Tusichoke kutembea kwenye barabara ya kumbukumbuku

Tusichoke kutembea kwenye barabara ya kumbukumbuku

Mohamed Said

JF-Expert Member
Joined
Nov 2, 2008
Posts
21,967
Reaction score
32,074
TUTEMBEE KATIKA BARABARA YA KUMBUKUMBU...VINGINEVYO ITAOTA MAJANI

Siasa za kikoloni zilikuwa zikibadilika na kwa hivyo zilihitaji damu changa zenye mawazo na mbinu mpya ili kuongoza harakati za kudai uhuru wa Tanganyika.

Serikali ya kikoloni ilikuwa kila kukicha inabadili mitindo, hila na mbinu za ukandamizaji ili kuendeleza utawala wake.

Ukitazama mwelekeo wa siasa na mazingira ya wakati ule, uongozi wa wazee katika TAA, kwa hali yao na kutokana na mambo yaliyokuwa yakiwakabili, walikuwa hawana uwezo wa kukabiliana na changamoto ya ukoloni.

Lakini pamoja na yote hayo, wazee hawakutaka kuachilia madaraka.

Jambo hili lilizusha mvutano baina ya wazee viongozi wa African Association na wanasiasa vijana waliosomeshwa na Waingereza.

(Rais wa TAA wakati ule alikuwa Mwalimu Thomas Plantan, mtoto wa Affande Plantan (Chief Mohosh) ambae baba yake alikuwa Chifu wa Kizulu kutoka Imhambane, Mozambique aliyeingia Tanganyika (Germany Ostafrika) mwishoni 1800 akiongoza askari mamluki 400 wa Kizulu kuja kulitia nguvu jeshi la Wajerumani chini ya Hermann von Wissman lililokuwa linapambana na Abushiri bin Salim na Mtwa Mkwawa).

Vijana waliokuwa wanataka mabadiliko ndani ya TAA walikuwa Abdulwahid na Ally Sykes, Tewa Said Tewa, Stephen Mhando, Dossa Aziz, James Mkande kwa kuwataja wachache.

Pamoja na hawa vijana wanamji wa Dar es Salaam walikuwapo madaktari watano – Dr. Joseph Mutahangarwa, Dr. Luciano Tsere, Dr. Michael Lugazia, Dr. Vedasto Kyaruzi na Wilbard Mwanjisi.

Haya yalikuwa ni mapambano baina ya kizazi kipya na kile cha kale.

Katika mvutano huu wa madaraka kwa upande wa vijana waliokuwa wakiinukia katika siasa za Tanganyika alikuwepo kijana wa Kidigo kutoka Tanga aliyesomea Makerere na Uingereza - Hamza Kibwana Mwapachu.

Mwapachu alikuwa ameajiriwa na Idara ya Maendeleo ya Jamii kama 'Assistant Welfare' Officer, Ilala Welfare Centre mjini Dar es Salaam.

Historia ya Mwapachu katika siasa inaanza Makerere College, Uganda ambako alijihusisha na mambo ya siasa wakati alipokuwa mwanafunzi.
Mwaka wa 1947 Mwapachu akiwa Tabora alichaguliwa kuwa katibu wa African Association, Julius Nyerere akiwa Naibu Katibu.

Huu ulikuwa ndiyo wakati Wasomi wa Makerere ''Makerere Intellectuals,'' jina walilopewa na Judith Listowel walikuwa wameanza kujishughulisha na TAA.

Hamza Mwapachu na Abdul Sykes walikuwa na usuhuba mkubwa sana.
Kipande hiki hapa hakitoshi kueleza nini wazalendo hawa wawili walifanya katika kupigania uhuru wa Tanganyika.

Mwaka wa 1950 Mwapachu alikuwa na umri wa miaka 37 na Abdul Sykes alikuwa na umri wa miaka 26, mdogo kwa Mwapachu kwa miaka 11.
Vijana hawa wawili, Hamza Mwapachu na Abdul Sykes walikuja kugeuza mwelekeo wa TAA na wakaingiza ndani ya chama hicho aina mpya ya uongozi uliokuwa haujapata kuonekana katika historia ya Waafrika wa Tanganyika.

Lakini wote wawili walifariki dunia katika ujana.

Hamza Mwapachu akiwa na umri wa miaka 49 mwaka wa 1962 na Abdul Sykes miaka 44, mwaka wa 1968.

Jambo la kusikitisha na kushangaza ni kuwa wote wawili ilipokuja kuandikwa historia ya TANU hakuna hata ukurasa mmoja uliokuwa na majina yao.

Halikadhalika madaktari hawa watano historia yao haifahamiki.
Wote wamesahauliwa na historia.

Hakuna kati yao hawa ambaye hii leo jina lake linahusishwa na historia ya uhuru wa Tanganyika.

Tusichoke kutembea katika barabara waliyopita hawa wazalendo mashujaa wa uhuru wa Tanganyika.

Picha: Dr. Joseph Muhangarwa, Dr. Liciano Tsere, Dr. Vedasto Kyaruzi, Hamza Mwapachu, Abdulwahid Sykes na Thomas Saudtz Plantan.


Dr. Joseph Mutahangarwa


Dr. Luciano Tsere


Dr. Vedasto Kyaruzi


Hamza Mwapachu na Abdulwahid Sykes


Thomas Plantan
 
Back
Top Bottom