuo kimoja mjini Moshi aliwahi kusimulia uzoefu wa maisha yake katika sayari hii, mzee huyu mstaafu katika mojawapo ya semina alizokuwa akituhamasisha vijana hasa tuliopata fursa ya kupata elimu ni namna gani ubunifu ni chachu ya maendeleo katika jamii, taifa na ulimwengu kwa ujumla. Alieleza ni namna gani amekuja kushuhudia katika maisha yake ya uzee mambo ambayo yalikuwa ndoto tu na mengine hayakuwahi hata kufikiriwa enzi za ujana wao, hawakuwahi kufikiri kuwa kutakuja kutokea chombo kinachoweza kupaa angani kama ndege na kuwasafirisha watu kwa uharaka!, na hawakuwahi kuwaza kama kuna siku wataweza kuzungumza na watu walio maili nyingi mbali kutoka walipo kwa kifaa kinachoitwa simu!" Ni baadae sana katika kusoma na kusimuliwa tulijua kuwa, ukiacha magari yanayokokotwa na wanyama kama farasi na punda, kuna magari yanajiendesha kwa kutumia nishati iliyotokana na mvuke pamoja na moto na tulisoma katika sayansi kuwa magurudumu yalibuniwa ili kupunguza msuguano kati ya ardhi na magari" Profesa Alieleza. Alieleza pia ni kwa nini kuna jina kama gari moshi "liliitwa gari moshi sio tu kwa sababu linatoa moshi mwingi la! Hasha, palikuwa na jiko maalumu katika treni ambapo wanaume walifanya kazi ya kuchochea kuni na makaa ya mawe ili kutengeneza nishati ya kuiwezesha treni kujongea, sio hivyo tu, hata meli kubwa zilikuwa na mfumo huo wa majiko kwa ajili ya kuzalisha nishati". Nilikuja kuamini habari hizi baada ya kuangalia senema mbalimbali, ikiwa ni pamoja na iliyojitwalia umaarufu sana katika miaka ya 2000 inayojulikana kama Titanic, ni kweli watu walichochea moto kuwezesha meli kusafiri, lakini ubunifu uliendelea, teknolojia ikakua yaliyofuatia ni historia.

Tupo katika karne ya 21 wakati ambao mapinduzi ya sayansi na teknolojia ni makubwa kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa kabla, maarifa yameongezeka kwa kiwango kikubwa sana, namna ya maisha imebadilika, namna ya uzalishaji ni tofauti pia, Shughuli za uzalishaji mali zinafanyika kwa namna na njia tofauti tofauti, elimu ikiwa imeshika usukani katika kuendesha gurudumu la maendeleo, kilimo kinahitaji elimu, biashara inataka elimu, uongozi unataka elimu, ufugaji unahitaji elimu, uvuvi, shughuli za viwanda hata burudani inataka elimu. Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wakati wa utawala wake aliwataja na kutangaza vita dhidi ya maadui wakubwa watatu, Ujinga, Umaskini na Maradhi, mzee huyu alikuwa na maono makubwa na wengi hawakujua maana halisi ya vita hivi, ndio maana imetugharimu muda mrefu sana kuwafanya wazazi wote wathamini elimu na kuiweka kipaumbele kwa watoto wao. Kwa namna iwayo yote, thamani ya mtu kupata elimu itabaki kuwa kubwa tu katika Taifa, ili jamii na nchi kwa ujumla ipate maendeleo lazima elimu ipewe kipaumbele

Bila shaka hakuna mtu anaishi ili kula tu! Kila mtu ana kitu ambacho ama tayari ama bado familia, jamii na Taifa kwa ujumla linasubiri kutoka kwake. Ni kweli tunakula,tunapumua,tunatoa taka mwili,tunakua,tunazaliana na tunajongea,kuashiria tunaishi, lakini maisha yetu yasiwe mzigo kwa wengine, sote tuna wajibu wa kulijenga Taifa, chakula unachokula kikupe nguvu ya kulitumikia Taifa, na kikukuze kimwili na kiakili, akili itumike kuwaza na kubuni vitu kwa faida ya kizazi cha sasa na baadae, pamoja na mengine, unapojongea usitembee kizembe kuwa na mizunguko yenye faida tengeneza mitandao na watu, tafuta masoko na jenga mahusiano mazuri na jamii inayokuzunguka. Mwili unaoshughulika na kunyumbulika unaonesha mtu yu hai, hata kama kazi zako zinakutaka kuwa sehemu moja tu, Tafuta muda na utumie kufanya mazoezi kwa faida ya afya yako.

Mwisho kabisa, usisahau hii,

2022 ni mwaka wa Sensa, toa ushirikiano katika zoezi hili la kitaifa, faida yake ni kubwa kwa ajili ya maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.
"JIANDAE KUHESABIWA"
download (4).jpeg
 
Upvote 0
Hello members
Please karibu sana kwa mijadala na nitafurahi kama mtanipigia kura kwa threads zangu
 
Back
Top Bottom