SoC02 Tusilishwe Uchafu Kilimo Kiboreshwe

SoC02 Tusilishwe Uchafu Kilimo Kiboreshwe

Stories of Change - 2022 Competition

Jade_

Senior Member
Joined
Apr 19, 2015
Posts
122
Reaction score
214
Umefika sokoni kununua maharage unakuta yamepangiwa magunia tofauti. Muuzaji anakueleza kuwa kila aina ya maharage yapo ndani ya gunia lake, na unaona yana mwonekano wa kutofautiana.

Anaandisisha kuwa maharage haya ni ya soya, haya huku ni mekundu na yale kule ni ya njano. Mchuuzi huyo anaainisha sifa za maharage yote na unachagua unayoyataka. Unaondoka na kilo mbili.

Maharage yanauzwa kwenye magunia sokoni

Mchoro: Maharage ya aina tofauti kwenye magunia tofauti sokoni.

Nyumbani ukifika unachambua maharage ili kuweka kando mawe na matakataka mengine yasiyolika. Baada ya uchambuzi unakadiria sazo ya maharage ipo kilo moja na robo tatu kutoka kilo mbili. Unatafakari iwapo maharage yanaota na mawe.

Bado jibu linachanganya zaidi na chanzo ni namna maharage yanavyoota kwenye vifungashio ambamo si rahisi chochote kiingie ndani. Je mawe mengi hivi na takataka nyingine zinaingiaje?


Maharage yakiwa na matakataka mengine

Picha: Maharage yakiwa na matakataka mbalimbali


Kilimo: Vifungashio vya maharage

Mchoro: Maharage yanavyoota kwenye vifungashio.

Ikiwa haiwezekani matakataka yaingie wakati mazao yanaota itakuwa upungufu upo wakati wa uvunaji, uhifadhi na usafirishaji unaofanya maharage yachafuke.

Ukiununua choroko sokoni utaonana na kituko zaidi ya maharage. Kuna siku nilichagua takataka na choroko zikabaki nusu ya kiasi nilichonunua. Choroko zinaotaje? Choroko zinaota sawa na maharage vifungashioni.

Haya matakataka yanaingiaje humo? Yanapeperushiwa humo? Yanavutwa na sumaku? Au ni mbinu moja wapo ya wadau wa kilimo kuongeza faida kwa kuweka uchafu ili uzito uongezeke? Hatukatai uchafu hauepukiki ila kuna kiasi, au pesa yangu inatumika kununua chakula na uchafu?

Kilimo: Vifungashio vya choroko

Mchoro: Choroko zinavyoota kwenye vifungashio.

Ni siku za karibuni nilipatiwa maarifa kumbe bamia hazichimbwi chini ilivyo viazi ila zinaota mitini. Nilifikiri bamia zinaota kama viazi sababu ukizinunua sokoni uje uzipike ni mpaka uzioshe sana ikiwezekana usugue na dodoki la chuma kuondoa udongo unaokuwa umejikumbatia kwake. Nahoji udongo na matawi ya mti wapi na wapi? Asaa bamia zinaota mitini zinafikiwaje na udongo tele? Naelewa kuna upepo unaopelekea vumbi ila haiwezi fanya bamia zichafuke sana na udongo ung’ang’anie.

Bamia chafu

Picha: Bamia zikiwa chafu baada ya kuziosha mara moja.

Je shida ni kipindi cha uvunaji, uhifadhi au usafirishaji? Au vyote? Wakulima na washiriki wengine wanatunzaje haya mazao baada ya kuvuna ili kuhakikisha thamani ya mazao yetu haipungui?

Sawa turudie maharage uliokua unaandaa. Unaamua kukubaliana na hali, unawasha jiko lako ili uyachemshe yaive kabla ya kuunga. Baada ya muda unakuja kuyaangalia na kuyageuza. Unakutana na yaliyoiva, mengine yanakaribia, na mengine hayana dalili ya kuiva, yaani ni magumu kama mawe. Hii inadhihirisha mpaka maharage yote ndani ya sufuria yaive, mengine yameshapondeka na kuwa uji au yameshika chini na kuungua.

Tatizo ni wauzaji au wakulima? Aina za maharage zinaanza kuchanganyika wakati wa kulima ambapo mbegu tofauti zinapandwa eneo moja bila kutengwa, au wakati wa kuvuna zinachanganywa moja kwa moja na kupelekwa sokoni? Au maharage yanakuja yametengwa na ni wauzaji wanayachanganya? Kulikuwa na haja gani ya wataalamu na watafiti kutenga aina za maharage au wauzaji kuyatenga kwenye magunia tofauti kama tunakuja kupika aina zote kwenye sufuria moja?

Hali ya maharage haitofautiani na ya viazi. Ukichemsha viazi, vingine vitaporomoka na vingine bado vitakuwa vigumu hadi kukosa ishara ya kuiva. Vingine vina maji ndani wakati kuna vyenye unga ndani. Ukikumbuka unavyonunua uliambiwe vyote ni aina moja.

Tunasisitiza tunataka kupeleka chakula nchi nyingine duniani isipokuwa ubora wetu una dosari. Ikiwa hatuwezi kutenganisha aina moja ya zao ili tukiuza tuweke katika makundi tofauti, tutaonekana tuko makini kweli? Tutaaminika? Natoa tahadhari, ukimwambia wa kwenu ‘vaa’ akakataa, ukutanapo na wanaocheka nawe hucheka.

Upo uwezekano vile vya kuuza nje ni vizuri kuliko ya tunavyotumia ndani, nawaza, Watanzania hatufai kula vitu vizuri?

Tuongeze thamani ya mazao yetu na si lazima kila kitu kizidi usafi, au kifunganywe katika plastiki. Tumpunguzie mzigo mtumiaji, akifika nyumbani, achambue kidogo na aoshe kuondoa vumbi la pale sokoni.

Wakulima na wafanyabiashara wakifanyia kazi upandaji, uvunaji na uhifadhi mzuri basi hawataingia gharama za ziada katika kuboresha bidhaa zao.

Yai halitamii kuku. Hatuwezi kuongelea ubora wa mazao kabla ya kushirikisha wataalamu. Kilimo hakiwezi kuendelea bila tafiti na tafiti lazima zifanywe mara kwa mara kwa kuwa hali ya hewa hubadilika, pamoja na virutubisho na viumbe hai vinavyoingiliana na mimea. Mahitaji ya watu na yenyewe hubadilika.

TARI inajitahidi kufanya kazi na wakulima ila safari bado ni ndefu. Tafiti zao na machapisho yenye maelezo ya kutosha hayapatikani kiurahisi hasa mtandaoni ambako mtu anaweza kupata maelekezo haraka. Tafiti zao ni chache, kwa hiyo waziongeze ili kukutia kila kinacholimwa Tanzania. Ni muhimu tafiti hizi ziwepo katika lugha ya Kiswahili.

Mzigo wa tafiti usiachiwe TARI pekee, vyuo vikuu na majeshi (mfano SUMA JKT na Magereza) yasibakie kulima tu yafanye tafiti zao ili kuboresha na kuongeza aina ya mazao hapa nchini.

Si hivyo tu bali kuwe kuna viwango vya kudhibiti ubora. Mazao yakaguliwe aidha huko yanakotoka au sokoni yanapofikia kabla hayajampata mtumiaji. Wizara ya Kilimo kupitia idara ya “Crop Development” idhibiti ubora wa bidhaa zinazouzwa kote Tanzania kabla watu hawajaanza kuuziwa. Serikali inatakiwa ihakikishe ina macho kila kona ili ijue ni nini wakulima na wafanyabiashara wanauzia watu. Kitu kama hiki kimeanza kutekelezwa kwenye mifugo lakini isishie kutambua wanyama ije kutambua mimea.

Rasilimali watu ya ziada itahitajika, sambamba na matumizi ya teknolojia, yenye kuwezesha ufuatiliaji na kupunguza mianya ya rushwa itakayojitokeza.

Tunahitaji wataalamu wa kilimo na teknolojia kutoka vyuo vikuu na vyuo vya ufundi watakaosaidia kutengeneza na kusimika mitambo-fuatilizi ili kutengeneza mifumo madhubuti ya kulinda na kusimamia ubora wa mazao tangu yanapooteshwa. Ni ngumu lakini inawezekana kutambua kila mmea unaoenda kuuzwa hapa Tanzania.


Kilimo; Utambuzi wa mimea kama mahindi, mchicha na magimbi

Mchoro: Utambuzi wa kila mmea Tanzania

Mamlaka ziwe karibu na wakulima tangu wanapoanza kupanda mazao ili kutambua changamoto na wasisubiri kuwakata kodi kupata mapato.

Tusijenge masoko pekee bali tuhakikishe yale yanayouzwa sokoni yanaendana na hadhi ya masoko yenyewe. Masoko yawe na vitengo vya kukagua bidhaa zote kabla hazijaruhusiwa kuwepo vizimbani. Kila muuzaji anajua anapotoa bidhaa zake, hivyo ni ngumu masoko kudhibiti. Lakini mazao yote nchini yakipata ithibati ya ubora kabla ya kuuzwa, masoko yatakagua ile ithibati kuhakikisha yanayouzwa yana ubora.

Tupige hatua kwa kuweka juhudi za makusudi kwa kupanga mipango ya muda mfupi na mrefu, tusikubali kubaki hivi tulivyo. Baadhi ya tunavyolishwa unajiuliza ni mimi binadamu ndio ninaletewa ninunue na nile? Tujipende na tuwe na chachu ya vitu vizuri ambavyo vitasaidia kuboresha maisha yetu.
 
Upvote 2
Ahsanteni kwa kusoma andiko langu. Msisite kutoa mawazo na kulipigia kura andiko hili kama limekupendeza.
 
Habari yako ndugu, Jade.

Hongera kwa nakala nzuri yenye mawaidha na tija kwa jamii.

Kura yangu umepata!!

Nikiamini katika uchakataji wako wa mambo na uwezo wako wa fikra na ubunifu, naomba ukipendezwa, nipate mawazo yako au mapendekezo juu ya nakala ihusuyo


Ahsante!!
Ahsante mkuu. Ngoja niipitie nakala yako.
 
Kama una swali au unafahamu zaidi kuhusu kilimo usisite kuacha mchango wako hapa.
 
Naendelea kutafakari. Mazao ya kilimo yana harabika pia wakati yanashushwa sokoni kuwafikia wanunuaji. Unakuta viroba vya mazao vinatupwa chini kwa nguvu kutoka kwenye magari kana kwamba sio chakula.
Je hatuwezi kuwa makini zaidi?
 
Nasisitiza kuboresha usafi wa chakula si kufanganya kwenye plastiki. Plastiki nazo zina madhara yake
 
Makala nzuri sana hii..
Tunakula chakula kimejaa taka mnooo, yaani hatuzingatii suala la usafi na ubora kwenye mazao yetu kwakweli.
Kuna haja ya kubadilika sana
 
Bodi za mazao husika zinapaswa kuweka viwango visimamiwe
 
Makala nzuri sana hii..
Tunakula chakula kimejaa taka mnooo, yaani hatuzingatii suala la usafi na ubora kwenye mazao yetu kwakweli.
Kuna haja ya kubadilika sana
Kweli mkuu. Kama tunataka nchi yetu iwe na maendeleo kwa kupiga hatua lazima tuboreshe mazao yetu ya kilimo. Hali sio nzuri.
 
Back
Top Bottom