SoC02 Tutaingia wenyewe

Stories of Change - 2022 Competition

Babuakilihuru

New Member
Joined
Nov 21, 2020
Posts
1
Reaction score
1
Huwezi kuepuka kula kama unataka kuishi, virutubisho vinavyopatikana katika chakula ndivyo hufanya maisha waye endelevu kwetu, mwili na akili hujengwa kwa vyakula tunavyokula kwa makundi yake. Swali laweza kuwa, ule nini? Swali hili ni rahisi sana kulijibu kwa sababu kila mmoja huchagua kula chakula anachokipenda na kwa wakati ambao ni sahihi wake. Swali rahisi zaidi ni hili, chakula chatoka wapi?, kila mtu anajua jibu la swali hili, chakula chatoka shambani, mkulima hufanya kazi msimu mzima na mara kadhaa huamua kukaa shambani siku zote akilima ili kiwepo chakula majumbani.

Ulimwengu umebadirika, uvumbuzi katika nyanja ya sayansi na teknolojia una mchango mkubwa katika kukua kwa nyanja muhimu za maendeleo ikiwemo nyanja ya kilimo, teknolojia inaokoa muda na gharama zisizo za lazima katika uzalishaji. Uhakika wa chakula cha kutosha nyumbani hufanya mambo mengine yafanyike kwa weredi mkubwa kuanzia katika ngazi ya familia, jamii na nchi kwa ujumla, familia haiwezi kuwa salama kama njaa imeingia nyumbani kadharika jamii na nchi haiwezi kujikita katika kuandaa mipango ya maendeleo kama vile utoaji wa huduma za kijamii na miundombinu ikiwa inakabiliwa na janga la njaa.

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa mataifa (FAO) na Shirika la Mpango wa Chakula duniani (WFP) hutoa ripoti ya hali halisi ya uwepo wa chakula duniani, ripoti hizo ni ishara mbaya sana hasa ukizingatia madhara yatokanayo na janga la njaa, mfano halisi ni janga la njaa la mwaka 1998 linalojulikana kama Elnino, licha ya hivyo vyombo vya habari duniani kote huripoti namna njaa inavyowakabili watu mahali mahali fikiria kuhusu sudani ya kusini, yawezekana sisi Tanzania tupo katika hali nzuri zaidi, changamoto tunayoipata ni moja tunajipanga vipi kuhakikisha kuwa hatuingii kwenye mtego wa janga la njaa.

Hadithi za vitabu vya kiimani huzungumzia madhara ya njaa kama huleta utumwa, ukiwa na njaa utakubali kufanya chochote unachoambiwa na mwenye chakula, kitabu cha Mwanzo sura ya 47 aya ya 13 mpaka aya ya 25, nanukuu aya ya 25 “Wakasema, Umetulinda hai, na tuone kibali machoni pa bwana wetu, nasi tutakuwa watumwa wa Farao.” Pia hadithi ya Esau na Yakobo inaonyesha madhara ya njaa, Esau anazipoteza baraka za uzaliwa wa kwanza kwa ajili ya dengu.

Kwanini turuhusu njaa itutawale wakati tunazo njia za kuiepuka? Ni kweli tumeshindwa kuwa wabunifu wa kujiwekea akiba ya chakula mpaka tuwe watumwa? Tushindwe kujipambanua kifikra na kimtazamo sababu ya njaa? Hapana, tunazo njia nyingi za kuuepuka utumwa nyumbani kwetu, wenye hekima wanajua kuwa “ulapo ndipo penye fadhili yako”.

Wahenga wa lugha adhimu ya kiswahili wanao msemo usemao, “uvivu na njaa ni ndugu pacha” kimsingi njia pekee ya kuepuka njaa ni kuachana na uvivu ambao ndiyo tatizo kubwa kwa vijana wa kizazi hiki, haimaanishi kwamba wote twende shamba tukalime, hapana lengo kila mtu afanye kazi anayoweza kuifanya katika ngazi ya familia mpaka ngazi taifa itakayoweza kuleta kitu chenye manufaa kwa familia na nchi yetu. Lengo ni kuzitumia fursa zilizopo kutatua matatizo yanayoikumba jamii ya Tanzania.

Uhuru huja kwa kufanya kazi na kujitegemea. Wazazi na walezi wanayo kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha kuwa vijana wao wanakuwa sehemu ya maendeleo ya familia, ushirikishwaji wa kundi hili muhimu na kubwa katika majukumu ya kifamilia huwajengea tabia ya kujiamini katika majukumu wanayopewa wakiwa nyumbani hata pale watakapo kuwa wameyaanza maisha yao mbali na nyumbani, wahenga hawakuacha jambo hili liwapite bure wazazi au walezi wakawaambia “mtoto umleavyo ndivyo akuavyo”, kwa maana kwamba, kama mzazi au mlezi hatamshirikisha huyu kijana kwenye majukumu ya familia, kijana hataona kama anatakiwa kushiriki majukumu na kila kitu kinachofanywa ataona kitapaswa kufanywa na mzazi au mlezi hata yale majukumu madogo ambayo yanaweza kufanywa na mtu yeyote mwenye akili timamu.

Mfumo wa maisha umebadilika, miaka ya zamani kidogo ilikuwa ni nadra sana kumkuta kijana nyumbani amelala mchana kama si mgonjwa, wazazi walikuwa bega kwa bega na watoto wao, vijana wa kiume wanafanya kazi pamoja na baba kadharika mabinti wapo na mama wanajifunza kazi, vijana walipewa nafasi za kukosea kazi hadi pale watakapokuwa wabobevu wa kazi wanazofundishwa, hatupishani na nyakati mambo yamebadilika, sasa vijana wanapata nafasi za kwenda shule wanamaliza masomo yao wanatunukiwa vyeti na shahada zao, kilio chaja hakuna ajira. Vijana wanaamua kulala nyumbani kusubiri ajira, ajira haziji haraka kama walivyodhania wakiwa vyuoni bahati mbaya zaidi hawajatengenezewa uwezo wa kuamua na kufanya vitu bila utegemezi, mzazi au mlezi atafanya lakini kijana hawezi. Hii haiathiri familia tu bali nchi kwa ujumla.

Wapo waajiri wanaoamua kuwaamini vijana, “ Vijana wanazo nguvu” ni msemo mashuhuri sana kuwahusu vijana hii ikiwa na maana wanaweza kufanya mambo makubwa wakipata nafasi, nafasi zipo chache, wachache wanazipata nafasi hizo, swali gumu zaidi kwao ni wanawawakilishaje vijana wenzao katika ajira walizozipata?,

Bahati mbaya zaidi kwao waajiri wanawapima katika mambo mengi ili imani iongezeke vijana wengine wapate nafasi, tathmini zinaonyesha kuwa vijana wengi ni wavivu, kwa maana ipi? Kazi zinatakiwa zifanywe kwa weredi mkubwa na kwa wakati uliopangwa, hapo vijana wengi walioajiriwa wameingia mtegoni na wamenasa, jambo lingine ambalo waajiri wanaliangalia kwa vijana ni tabia za vijana kwa ujumla, kuanzia mwonekano wako, ufanyaji kazi na namna unavyoweza kushirikiana na waajiriwa wengine kuleta manufaa kwa mwajiri, ukubali wa kujifunza na mwisho ubunifu wa vijana katika kufanya kazi, hapa vijana wengi wanashindwa kwa sababu uhalisia ulivyo ni huu mambo waliyosoma vyuoni hayapatikani moja kwa moja kazini.

Hivyo basi vijana waliopata nafasi za kuajiriwa wawakilisheni vyema wengine waajiri waone kuwa vijana wanaweza kufanya kazi kwa weredi mkubwa na kiwaletea manufaa, tabia njema ni muhimu zaidi kwa sababu humtambulisha mtu zaidi kuliko kitu chochote. Tabia njema hushinda vyote.

Tutaingia wenyewe utumwani, tutaingia wenyewe kwenye mtego wa waajiri, tutaingia wenyewe shimoni, tutaingia wenyewe matatizoni, tutaingia wenyewe kwenye mijadala ya lawama, kuilaumu serikali wakati huo serikali inatusubiri sisi tuiwezeshe ili itekeleza majukumu yake.

Usisubiri uingie huko nafasi inayopatikana itumie kwa akili nyingi na unyenyekevu, heshimu kila mtu, kubali kujifunza kila siku.

Imeandaliwa na,
Cley.
 
Upvote 1
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…