Taswira
JF-Expert Member
- Sep 23, 2012
- 1,198
- 447
MAONI YA MHESHIMIWA (HAYATI) TUNTEMEKE MESAKA NNUNG'WA SANGA KUHUSU MUUNGANO MWAKA 1993.
MBUNGE mashuhuri kutoka Makete, Tuntemeke Sanga, ambaye mitaani habari zilipata kusambaa kwamba ni msomi mwenye degree saba, alikuwa mmoja wa wachangiaji wa hoja kuhusu Serikali tatu ndani ya Muungano, iliyozua mvutano kati ya kundi la wabunge, maarufu kama G55 na Serikali, na sehemu nyingine ya wabunge. Yafuatayo ni maneno yake kwa mujibu wa kumbukumbu rasmi za Bunge (hansard) Agosti 24, mwaka 1993, kama yalivyoandaliwa na Godfrey Dilunga.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninashukuru kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kutoa mchango wangu kuhusu hoja iliyoko mbele yetu. Nina mpongeza Mheshimiwa Kasaka, pamoja na wale wenzake wengine 54 kwa kutuletea hoja ya aina hii baada ya kutafakari kwa makini kabisa nini taifa letu linahitaji lifanye ili tuweze kuishi kwa utulivu kwa amani na kuendeleza taifa letu kama inavyotakikana.
Kwa hiyo moja kwa moja naunga mkono hoja hii kama ilivyo. Kwa lengo zima la kutoa nafasi kwa Serikali, Chama, Watanzania wote na taasisi mbalimbali ili tushiriki kupata mwafaka wa kuendesha suala zima la umoja wetu na amani yetu na maendeleo yetu kwa mujibu wa katiba na kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, yako mambo mengi sana ya kuzungumzia juu ya uhai na usalama wa taifa. Kwa dhati kabisa naona hakuna tatizo lolote katika Muungano wa Tanzania. Hakuna tatizo lolote. Lakini ninakiri kwamba tatizo lipo katika uongozi, katika namna ya kuiendesha nchi yetu. Hilo ndilo tatizo kubwa na tusipojihadhari tutafikia mahali tukaanza kuvunja maadili yetu, tukaanza kuvunja sheria zetu, hata kuvunja Katiba yetu kwa sababu ya wale wanaotuongoza na sisi tunaowaongoza. (Makofi)
Nimejifunza sana masuala ya dini, kwa upande wa Wakristo, kwa upande wa Waislamu na kwa upande wa Budha na kadhalika. Ni wazi kabisa sababu ya kuweka sheria za Hamirabi, ilikuwa ni kudhibiti mwenendo wa raia na wale wanaotawala. Sababu ya kuweka zile amri kumi za Mungu ni kwa lengo hilo hilo la kutuweka sawa na kudhibiti. Inakuwa kama ni kioo. Pale ambapo tunapopata matatizo watu wanaanza kufanya mambo yao kibinafsi, wanakwenda kinyume cha taratibu, sheria na Katiba.
Suala la kudhibiti na kuwajibika lipo. Naomba niseme hivi hapa tutakapopata hiyo Serikali ya Tanganyika, kama tutaipata; na mimi nitasikitika sana kama tutapata. Nataka nishauri, nasema maneno yangu kwa uangalifu sana, napenda nishauri kwamba hapo tutakapopata hiyo Serikali ya Tanganyika kama tutaipata na mimi sipendelei tuipate, basi suala la kuheshimu Katiba, suala la kuheshimu sheria na maadili yetu ya Chama, vitakuwa ni vya muhimu sana.
Ili hicho tutakachokiunda na kukiumba tuweze kukiheshimu kwa mujibu na taratibu zake. Mtu yeyote anayekwenda kinyume cha Katiba pamoja na sheria suala zima la kuwajibika lipo. Tuwe na hilo lengo na naishauri Serikali mkazo mkubwa sana kwa chochote kitakachotokea ni kuona suala la sheria na kuheshimu Katiba ni la msingi kabisa. Ule mnara wa Babel, watu walienda kinyume kabisa cha kuheshimu sheria na taratibu zake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kila mtu aka-develop, akaanzisha lugha yake. Halafu baadaye ikawa watu hawaelewani na nchi nyingi sana duniani Somalia ikiwepo, Yugoslavia ikiwepo, Urusi ikiwepo, inatokana kwanza na uongozi ambao sio shupavu, viongozi ambao wanaendeleza ubinafsi zaidi kuliko kitu kingine hata wakafikia mahala ambapo sheria wakaanza kutoziheshimu. Sasa Muungano huu uliotolewa na Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere na Hayati Karume, kilikuwa ni kitendo cha kujivunia sana katika Tanzania na katika Afrika. Kitendo kizuri kweli. (makofi).
Mimi ningependa tutafute lugha ya kumheshimu Marehemu Mzee Karume, kwa kukubali at a time, wakati ule wengine wanapenda kwanza wafurahie uhuru wao yeye anatamka Mwalimu nakuomba uwe Rais. Tuwe na Muungano wewe uwe Rais. Mimi najiondoa. This is the hero. Hero number one wa Afrika hakuna kiongozi mwingine, a political saint wa siasa, mzito huyu na tumkumbuke kwa heshima kubwa sana hata kama amekufa, amekufa kimwili lakini kiroho na mawazo ya Afrika anaishi, he is number one in Africa. Huyu ana merit ya Lenin, nafasi ya Max Garvey, nafasi ya Nkrumah, hakuna mfano kama huo katika Afrika nzima. Nawaombeni sana Watanzanai tu emulate ile spirit ya kujitolea kwa ajili ya mazuri ya Tanzania na Afrika, tukipata viongozi wawili, watatu katika Afrika ambao wanaweza kujitolea wakaacha ile nafasi ya kuitwa marais kwa lengo la kuleta umoja na katika umoja kuna vitu vingi sana, nadhani tutakuwa tunafanya justice kubwa sana kwa Bara la Afrika. (makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Bara la Afrika lina matatizo mengi sana tena makubwa sana. Mwafrika leo ulimwengu mzima anadharauliwa tena kwa kweli kabisa kwa sababu ni mnyonge tangu mkutano wa Berlin Conference mwaka 1884/85 Afrika ilipelekwa mahala ambapo kuna dharau kubwa sana, Afrika iliyokuwa moja kukatokea vijinchi vingi sana na mpaka leo wako wanaoheshimu unyonge huo. Utumwa ukatokea, njaa imetokea, unyonge umetokea, usalama wa Afrika uko hatarini tuna Vijirais vingi mno katika Afrika – vingi mno, wakati huu inatakiwa kuondoa ondoa udhaifu wa kuwa na Virais vingi na viserikali vingi na vikatiba vingi vingi.
Jana nilipata kusikia mawazo kwamba ati Marekani ina Katiba nyingi hamsini na kitu, Marekani ina nchi nyingi; lakini si kweli hata kidogo Marekani ile inawezekana ina vinchi vijimbo, vijimbo hamsini na kitu labda hata Cuba baada ya Castro kuondoka itakuwa ni State ya Marekani/Jimbo la Marekani la hamsini na mbili sijui. Lakini Marekani ina Katiba moja tu na Marekani ina bendera moja tu ni kweli tupu.
Katika historia ya Marekani kwa wale wanaoijua, wako Wamarekani ambao hawakupenda wawe na bendera moja walikimbilia Canada, wako Wamarekani waliotaka kuwa vijimbo, vi nchi vingi lakini ikatokea vita Civil war na Abraham Lincon akasema, a house divided cannot stand, kwa hiyo wakapigana mle mle Marekani wakapigana kwa kulinda taifa moja na heshima moja; leo Wamarekani ni taifa number one.
Urusi baada ya mapinduzi ya mwaka 1917 ilikuwa inaelekea katika nguvu sawa na Wamarekani na ilifika mahali likawa taifa kubwa kabisa, lakini kutokana na ubinafsi, kutokana na mawazo finyu, kutokana na mawazo ambayo hayapimwi na umoja wa taifa Urusi imesambaratika Gorbachev amesababisha hayo. Leo kuna bendera nyingi katika Soviet Union, leo kuna Katiba nyingi katika Soviet Union huu mfano hatuwezi kuuiga haiwezekani, ni aibu. Watu wanagombana, uchumi wao umekwisha kabisa wamebakiwa kusaidiwa tu na Waamerika ambao ni adui yao mkubwa kabisa.
Ninawaombeni Watanzania, tuiruhusu Serikali na Chama cha Mapinduzi, kutuletea mwafaka wa kuangalia hivi sasa tunakwenda wapi, Tanganyika ilikufa mwaka 1964, Zanzibar ilibaki.
Tukitaka kuboresha Muungano wetu mimi nasema basi, lakini naheshimu mawazo ya wenzangu, lengo siyo kurudi kufufua Tanganyika, lengo ni kuona kwamba tuna Rais mmoja, Katiba moja na Zanzibar ikiwezekana ifike mahali iache hilo neno Zanzibar. The proposal is very unpopular, naelewa hivyo. Naelewa fika lakini kwa lengo la kuboresha umoja wa Afrika kwa lengo la ku-modernize siasa zetu na uchumi wetu ni vizuri zaidi kwa Zanzibar isiwe a sovereign state, wala Tanganyika ni vizuri zaidi kuliko kuanzisha lingine na kurudi nyuma. Huu ndio ukweli.
Watanzania, wakulima, wafanyakazi na wanafunzi wenye shida mbalimbali, watu wasio na kazi, watu wenye njaa, watu wenye magonjwa mbalimbali wanaoishi katika nchi ambayo haijaendelea kikubwa zaidi ni kuwa na nguvu ya kutatua matatizo ya taifa tukigawana nguvu inapungua, hatuwezi kuhimili matatizo ya Tanzania, ya Afrika kwa kuwa na Vikatiba katiba vingi na kuwa na Viserikali serikali vingi ni uchoyo, uchu wa madaraka. (makofi)
Ninawaomba, umoja ni nguvu utengano ni udhaifu. La kufanya leo ni kusonga mbele, la kufanya leo ni kuimarisha hiyo Tanzania yetu. Sasa ziko njia mbili, naamini fika kabisa tukiendelea tulivyo bado tutakuwa na vineno vineno na Zanzibar itaona inaonewa katika hili na hili. Sisi tuko watu milioni 25 au 26 na wenyewe wako laki saba, Watanganyika nao wataona wanaonewa onewa au tunadharauliwa. The tyranny of the manority is equal in a very small way with the tyranny of the majority. Compartibility inakuja katika kukubaliana mambo tufanye nini kwa ulimwengu wenye matatizo makubwa sana na tusonge vipi ki-mshikamano.
Dar es Salaam na Costal Union hii ilikuwa part of Zanzibar. Walioitawala Zanzibar walitawala hii Dar es Salaam. Hata Kenya, Mombasa, Malindi Wazanzibar walikuwa wametawala kisha Mjerumani akaja akanunua, Dar es Salaam na huko Kenya Mzee Karume na serikali yake wakamkabidhi Kenyatta Mombasa na Malindi ambayo ilikuwa ni part and parcel ya Zanzibar, I stand corrected; lakini ndivyo ninavyoamini na kuelewa. Kwa hiyo mahusiano kati ya Zanzibar na sisi ni kitu kimoja kwa damu.
Nimefurahi sana na hotuba moja iliyotolewa hapa, tumepigana vita vya Uganda kama Tanzania na tukashinda, sijui kama Zanzibar ingepigana vita hiyo kama ingeshinda au Tanganyika lakini kwa umoja wetu tumepigana na tumeshinda. Tumesaidia ukombozi wa Afrika kama Tanzania, Watanzania walio wengi wamezaliwa katika himaya ya Tanzania hatuwezi tukaanza kuandika vitu upya, tumefanya mikataba mingi ya uchumi, mingi tu zaidi ya 180 na mataifa mengi ulimwenguni kwa jina la Tanzania, ni heshima kubwa sana, tukirudi nyuma a lot of papers will have to be changed, hatuna nafasi hiyo katika ulimwengu wa leo hakuna nafasi kabisa. Foward yes and back ward no.
Napenda nieleweke hata kama hakuna atakayekubaliana na mimi wakati huu mwaka 1993 mwezi wa nane na kuendelea, naiomba Serikali iangalie tulikotoka tumefanikiwa vipi, tunakwenda wapi, tusithubutu kuunyofoa Muungano, kuuvunja Muungano bali kuuimarisha tu, lugha ya Kiswahili sasa inaelekea kwenye eneo la kukubalika itumiwe katka Universties na Colleges nyingi ulimwenguni zinafundisha Kiswahili, hiki ni chombo chetu kizuri sana, tumeanza vizuri.
Matatizo yaliyoanza kujitokeza hapa na pale ya uchumi na dini tumeyadhibiti, Tanzania ni member of OAU, Tanzania is a Member of United Nations, Tanzania imetia saini kule Abuja – tamko la Abuja Declaration la kuboresha uchumi kuwa na soko moja la Afrika. Tuko PTA, tuko SADCC na kadhalika kadhalika, kwa hiyo agenda nambari mbili katika karne ya 21 inayokuja ni kuboresha uchumi wetu wa Tanzania na Africa Collectively kwa umoja, kwa mshikamano.
Vitatizo vitajitokeza viko mpaka Yesu/Mohamed watakapokuja viko, lakini tutatatua matatizo yetu kama mmefunga ndoa, suala zima ni kulinda hiyo ndoa, mke wako atakuletea matatizo, mume wako atakuletea matatizo, watoto watakuletea matatizo lakini hamwanzishi vita mnajifunza kiutu kutatua matatizo yenu.
Lakini nikisema haya naamini, kuna baadhi ya watu ndani ya Tanzania ambao kwa kweli wameapa na wanataka kutawala na kupewa majina makubwa makubwa na hii inatuumiza, inakwenda kinyume cha spirit ya hayati Mzee Karume.
Naiomba Serikali na Chama tutekeleze Ilani ya mwaka 1990 kifungu cha 15 kinachosema: "Wewe unayogombea ubunge, uahidi kwa watu wako wapiga kura kwamba, utaulinda Muungano kwa njia zote zile na tukifanya vinginevyo tunawajibika turudi kule, kwa wananchi na mimi nakwenda kusema hivyo Makete."
La pili, tumekuja hapa ndani, sikusimama kule mimi wala pale, nilisimama hapa na nikaapa na kiapo hicho kinasema, mimi Tuntemeke Sanga, naapa kwamba nitakuwa mwaminifu kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na nitaitetea na kadhalika, Mungu nisaidie. That is what I said, mambo mazito sana haya. Kiapo hiki lakini uwezekano wa kuunda Tanganyika upo, huwezi ukalinganisha Somalia na Tanzania haiwezekani kabisa lakini tunaweza kwenda huko kubaya. Huwezi ukalinganisha Tanzania na Urusi, demokrasi ya Urusi ilikuwa imebanwa tangu wakati wa mapinduzi ya 1917, ilikuwa imewabana watu hawakuwa huru na Somalia ni hivyo hivyo.
Lakini hapa hanibishii mtu, demokrasi imekuweko hata ndani ya chama kimoja na hivi sasa vyama vingi vinakaribishwa kuingia na viko vinakuja tuna amani ya ajabu kabisa tuilinde, tuna umoja wetu, tuulinde, tuna heshima zetu tuzilinde.
Leo asubuhi na jana watu wanazungumzia suala la ndoa, ndoa huku ndoa huku ndiyo sisi wenyewe, kwa hiyo tusonge mbele, kurudi nyuma haiwezekani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii.
Namshukuru Mheshimiwa Njelu Edward Mulugala Kasaka na wenzake kwa sababu wameniruhusu kwa hoja yao niweze kutoa haya mawazo yangu, lakini kwangu kurudi nyuma haiwezekani; never bali ni kwenda mbele.
Suala la Muungano kusifanyike chochote ila kuboresha, neno kuboresha limekuja karibuni, kukarabati – to modernize ili tuwe na Serikali moja, bendera moja, taifa moja, uraia mmoja, masuala ya uchumi wa Zanzibar na mahali pengine tutayaboresha kwa sababu hii ni agenda nambari two katika Afrika – kuboresha uchumi wetu. Nashukuru sana, ahsante sana. (makofi).
Tuntemeke sanga,
Alikuwa mbunge wa Wilaya ya Makete.(Iringa)
Alikuwa msomi wa kwanza bunge la Tanzania(Degree 7).
Ndiye mbunge aliyetamka wazi wazi kuwa anautaka "UNYERERE" (URAIS) baada ya kutoka kusoma.
Alifariki mwaka 1997.
Amezikwa Makete.