SoC04 Tunapaswa kukabiliana na athari za Ubebaji Mabegi Mazito kwa Wanafunzi wadogo

SoC04 Tunapaswa kukabiliana na athari za Ubebaji Mabegi Mazito kwa Wanafunzi wadogo

Tanzania Tuitakayo competition threads
Joined
Jun 13, 2024
Posts
5
Reaction score
5
Tunapaswa kukabiliana na athari za Ubebaji Mabegi Mazito kwa Wanafunzi Wadogo
Utangulizi
Moja kati ya mambo muhimu ya kuzingatia kwa wanafunzi ili kuwa na utimamu ni pamoja na afya zao, ikiwa ni pamoja na pande zote akili pamoja na mwili. Wanafunzi wengi hasa wadogo wameonekaana wakibeba mabegi mazito jambo ambalo lina athari kwenye miili yao. Mfano siku moja majira ya jioni muda wa wanafunzi kurudi nyumbani wakitokea shuleni, macho yangu yalikutana na watoto wadogo ambao migongoni mwao wamebeba mabegi makubwa bila shaka ni vifaa vya shule, nikajiuliza mbona ni makubwa ukilinganisha na umri wao bila shaka hii ina athari kiafya, nikasogea na kupiga nao stori ili nifahamu sababu ya kubeba mabegi mazito.

Walio wengi walisema tatizo ni kutokufuatwa kwa ratiba ambazo ndio mwongozo hivyo kuwalazimu wao kubeba madaftari yote ili lolote likitokea wanapata nafasi ya kushiriki kipindi bila tatizo, wengine wakasema walimu wengi hupenda kumaliza silabasi zao mapema hivyo wanapopata muda wa ziada wanaingia kufundisha hata kama sio vipindi vyao.

Athari Kiafya
Kiafya kuna athari kubwa kwa watoto wanapobeba mikoba au mabegi makubwa na mazito kupita umri wao ambapo kwa mujibu wa Mtaalamu wa viungo au Fiziotherapia kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Daktari Mussa Twalib, moja kati ya athari za watoto wadogo kubeba mizigo mizito ni pamoja na maumivu makali ya mgongo na shingo kwa sababu kutoka shingoni mpaka kwenye makalio kuna diski zilizo katika mfumo wa herufi C ambazo zinategemeana wakati wa kutembea hasa mtu anapokuwa na mzigo, hivyo uzito wa mzigo ukizidi unaathiri moja kwa moja mwili wa mwanafunzi.

Mkuu wa shule ya Sekondari Kerezange iliyopo Ilala Dsm, Mwalimu Simon Lupogo anasema kinachochangia wanafunzi kubeba mizigo mizito ni upungufu na ukosefu wa miundombinu bora katika shule hasa za serikali jambo ambalo linasababisha kukosekana kwa makabati ambayo wanafunzi wangeweza kuyatumia kuhifadhi na kutunza vifaa vyao vya shule na kuepusha kubeba mabegi mazito kila siku kwenda na kurudi

Moja kati ya vitu muhimu na vinavyoweza kuondoa tati kwenye taasisi za elimu sio tu uwepo wa ratiba bali ratiba inayozingatiwa ambayo inawaongoza wanafunzi pamoja na walimu katika kuhakikisha watoto wanasoma kile tu kilichopo kwenye ratiba ya siku na si vinginevyo. Kwa mujibu wa chapisho la kitabibu la East African Medical Journal zaidi ya asilimia 65 ya watoto wanakabiliwa na maumivu makali ya mgongo pamoja na shingo ambayo yanatokana na uzito wa mabegi au mikoba yao ya vifaa vya shule kama vile madaftari, vitabu pamoja na vifaa vingine vya kujifunzia.

Kama ilivyo kwa nchi nyingine duniani Tanzania inapaswa kutunga sera na miongozo ambayo itaongoza utaratibu wa ubebaji mikoba au mabegi kwa watoto hasa kwa kuzingatia umri wao, kwa mfano India kwa wanafunzi kuanzia darasa la kwanza mpaka la pili uzito wa begi unapaswa kuwa kilo 1.6 mpaka 2.2 huku kwa darasa la tatu mpaka darasa la tano uzito unapaswa kuwa ni kilo 1.7 hadi kilo 2.5.

Katika nyakati tofauti wadau mbalimbali wa Elimu wamekuwa wakitoa ushauri wa namna ya kufanya au kulishughulikia jambo hili ikiwa ni pamoja na kuwakumbusha watunga sera na viongozi kuweka utaratibu utakaozingatia uzito wa mabegi. Mfano Mkurugenzi wa Taasisi ya Haki Elimu Dkt. John Kalaghe ambapo amesema kuwa msaada kwa shule za serikali ni pamoja na kuwa na miongozo wakati wa kutunga mitaala ili idadi ya masomo iendane na umri kwa sababu kumekuwepo na baadhi ya taasisi za elimu hasa za watoto wadogo ambao wanawafundisha watoto wa umri mdogo masomo mengi kuliko umri na uwezo wao wa kuyashika na kuzingatia jambo linalofanya watoto kubeba mabegi yengi daftari nyingi pamoja na vifaa vingine

Pamoja na kwamba hili ni jukumu la kwetu sote lakini serikali ndio inapaswa kuja na mpango thabiti kwa maana ya mwongozo na kanuni ili kudhibiti hili, katika moja ya mahojiano na chombo cha habari cha umma TBC Taifa, Kamishna wa Elimu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Lyabwene Mutahaba amewahi kusema kuwa wao ambao ndio wasimamizi wa sera wamekuwa wakihimiza kupitia nyaraka mbalimbali kuhusu kuzingatia ubebaji wa mabegi japo utekelezaji umekuwa mgumu, hii ina maana serikali imekosa nguvu ya kudhibiti taasisi za elimu ambazo inazisimamia kupitia wizara ya Elimu.

Hitimisho
Maumivu makali ya mgongo pamoja na shingo yanayosababishwa na uzito mkubwa wa mabegi yanaweza kusababisha udumavu na ulemavu kwa mtoto na hatimaye maendeleo duni ya elimu hivyo ni jukumu letu sote kulitazama jambo hili na kulichukulia hatua kwa mustakabali wa afya za wanafunzi na maendeleo ya elimu kwa ujumla ikiwa ni pamoja na kuja na mpango thabiti ili kuziongoza shule, lakini pia kwa wazazi ni kushirikiana na walimu ili kuzingatia ratiba za masomo shuleni ili wanafunzi wawe wanabeba vifaa vya siku husika tu.
 
Upvote 1
Back
Top Bottom