Kiwalani finest
Member
- Jul 6, 2024
- 97
- 72
Tunadharau malalamiko ya mafukara walio wanyonge, kisha tunawekea watoa rushwa kupata vyeo na kulazimisha mafukara wacheke wakubali waovu kuwa viongozi wao. Kisha, tunatoka hadharani kusema ya kuwa tunamsaidia fukara. Kwa matendo haya, tumelaaniwa kwa laana kubwa ingawa hatujioni wenyewe.
Nilisikika huko ndotoni nikitema cheche kukemea unafiki wa watu kijifanya wema huku wakiwa watu waovu na wakaidi wasiojali kauli za viongozi wakuu wa kitaifa na pia wasiojali ilani, katiba, kanuni, miongozo na taratibu. Bali matumbo yao ya faida wazipatazo kwa dhulma ya kutumia maneno ya hila na janja janja kuendelea kuwadumaza mafukara. Nikalianzisha huko huko ndotoni.
Lazima viongozi wakuu wa kitaifa waheshimiwe kwa kauli zao. Lazima maandiko ya kimfumo yatafsiriwe kwa vitendo na sio porojo zenye milengo ya dhulma. Tukitii ilani, katiba, kanuni, miongozo na taratibu kwa vitendo itakuwa ndiyo haki ibebayo maneno tuyatamkayo kuhusu kuwasaidia mafukara.
Nakumbuka tarehe 06/10/2024, Mheshimiwa Balozi Dkt Emmanuel John Nchimbi, Katibu Mkuu wa CCM Taifa, alisema: "Hiki ndiyo Chama kilichoanzishwa na Wazee wetu (Hayati Mwl Nyerere) (Hayati Mzee Karume), lakini chama ambacho kimeendelea kushika misingi yake kwamba hiki ni Chama Cha (watu) wanyonge. Chama kinachotetea maslahi ya watu." Mwisho wa kunukuu.
Utetezi wa watu ni kuwa waadilifu, waaminifu na watenda haki wenye kuwa tayari kuyafia maandiko yanayotufanya kujiita sisi ni wamoja. Nje ya haya ni dhulma, utapeli hila na janja zisizoweza kumsaidia fukara bali kundi dogo la watu waovu, wabinafsi, wauwa ndoto za kundi kubwa lililo changanyika na wapenda haki wenye kudharauliwa.
Ni lazima kwa mujibu wa ilani ya CCM 2020-2025 uk 161-168 na ibara 04 uk 01 na uk 08 ibara 10 na 11 vipewe kipaumbele kwa vitendo vyenye ucha Mungu ndani yake visivyokuwa na blabla za kijinga jinga.
Nakumbuka tarehe 08/10/2024, Mheshimiwa Balozi Dkt Emmanuel John Nchimbi, akiongea katika uwepo wa Mbunge wa Kisesa, alisema: "Mimi ni muumini wa utawala wa sheria. Kwamba napenda kila mtu katika nchi yetu afuate sheria. Na naamini kwa dhati kwamba ukiruhusu watu wawili, watatu, wawe juu ya sheria (ujuwe wewe unayeruhusu) unaharibu mfumo wa utawala bora katika nchi. Kwa hiyo kwanza nisisitize kwamba nataka kila Mtanzania afuate sheria bila shuruti. Yaani kila mtu asikie moyoni mwake kwamba anatimiza wajibu wake wa kiraia wa kufuata sheria katika nchi yetu. Kwa hiyo naomba kila Mwananchi aweke moyoni mwake kwamba anayo changamoto… Anayo sababu… Anayo dhima ya kuhakikisha kwamba sheria za nchi yetu anazifuata popote alipo, lakini pia anawashawishi (watu) wengine kufuata sheria." Mwisho wa kunukuu.
Katika chaguzi za kura za maoni, watu wasiokubalika kwa jamii walipuuza kauli za viongozi wakuu wa kitaifa. Wakatumia rushwa. Wakaita watu wasiokuwa wajumbe wa vikao wakawatumia kwa hila kama wapiga kura halali huku wakijuwa kufanya hivyo ni kuvunja sheria za nchi. Wakatoa rushwa ngazi za uteuzi zikapuuza maandiko ya mafukara ya malalamiko ya uvunjifu wa ilani, katiba, kanuni, miongozo na taratibu. Wakachukua wanaolalamikiwa kuwa ndiyo wagombea safi bila kuzingatia kauli na malalamiko ya mafukara huku wakijuwa watoa rushwa kununua vyeo hawana tija wala msaada kwa mafukara.
Kwa nini hawa viongozi wanaodharau na kupuuza malalamiko ya mafukara wanalindwa?!? Kwa nini watoa rushwa na wapindisha haki na sheria wanafanywa kuwa viongozi tegemezi wa mafukara?!? Hawa wote wanalindwa na nani?!? Haki tunazotangaza ziko wapi?!? Uhalali wetu wa kuiambia jamii ya kuwa sisi ni watenda haki wenye kusimamia sheria uko wapi?!? Wapi haki yetu ya kuilinda, kuihifadhi na kuitetea katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara 26(1)(2), ibara 09 a, b, f na h?!?
Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, akiwa katika hafla ya ufunguzi wa jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, nakumbuka tarehe 25/09/2024 alisema: "Utumishi wetu Mimi na ninyi ni kuhudumia wananchi. Sisi ni watumishi wa wananchi na si mabwana wa wananchi. Si watawala wa wananchi. Sisi ni watumishi kwa wananchi. Ndiyo yale niliyo waambia kwamba sisi serikali ni watumishi wenu. Kazi yetu ni moja tu, kuondosha shida zenu wananchi." Mwisho wa kunukuu.
Tusome katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977 toleo 2005 ibara 08(1) a,b,c,d. Ilani ya CCM 2020 uk 01 ibara 04. Naomba watu waliopenya kwa rushwa na wasiokubalika kwa mujibu wa kauli za viongozi wetu wakuu watolewe. Wasiruhusiwe kujihusisha na uongozi. Kiongozi bora huheshimu ilani, katiba, kanuni, miongozo na taratibu. Hawa waliokiuka wamepoteza sifa hatupaswi kuwakumbatia kivyovyote vile ili kulinda kauli za viongozi wakuu wanaotaka sheria zifuatwe.
Lazima tujisikie uchungu mioyoni mwetu wa kujifanya kama hatuoni mateso ya mafukara wanayopitia. Ni lazima tudhamirie kusimamia sheria ndani ya nchi ziwe kwa wote. Kulazimisha watoa rushwa wawe viongozi wa mafukara sio uzalendo ni ushenzi usiokuwa na utu zaidi ya ushetani.
Tukisoma kitabu kilicholewa na Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Agosti 2020 kiitwacho "Mwelekeo wa Sera za Chama Cha Mapinduzi katika Kipindi Cha Mwaka 2020-2030" uk 190 ibara 143 inatueleza: "Huwezi kuwa mwana wa nchi ukiwa huna uchungu wa nchi yako. Ni wajibu wako uitetee na kuipigania nchi yako. Huo ndiyo utu na huo ndiyo uzalendo." (Abeid Aman Karume Rais wa Kwanza wa Zanzibar) Mwisho wa kunukuu.
Sisi kama chama, tumeahidi kutenda haki na kuwa wasimamizi wa sheria kwa wote bila kushabikia uchawa. Tumekataa uongo na tunajiuliza, kwa nini tunawadharau mafukara na kujihusisha na tabia za kitapeli, huku tukijifanya watu wa haki? Ni wapi Mtume Muhammad alituamuru kutumia uongo, wakati tukiwa tunakula milo mitatu kwa siku?
Katika Maandiko Matakatifu, kitabu kiitwacho Muntakhab Ahadith uk. 789, Anas Bin Maliki Radhiallahu Anhu anasimulia kuwa Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam alisema: "Enyi watu, nipeni dhamana ya mambo sita, nami nitakupeni dhamana ya Jannah." Mambo hayo ni pamoja na: "Anapozungumza mmoja wenu asiseme uongo; anapoahidi asivunje; anapoaminiwa asifanye khiana; inamisheni macho yenu na idhibitini mikono yenu; na zichungeni tupu zenu."
Tunapaswa kuepuka mambo ya uongo, na tunajua majina yaliyorudishwa yameletwa na watoa rushwa ambao siyo chaguo la watu. Huu ni ushetani na unafiki. Tuwatokeze matapeli hao waovu wasiokuwa na hofu ya Mwenyezi Mungu.
Katika Muntakhab Ahadith uk. 672, Allah (Subhahanahu Wataalla) anasema: "Na saidianeni katika wema na ucha Mungu, wala msisaidiane katika dhambi na uadui." Watu wametumia rushwa na wanataka kuwaongoza mafukara, lakini wao ni watoa rushwa. Tunapaswa kuepuka kuwasapoti na tuwatoe sasa. Wamekiuka mifumo ya haki na ahadi za uadilifu zilizomo katika vitabu vyetu.
Kama chama, tunavunja sheria ya nchi The Political Parties Act, sura 258, na ibara 26(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mheshimiwa Jaji Francis Mutungi, Msajiri wa Vyama vya Siasa, alisema tarehe 26/09/2024 kuwa "Na mimi lazima niseme kwamba na sisi tunakemea vitu kama hivyo."
Katika Muntakhab Ahadith uk. 473, Abu Darda Radhiallahu Anhu anasimulia kwamba Mtume Swallallahu Alaihi Wasallam alisema: "Nitafuteni miongoni mwa wadhaifu, kwani mnaruzukiwa na kusaidiwa kutokana na wadhaifu miongoni mwenu." Tunapaswa kuwaondoa wababaishaji.
Kama tunashupaza shingo, tunajua kwamba hatumpendi Mtume na tunapenda unafiki kuliko imani zetu. Mheshimiwa Rais wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Albert John Chalamila, alikabidhi vitendea kazi kwa Jeshi la Polisi na alisema tarehe 07/10/2024, "Hoja yangu ya msingi inapofika pahala ambapo pana kweli na haki, katika kutetea ni muhimu tukafanya hivyo."
Mheshimiwa Rais Dkt. Hussein Mwinyi, akisema katika Sherehe za Maulid, alisema tarehe 18/09/2024, "Mtume Muhammad (SAW) ndiye kiigizo kizuri, kama alivyosema Mwenyezi Mungu katika Qur’an Sura ya Al-Hazzard aya ya 21."
Padre Dkt. Charles Kitima, Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki (TEC), alisema tarehe 27/04/2024, "Servant leadership means that you are a servant first before becoming a leader. The leadership comes later. You are after the success of the people you got to solve their problems."
Malalamiko ya mafukara yamekiukwa na watu wanafiki, wenye sura za kiucha Mungu. Tutende haki sasa. Kila aliyehusika kudharau malalamiko ya mafukara awajibike. Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, alisema tarehe 15/09/2021, "Nchi yetu inaongozwa kwa mujibu wa Sheria ambapo hakuna mtu aliye juu ya sheria."
Mheshimiwa Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, alisema tarehe 02/03/2020, "Rais aliyesema ndiye Mwenyekiti wa CCM, kwa hiyo kauli ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kauli ya CCM." Tarehe 14/10/2024, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alisema, "Tumepokea maoni, ushauri, na mapendekezo yaliyotolewa, na hakika tutakwenda kuyafanyia kazi."
Mwisho, tunasisitiza kwamba, tutachukua hatua kwa kuzingatia katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ibara 13(1)(4)(5) na ibara 09 a,b,f,h. Tunataka kuleta mabadiliko ya kweli kwa kushughulikia masuala ya kijamii kwa haki.
Kidumu Chama Cha Mapinduzi,
Mathias Mugerwa Kahinga