Tukuza hospitality
JF-Expert Member
- Jul 30, 2022
- 321
- 691
Kwa mujibu wa “Wikipedia ya Wamachinga”, Wamachinga ni kabila la watu wa Tanzania wanaoishi katika mkoa wa Lindi, wilaya za Kilwa na Lindi; lugha yao ni Kimachinga.
Kwa mujibu wa “Wikipedia” hii, kwa kipindi cha karne ya 20 na 21, Wamachinga wamekuwa maarufu katika miji mbalimbali kwa kuuza bidhaa, hasa nguo za mitumba, wakiwa wamezishika mikononi wakisaka wateja. Hali hii imepelekea wafanyabiashara wa namna hiyo wote kuitwa Wamachinga, ingawa wanatoka makabila mbalimbali na mikoa (maeneo) tofauti nchini Tanzania.
Ingawa sina takwimu rasmi za Wamachinga, ni dhahiri kwamba wengi wao ni vijana wa umri wa kati ya miaka 14 na 45, wanaume kwa wanawake (wanaume wakionekana kuwa wengi zaidi).
Tofauti na ilivyozoeleka zamani, kwamba Wamachinga ni wafanyabiashara wadogowadogo, wanaotembeza bidhaa zao mikononi, wengi wao hivi sasa wanapanga bidhaa zao katika barabara za mitaani, chini au mezani, mbele ya maduka ya wafanyabiashara.
Wamachinga wanaongezeka mijini kila mwaka, (hasa jijijini Dar es Salaam); na hii inatokana na ukweli kwamba kila mwaka kuna maelfu ya vijana (wa kike na wa kiume) wanaohitimu elimu katika ngazi mbalimbali (shule za msingi, shule za upili, vyuo vya kati, na vyuo vikuu), ambapo wengi wao ama hawaendelei na ngazi nyingine za elimu, au hawapati ajira (sekta binafsi au sekta ya umma).
Hali hii imefanya miji mingi kuwa na mafuriko ya Wamachinga, hasa jijini Dar es Salaam. Jijini Dar es Salaam, hasa maeneo ya Kariakoo, barabara za mitaa mingi imefurika Wamachinga na bidhaa zao, licha ya juhudi za serikali kuwatengea maeneo mengine kwa ajili ya biashara zao. Hali hii husababisha magari kupita kwa shida au kushindwa kupita katika barabara za mitaa hii. Wamachinga wameshindwa kutii maelekezo ya serikali ya kuhamia maeneo mengine, wakidai kwamba wanakopelekwa hakuna wateja.
Kwa maoni yangu, itakuwa ni vigumu sana kwa serikali kuwaondoa Wamachinga katika mitaa ya majiji na miji, kwa sababu kila mwaka kuna wimbi kubwa la vijana wanaoingia mitaani baada ya kuhitimu katika shule/vyuo mbalimbali nchini.
Kumbe ni muhimu kutafuta mzizi wa tatizo, kuliko kuhangaika na matokeo ya tatizo!
Kundi la Wamachinga, jijini Dar. Chanzo: www.ippmedia.com (Disemba 14, 2016)
Biashara ndogondogo zipo duniani kote
Biashara ndogondogo na zile za wastani zinatambuliwa na Umoja wa Mataifa, ndio maana Juni 27 kila mwaka ni siku ya kimataifa ya biashara ndogondogo na zile za wastani. Kwa mujibu wa Jarida la Umoja wa Mataifa (Juni 30, 2017), siku hii ambayo imeadhimishwa kwa mara ya kwanza mwaka 2017, baada ya kupitishwa na azimio la Baraza Kuu ya Umoja wa Mataifa, inalenga kuhimiza umuhimu wa sekta ya biashara ndogondogo na zile za wastani katika kutimiza Malengo ya Maendeleo Endelevu.
Jarida linaendelea kusema, biashara hizi hutoa fursa za ajira kwa takriban watu milioni 250 na ni uti wa mgongo wa uchumi katika mataifa mengi kote ulimwenguni, huku zikitoa mchango muhimu katika nchi zinazoendelea. Biashara hizi zinatajwa kuwa muhimu katika ajira na fursa za kujipatia kipato, na ni muarobaini katika kukabiliana na umaskini na kuchagiza maendeleo, hasa lengo namba nane la Malengo ya Maendeleo Endelevu (“Sustainable Development Goals [SDGs]”).
Kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa, biashara ndogondogo na za wastani, rasmi na zisizo rasmi zinajumuisha asilimia 90 ya biashara zote na kwa wastani huajiri asilimia kati ya 60-70 ya jamii, huku zikichangia asilimia 50 katika pato la ndani la taifa (“Gross Domestic Product - GDP”).
Nchini Tanzania, bidhaa nyingi zinazouzwa na Wamachinga ni zile ambazo sii za chakula, kama simu na vifaa vyake, viatu, vitabu, vifaa vya maofisini, nk, ambazo kwa kiasi kikubwa zinatoka nje ya nchi.
Kwa mujibu wa taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania, Tanzania huagiza bidhaa mbalimbali kutoka nchi mbalimbali, hususani China, India, Afrika Kusini, Kenya, na Muungano wa Falme za Kiarabu (United Arab Emirates). Bidhaa zinazoagizwa kwa wingi ni pamoja na vyombo vya usafiri, mashine mbalimbali, vifaa vya ujenzi, mafuta, mbolea, malighafi za viwanda, na bidhaa za matumizi ya nyumbani.
Wafanyabiashara wengi wadogowadogo (wa kiwango cha wa Wamachinga) na wale wa kati husafiri kwenda nchi mbalimbali (hasa, China, Taiwan, Umoja wa Falme za Kiarabu, Afrika Kusini, Uturuki, na baadhi ya nchi barani Ulaya) kununua bidhaa mbalimbali kama nguo, vifaa vya kielektronik n.k na kuzileta katika soko la Tanzania. Wengi wa hawa wafanyabiashara hawajasajiliwa, hivyo naamini takwimu za biashara hii haziingizwi katika vitabu vya serikali.
Wamachinga wawezeshwe Kuuza Bidhaa Nje ya Nchi
Kwa mujibu wa taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania, Tanzania huuza nje ya nchi bidhaa hizi: tumbaku, kahawa, pamba, korosho, chai, na karafuu. Bidhaa nyingine ni dhahabu na bidhaa za viwandani. Biashara hii hufanywa na aidha serikali au wafanyabiashara wakubwa.
Kwa mujibu wa Benki Kuu ya Tanzania, Tanzania imesajili nakisi ya biashara (“trade deficit”) ya dola za kimarekani Milioni 1,371.70 katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2022. Nakisi hii inatokana na ukweli kwamba nchi inatumia fedha nyingi za kigeni kuagiza bidhaa nje ya nchi, kuliko kiasi cha dola kinachopatikana kutokana na kuuza bidhaa zake nje ya nchi.
Kwa kuwa wafanyabiashara wengi nchini Tanzania ni wadogowadogo, na ni muhimu sana katika uchumi wa nchi, serikali inaweza kutengeneza mazingira mazuri yatakayowawezesha kuchakata na kuuza bidhaa zao nje ya nchi. Hii itasaidia nchi kuwa na Uwiano chanya wa Malipo (“Positive Balance of Payment”), na hivyo kuongeza thamani ya shilingi yetu. Nguvu nyingi wanayotumia wafanyabiashara hawa wadogo kuagiza bidhaa ndogondogo nje ya nchi, ihamie katika kuuza bidhaa zetu nje ya nchi. Polepole, jitihada hizi zitapunguza kwa kiwango kikubwa Wamachinga mijini na majijini.
Mapendekezo
Serikali iimarishe sekta ya uchakataji wa bidhaa nchini kukidhi soko la ndani na la kimataifa.
Serikali iweke mazingira mazuri (mafunzo, vibali, nk.) kwa wajasiriamali na/au wafanyabiashara wadogowadogo kuwawezesha kuuza bidhaa zao ndani na nje ya nchi.
Serikali itumie balozi zake zilizoenea nchi nyingi duniani kutafuta masoko ya bidhaa zinazozalishwa hapa nchini
Hitimisho
Jitihada hizi za kuwawezesha wafanyabiashara wadogowadogo zitasisimua uchumi wa nchi kwa kuongeza fedha za kigeni ambazo zitasaidia nchi kupunguza nakisi ya biashara, na hivyo kuwa na Uwiano Chanya wa Malipo.
Rejea
Jarida la Umoja wa Mataifa (Juni 30, 2017), Biashara ndogondogo na mchango wake katika fursa za ajira
sw.wikipedia.org

Wamachinga - Wikipedia, kamusi elezo huru
Upvote
10