SoC04 Tuoneshe kwa vitendo thamani ya elimu na namna ilivyo nguzo mama katika kila sekta ili tujikomboe

SoC04 Tuoneshe kwa vitendo thamani ya elimu na namna ilivyo nguzo mama katika kila sekta ili tujikomboe

Tanzania Tuitakayo competition threads

Bashiru Abdallah

New Member
Joined
Jun 20, 2024
Posts
1
Reaction score
0
Elimu bora yenye kujali hasa hali ya kila mtanzania wa chini ndiyo hasa daraja la kuivusha nchi yetu kutoka katika ulimwengu huu wa kidigitali na mapinduzi ya teknolojia na uchumi kwa ujumla. Ni ukweli usiopingika kuwa hatuko katika kiwango kizuri katika chati ya ubora wa elimu, wachilia mbali duniani, bali hata ndani ya Afrika Mashariki ambayo sasa ina nchi takriban nane.

Kama alivyosema Bwana Alvin Toffler kuwa “ujinga wa karne ya 21 sio kushindwa kusoma na kuandika”. Tuko katika zama za “ujinga ni kushindwa kujifunza kwa kuendana na kasi ya ukuaji wa teknolojia katika uulimwengu wa mapinduzi ya kiuchumi”

Leo hii ulimwengu wetu ni wa kidigitali kwa takriban asilimia 100, lakini mfumo wetu wa elimu bado haukidhi kuendana na kasi hiyo. Na mabadiliko haya si kwamba yamesimama, nayo yanabadilika kwa kasi sana kila uchao. Ni ajabu na inauma sana kuona Tanzania bado tunatoa wahitimu wa shahada ya kwanza katika nyanza tofautitofauti lakini hawana ujuzi na ufanisi japo wa kutumia Basic Computer Applications na tayari dunia imeshahama kwenye hili. Mfano mdogo tu, katika suala la ajira kwa sasa, tunazalisha watanzania wangapi ambao wanaweza kushindana katika soko la ajira ndani ya Afrika Mashariki, wachilia mbali Afrika na dunia mzima. Tazama leo namna ajira zinazozalishwa ndani ya nchi yetu zinavyojazwa na majirani zetu na wageni ambao kimsingi wanamudu si kwa jengine ni kwasababu ya namna walivyoandaliwa na mifumo ya elimu ya nchi zao. Na mfumo wa elimu ukiwa na mushkili, basi hapana shaka kila sekta itakuwa na mushkili. Sekta ya Elimu ndiye mama mlezi wa sekta ya Afya, Ulinzi na Usalama, Utawala Bora, Uchumi na Fedha na kila nyanja inayogusa ustawi wa jamii. Lazima elimu ipewe kipaumbele kuliko jambo lolote ili tukomboke.

Je, hatuwezi kubadili mfumo wetu wa elimu, ukawa mfumo unaoendana na kasi ya mabadiliko ya dunia? Mfumo ambao utazalisha watanzania wenye fikra pevu na uwezo mkubwa kufikiri kimantiki na kitunduizi bila kuegemea moja kwa moja kwenye fikra za wengine? Mfumo ambao utawafanya vijana wetu kutokuwa wakosefu na wasubirifu wa ajira na kubebwabebwa? Bila shaka inawezakana sana tukiwa na dhamira ya dhati na kama tutakubali kumng’ata jongoo kwa meno. Katika hili lazima tukubali kuumia. Ni lazima, kwani haya si mabadiliko madogo. Japo umakini mkubwa unatakiwa.

Tunapougusa mabadiliko ya mfumo wa elimu, moja kwa moja tunagusa nukta zake nyingi kwa mapana na marefu kama sera za elimu, mitaala, ubora na thamani tunayowapa walimu, nyenzo za kujifunzia, nk. Kwa kutazama duru ya miaka 5 hadi 25 tubnaweza kuanza kuyafanyika kazi kwa vitendo mambo yafuatayo.

1. Thamani ya elimu na mwalimu
Thamani ya elimu imekuwa ikinadiwa sana na kila mtu, lakini kwanini leo hii vijana wengi huchagua kusomea ualimu ikiwa tu ufaulu wao hauwapi wigo mpana wa kuchagua taaluma nyingine. Mfamo mdogo tu; ni nani n ani wangapi kati wanafunzi 10 bora katika ngazi za wahitimu wa sekondari ambao kwa ridhaa na mapenzi yao wameuchagua fani ya ualimu? Nachelea kusema hakuna, lakini hapa ndipo tunapotakiwa kubadilisha huu mtazamo kwa kuamua kwa dhati kuipa thamani elimu ambako kunakwenda sambamba na kumthamini mwalim. Kumthamini mwalimu ni sambamba na ualimu kusomewa na watu mahiri zaidi huku maslahi na mazingira yao yote kutazamwa kwa kina na kuboreshwa.

2. Ubora na umahiri wa walimu
Tuna vyuo vingi sana, lakini wahitimu ambao tunawatunuku vyeti kuja kufundisha watoto wetu, wengi wao si mahiri kwa kiasi kinachoridhisha. Na kwa asilimia fulani hili linachangiwa na nukta namba 1 hapo juu. Inakuwaje mwalimu ambaye sote tunajua kuwa anakuja kufundisha shule ya msingi, tunampa mafunzo ya kufundisha wanafunzi wa sekondari na vyuo vya kati? Atakuwaje mahiri wakati mafunzo yake hayaendani na anachokwenda kukitenda. Iweke sera maalumu ya kuliratibu hili, na lisimamiwe kwa umakini lisitendwe vinginevyo. Hili liende sambamba na mafunzo ya mara kwa mara ya walimu kuhusu ualimu wao na namna ya kuwa tayari kubadilika kulingana na mahitaji/hali za wanafunzi. Walimu wetu wasiwe mahiri kwa wanafunzi ambao wanaelewa haraka bali kwa wale ambao wanachelewa kuelewa na wasahaulifu.

3. Shule za umma ziboreshwe na kupewa kipaumbele
Kwa wengi sana, imeshaaminika kuwa elimu bora inapatikana shule zisizo za umma, na kwa kweli elimu sasa imekuwa biashara hasa katika shule hizi. Wengi katika watanzania hawana uwezo wa kumudu kulipia gharama za watoto wao licha ya kuwa wengi wanatamani watoto wao wasome shule zisizo za umma kutoka na ubora unaodhaniwa na kuonekana. Shule za umma zimekuwa na hali mbaya kuliko, wakati miaka 20+ nyuma ilikuwa ni fakhari mtoto kusoma shule ya umma. Na kusoma shule ya binafsi ilikuwa inatazamwa kama chaguo la waliofeli au kupata ufaulu wa kawaida. Tukitazama uwiano wa wanafunzi na idadi ya madarasa, uwiano wa walimu na wanafunzi na vitendea kazi, hali inatisha. Tazama hali ilivyo kwenye jedwali hili;

Nukta upembuzi wa haraka kutoka kwenye kiambatanisho: Wanafunzi ni wengi zaidi ambao wanasoma shule za umma kuanzia ngazi ya chekechea, lakini kwenye nukta ya idadi ya walimu peke yake kulinganisha na idadi ya wanafunzi hali ni mbaya sana. Vipi kwenye nukta ya nyenzo za walimu kufundishia na rasilimali nyinginezo?

Natamani kuona tunarudi katika zama za sote kutamani watoto wasome shule za umma na kupata elimu bora bila kuziua shule za binafsi kwa wenye uwezo wa kumudu.

4. Mazingira ya kujifunza kwa kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia
Nukta hii inazigusa nukta zote tatu zilizotangulia katika mazingira tofautitofauti. Tukiwatazama walimu wetu, shule zetu na akili za asili watoto wetu bado ni vitu vinavyokinzana. Watoto wengi sasa hivi wanashauku ya kujifunza kwa kutumia teknolojia, lakini mazingira yetu ya mashuleni, umahiri wa walimu na hata nyenzo zetu hazikidhi shauku hii ya watoto wetu. Jambo ambalo linahatarisha kuwadumaza watoto hawa wasiwe wadadisi, wagunduzi na wanamapinduzi wataolifaa taifa letu siku za usoni.

Mwisho, ili kuyafanya haya yawe ni yenye kutekelezeka kwa ufanisi zaidi ni kuunda sera au sheria itayowalazimisha viongozi wetu hasa wanaopatikana kupitia majukwaa ya kisiasa (kama wabunge, mawaziri, wateule wa Rais, na mfano wao) kuwaandikisha watoto wao katika shule za umma ndani ya nchi kwani katika hili kutakuwa na umakini katika uratibu, usimamizi, utekelezaji na uboreshaji wenye tija kwa taifa letu.
 

Attachments

  • Takwimu.jpeg
    Takwimu.jpeg
    41.4 KB · Views: 1
Upvote 5
Back
Top Bottom