Felix Mwakyembe
Member
- Feb 13, 2017
- 9
- 16
Taasisi ya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania, MISA TAN, imeanzisha tuzo maalumu kuwatunukia Watanzania wenye mchango ulio bayana katika uhuru wa kujieleza nchini.
Tuzo hiyo itakuwa ikitolewa kila mwaka kwenye kongamano lake la kila mwaka ka Uchechemuzi wa Hali ya Uhuru wa Kujieleza, Haki ya Kupata Taarifa na Uhuru wa Wanahabari, na kwa kuanzia mwaka huu iliwatunukia wadau saba.
Ni hatua muhimu na sahihi kwa MISA kuthamini mchango wa wale wote wenye kuhakikisha unakuwepo uhuru wa kujieleza na habari nchini, ikizingatiwa kuwa huru wa habari ndio shughuli yake ya msingi, hivyo kutambua mchango wa wale wenye kuupigania kwa vitendo ni hatua muhimu.
Hakuna asiyetambua mchango na misimamo ya Watanzania, Maxence Melo, Ndimara Ntengabwage, Richard Mabala, Ally Masoud, Prof Issa Shivji, Salma Said na Twaha Ulimwengu katika uwanja huo wa uhuru wa kujieleza kwani wamethibitisha umahiri wao kwa vitendo na sio nadharia.
Hawa ndio vinara wa kwanza kutunukiwa tuzo hiyo, hafla iliyofanyika Juni 01, mwaka huu katika Hoteli ya Hyatt Regency, wakati MISA ikihitimisha siku mbili za tafakuri kuhusu uhuru wa kujieleza nchini kwa mwaka 2023/2024.
Ndimara Ntengabwage ni mmoja wa waasisi wa taasisi hiyo kuanzia hatua ya wazo lake, pale Windhoek nchini Namibia, anaielezea hatua hiyo kuwa ni kitu kikubwa na cha thamani.
"Ni kama wanasema kwa Kiingereza, "it's a gem," ni kitu kikubwa ambacho quality yake vile vile ni kubwa, na waliokileta ni watu wanaohitaji kuheshimiwa kwa kitu cha namna hiyo," anasema Tengabwage, na kuongeza,
"Kwanza kinaonyesha jinsi wanavyofanya kazi yao, wanavyoi evaluate na jinsi wanavyotaka ionekane na hata kwa watu mbali mbali, pili inaonyesha wanavyofuatilia, kwamba kazi yetu imefika wapi, imefanywa na nani, tulianzia wapi na sasa hivi tukoje."
Tuzo hizo zilikabidhiwa kwa wateule na aliyekuwa Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi, ambaye kitaaluma ni mwandishi wa habari pia, na katika maelezo yake alikubaliana na hatua ya MISA-TAN kuanzisha tuzo hizo ikiwa ni ishara ya kuheshimu na kuthamini mchango wa wale wote wenye uthubutu wa kuchangia katika dhana zima ya uhuru wa kujieleza.
Matinyi alielezea hatua ya serikali kufungulia magazeti manne, mara baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuingia madarakani, kuwa ilionyesha dhamira ya kweli na mwelekeo sahihi katika kulinda uhuru wa kujieleza.
Katika kuhakikisha dhamira hiyo inafikiwa, Matinyi aliwafahamisha waandishi wa habari na wadau wa habari kuhusu kuwepo mchakato wa kufanyiwa mapitio ya sera ya habari na utangazaji na huduma ya habari kuhakikisha uwepo uhuru wa habari wa kweli.
"Nafurahi kufanya kazi nikiwa na amani kwa nchi ambayo inaheshimu uhuru wa habari," alisema Matinyi.
Wengi ni mashahidi wa vinara hao saba waliotunukiwa mwaka huu, katika nyakati tofauti wamedhihirisha kwa vitendo uthubutu wao kwa kutokutetereshwa na kubalidilikabadilika kwa mazingira ya uhuru wa kujieleza nchini, bali waliendelea na msimamo wao ule ule wa kutetea uhuru wa kujieleza na uhuru wa habari, na hata walipopata misukosuko, bado waliendelea kusimamia kile wanachokiamini.
Miongoni mwa misukosuko waliyokabiliana nayo kutokana na kazi zao ni pamoja na kukamatwa, kushitajiwa na hata kuhojiwa uhalali wa uraia wao, lakini pamoja na yote hayo waliendelea kusimamia walichokiamini kuwa sahihi.
Tuzo hizo zilikabidhiwa kwa washindi na Matinyi, katika siku ya pili ya Kongamano la mwaka kuhusu Uchechemuzi wa Hali ya uhuru wa Kujieleza, Haki ya Kupata Taarifa na Uhuru wa Wanahabari, mwaka 2024 lililofanika kati ya May 31 na June 02, mwaka huu jijini Dar es salaam.
Katika kongamano hilo walikuwepo pia Balozi wa Marekani hapa nchini, Michael Battle na Balozi wa Finland Theresa Zitting, wote wakiahidi kuendelea kusaidia ukuaji wa uhuru wa kujieleza nchini Tanzania kama nyenzo muhimu katika ukuzaji demokrasia.
Washiriki wengine ni pamoja na Foundation for Civil Society (FCS), Taasisi ya Kimataifa ya Demokrasia ya Marekani (NDI), Shirika la Kimataifa la Finland Vikes, Taasisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binaadamu, Jumuiya ya Ulaya na wadau mbali mbali wa habari.
Utoaji tuzo hizo ni jambo endelevu, na katika maelezo yake ya utangulizi, Mkurugenzi wa MISA-TAN, Elizabeth Riziki alithibitisha hilo akisema tuzo hizo zilizotolewa kwa vinara hao saba wa uhuru wa kujieleza ni mwanzo tu kwani ni tukio endelevu.
"Tulichagua watu wachache wa kuanza nao ambao wamekuwa wachechemuzi na vinara wa uhuru wa kujieleza bila kuvuruga amani wala kukiuka sheria za nchi" amesema Riziki.
Makamu Mwenyekiti wa MISA-TAN, Wakili James Marenga aliungana na mkurugenzi wake akisisitiza kuwa tuzo hizo ni mwanzo tu, na kwamba taasisi hiyo ameamua kutambua mchango wao kwa kuwapatia tuzo wakingali hai.
Kilichofanywa na MISA TAN ni hatua inayoonyesha kuthamini mchango wao mkubwa katika tasnia ya habari na uchechemuzi wa uhuru wa kujieleza nchini na kujenga moyo wa kujiamini kwa wananchi zaidi kuelezea fikra na mawazo yao bila hofu.