Tuwekane sawa kuhusu mafuta, gesi

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Joined
Feb 3, 2009
Posts
42,872
Reaction score
34,363
KWA UFUPI
Kwa kauli kama hizi, nachelea kusema kuwa viongozi hawaonyeshi ushirikiano wa kutosha kwa wazawa na badala yake wanawakatisha tamaa.


Ama kwa hakika neema ya kipekee imetufikia Watanzania baada ya gesi na mafuta kuvumbuliwa katika ardhi yetu mbali ya kugundulika kwa madini mbalimbali na urani.

Kila mmoja amepata tumaini jipya, huku matone ya faraja yakidondoka katika mioyo yetu baada ya kufahamu kuwa sasa nchi yetu imepata rasilimali muhimu ambazo zinaweza kuinua hali yetu ya kiuchumi ambayo hapana shaka ingali mahututi.

Lakini bado yapo maswali kadhaa kuhusu rasilimali hizi muhimu kwani wafanyabiashara wazawa na wananchi wengine kwa ujumla hawafahamu watanufaikaje na pia hawafahamu jinsi serikali inavyouuza rasilimali hizo.

Licha ya Rais Jakaya Kikwete kusema kuwa uwekezaji katika sekta ya mafuta na gesi utakuwa kwa manufaa ya Watanzania, lakini wadau wakuu katika sekta hiyo bado wanatoa kauli tata kuhusu masuala ya nishati hiyo.

Kwa mfano, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi hivi karibuni alisema vikampuni vidogo vidogo vilivyopo nchini haviwezi kuingia kwenye ushindi, akaongeza kuwa vikampuni vyenyewe, vimejaa rushwa.

Kwa kauli kama hizi, nachelea kusema kuwa viongozi hawaonyeshi ushirikiano wa kutosha kwa wazawa na badala yake wanawakatisha tamaa.

Kutokana na kauli hizo, inasemekana kuwa, wafanyabiashara wa kigeni ambao walitarajia kushirikiana na kampuni za ndani wameacha kabisa kufanya kazi na kampuni za ndani za mafuta na gesi, kwa kile walichoaminishwa kuwa zimejaa rushwa na hazina uwezo.

Siyo kauli hii tu, zimekuwapo kauli nyingi ambazo zinaonyesha kuidunisha sekta binafsi ya mafuta na gesi Tanzania kwa mfano hata Waziri wa Nishati na Madini, Sospeter Muhongo alisema, kampuni za gesi Tanzania ni wachuuzi na matapeli na kuwa wana uwezo mdogo wa kuwekeza katika sekta hiyo.

Inafahamika kuwa, hata kama mtoto wako mdogo hajui kutembea vyema au kula inavyotakiwa, anatakiwa apewe moyo ili ajitahidi kula vizuri.

Lakini kwa kauli hizi za udunisho na za kukatisha tamaa kwa kampuni za mafuta na gesi nchini, tutaendelea kuwa duni kwa miaka nenda miaka rudi kwa sababu hatusifiwi wala mchango wake hautambuliwi hata kwa kile kidogo inachochangia.

Siyo hivyo tu, baadhi ya kauli zilizotolewa kuhusu kampuni binafsi za nishati hiyo nchini ni kwamba, hazina mitaji, haziwezi kufanya biashara na mtaji wao labda mitaji yao inafaa kuuza matunda tu.

Kwa mtazamo wangu hatuwakatai wawekezaji kwa kuwa wanasaidia kuinua uchumi wa nchi, lakini tukumbuke kuwa rasilimali hizi ni za Watanzania, zinatakiwa zitumiwe na Watanzania wote, hivyo wawekezaji wanaokuja hapa hawana budi kushirikiana au kuingia ubia na kampuni za ndani. Ni nchi ipi duniani yenye viongozi wenye uwezo wa kujiamini kuzungumza hadharani wakiziponda kampuni zao ndani? Kwa hili, sina chembe ya shaka kuwa, tumekuwa makandarasi na wahandisi wa anguko letu wenyewe kwa kutotoa ushirikiano na kipaumbele kwa kampuni za wazawa.
Kwa mtazamo mwingine, hatuna teknolojia wala vifaa vya kuchakata mafuta na gesi, lakini ni lazima sera iwe na upendeleo kwa wazawa ili waweze kunufaika.

Mtaalamu wa masuala ya mafuta na gesi, Farouk Al- Kasim anasema Tanzania haina budi kuchukua tahadhari kuhusu rasilimali hiyo kwani nchi nyingi duniani zimeingia kwenye matatizo ya kiuchumi licha ya nishati hiyo muhimu kupatikana. chanzo. Tuwekane sawa kuhusu mafuta, gesi - Uchambuzi - mwananchi.co.tz

 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…