SoC01 Tusipofuata ushauri wa wataalamu Corona itatumaliza

SoC01 Tusipofuata ushauri wa wataalamu Corona itatumaliza

Stories of Change - 2021 Competition

Chu joe

Member
Joined
Jul 15, 2021
Posts
7
Reaction score
3
Na Chu Joe

Asiyesikia la mkuu huvunjika guu ni methali tuliyoachiwa na wahenga ikimaanisha asiyefuata ushauri wa wakuu wake, mabaya humpata, hii inasadifu hali ya watanzania wengi kwasababu tumeacha kujikinga na virusi vya Corona wakati tunafahamu virusi hivyo ni hatari.

Wananchi wengi kwasasa tumeacha utamaduni wa kujikinga na hatuchukui tahadhari zozote dhidi ya ugonjwa wa Covid 19, wakati ni wazi gonjwa hili ni hatari na limeondoka na maisha ya watu wengi huko ughaibuni.

Wakati tuliofikia sasa tunapaswa kubadilika na kuanza kuchukua tahadhari ikiwemo kunawa mikono kwa sabuni na maji safi yanayotiririka, kuvaa barakoa, na kujiepusha na mikusanyiko isiyo ya lazima ili kuziokoa afya zetu.

Rais Samia Suluhu Hassan, na Waziri wa afya Dkt Doroth Gwajima kwa nyakati tofauti wamekuwa wakitusihi wananchi kuendelea kuchukua tahadhari, kwani ugonjwa wa Covid 19 ni tishio kwa usalama wa maisha yetu lakini bado tumeendelea kuwa wakaidi.

Viongozi wa dini pia wamejitahidi kutusihi watanzania kujikinga kama alivyofanya Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Frederick Shoo na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Gervas Nyaisonga, ambaye alitoa waraka wa tahadhari dhidi ya virusi vya corona.

Kwa tahadhari zilizotolewa na viongozi tofauti ni wazi tunapaswa kubadilika na kufanya tunayoelekezwa na wataalamu wa afya kwani hali sio shwari, lakini bado watu wanaendelea kukusanyika bila sababu ya msingi na hawavai barakoa wala kutakasa mikono kwa maji safi au vitakasa mikono.

Hatupaswi kupuuza tahadhari hizo kwasababu kama tusipojilinda wenyewe hakuna wa kuja kutulinda, kwahiyo ni vyema kila mmoja kwa nafasi yake kujilinda yeye na familia yake na kuwalinda watu wengine.

Tusisubiri yatukute yaliyowapata wenzetu ili tuchukue hatua kwani wakati ni sasa, bado tuna idadi ndogo ya waliokumbwa na janga hili kwahiyo kama tukichukua hatua mapema basi ugonjwa huu hautaenea zaidi na tunaweza tukaumaliza.

Tuendelee kunawa mikono kwa maji safi yanayotiririka na sabuni, tuvae barakoa na tutakase mikono yetu, pia tuepuke mikusanyiko isiyo ya lazima ili sisi pamoja na taifa letu pendwa Tanzania tubaki salama.

Wahenga walisema asiyesikia la mguu huvunjika guu na mimi namalizia kwa kusema tusipowasikiliza wataalamu wa afya na kuchukua tahadhari basi tutaangamia kwa Covid 19, kuishinda Corona kwa pamoja tunaweza.

images-1.png
Mchoro ukionesha tahadhali unazotakiwa kuchukua ili kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona, (picha na mtandao).
 
Upvote 2
Back
Top Bottom