Tafakuri Jadidi
Twahitaji rais mhemea vibaba?
Johnson Mbwambo
Septemba 15, 2010
"......Na tunapokuja kwenye suala la kuchokwa na wafadhili, nakumbuka nilipokuwa nimelazwa THI nilisoma, kwenye gazeti la Mwananchi, kauli moja ya Jakaya Kikwete aliyoitoa wakati akihutubia mkutano wa kampeni huko Mbeya.
Kauli hiyo ilinikera kiasi cha kusababisha mapigo yangu ya moyo kuongezeka na kunifanya ghafla nizidiwe (tangu tukio hilo magazeti yakazuiwa kuingia wodini chumbani kwangu).
Kauli hiyo ni ile aliyoitoa kuwajibu wanaomshutumu kwamba anatumia mapesa mengi ya walipa kodi kufanya ziara nyingi za nje zisizo na ulazima. Alisema maneno mengi kuhalalisha ziara hizo, lakini yaliyoniacha hoi ni haya:
Mimi nakwenda kule (Ulaya na Marekani) kuhemea. Nikirudi narudi na kibaba.
Kwa mtazamo wangu, haya ni maneno ya hovyo kutamkwa na rais wa nchi kuliko mengine yote yaliyopatwa kutamkwa na Kikwete. Hata yale kwamba wasichana wanaopata mimba shuleni ni kwa sababu ya viherehere vyao, hayafikii hayo aliyoyatoa kwenye kampeni mkoani Mbeya.
Mimi nakwenda kule (Ulaya na Marekani) kuhemea. Nikirudi narudi na kibaba, ni maneno ambayo ukiyatafakari utagundua kwamba yanatolewa na mtu anayeifurahia hali hiyo.
Ningemwelewa Kikwete kama angeueleza umati ule kwa hali ya kusikitisha kwamba sisi Watanzania tunamwangusha kwa sababu hatuchapi kazi vya kutosha; kiasi cha kufikia hatua ya kujitegemea, na hivyo tunamfanya ajidhalilishe kwa kwenda Ulaya na Marekani kuombaomba hata mambo ambayo tungeyamudu wenyewe kujitafutia.
Ningemwelewa Kikwete kama angeielezea hali hiyo kwa uchungu na kwa masikitiko, na hata kutisha kwamba hatakubali tena kwenda Ulaya na Marekani kuombaomba mambo ambayo sisi wenyewe tuna uwezo nayo (kama vile kutengeneza na kusambaza vyandarua vya bei nafuu).
Lakini sivyo alivyofanya kwenye hotuba hiyo. Kikwete aliitoa kauli hiyo kwa namna inayoonyesha kwamba anazifurahia ziara hizo za nje za kuomba misaada. Kwa maneno mengine, ujumbe wake kwa waliokuwa wanamsikiliza ulikuwa huu:
Nichagueni mimi; maana ni hodari wa kwenda nje kuhemea na kurudi na vibaba.
Labda niwaulize Watanzania wenzangu: Je, tunamhitaji rais anayefurahia kutembeza bakuli la omba omba nje ya nchi au tunahitaji rais mwenye uwezo wa kutujengea misingi ya kujitegemea?
Je, kuna nchi dunia iliyopata kuendelea na kuondokana na umasikini kwa kutegemea misaada ya nje ya nchi? Je, ni familia gani duniani iliyopata kujikomboa kwenye umasikini inayoongozwa na baba ambaye kila kukicha hutembelea nyumba za majirani kuhemea vibaba vya unga kwa ajili ya ugali wa wanawe?
Ndugu zangu, tunapokuwa na rais wa nchi anayeona ni jambo la kawaida na linalofurahisha kwenda Ulaya na Marekani kuhemea vibaba, hatuwezi kamwe kujenga utamaduni wa kujitegemea.
Kwa hakika, rais wa namna hiyo huwa ana udhaifu mmoja mkubwa; nao ni kwamba si kiongozi
visionary. Si kiongozi mwona mbali anayeifikiria Tanzania ya miaka 50 ijayo. Na si kuifikiria tu; bali kuweka misingi na mwelekeo wa kuifikia.
Najua kuwa wanayo hiyo wanayoiita vision 2025 iliyopo kabatini. Nadhani waliiandaa tu ili wakiulizwa kama wanayo wajibu ndio, lakini si kuifuata.
Kwa hiyo, mnapomchagua mtu asiye na
vision kumiongoza, mjue kwamba mtapotea na mtatangatanga nyikani; maana hana uwezo wa kuiona njia itakayowatoa nyikani.
Labda nikumbushe kwamba Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere aliiona njia mapema na aliwaonyesha hawa kina Kikwete njia ya kutokea nyikani, lakini wameitelekeza, na ndiyo sababu tunatangatanga nyikani.
Naamini kwamba kama Kikwete na CCM yake ya sasa, ambayo imekumbatia mafisadi, atashinda uchaguzi mkuu wa Oktoba 31, basi, tujue wazi kwamba tutakuwa tumejikatia tiketi nyingine ya miaka mingine mitano ya kutangatanga nyikani.
Nasema hivyo bila kupepesa kope; maana kiongozi anayefurahia kuhemea vibaba Ughaibuni, hakika, si yeye wa kututoa nyikani.
Nihitimishe kwa kusema kwamba, kwa sasa, tunaweza kuikejeli siasa ya Ujamaa ya Mwalimu Nyerere, lakini ni upofu na ujinga kuitelekeza dhana yake ya Kujitegemea.
Ndugu zangu, Tutakuja kulipia kwa makosa hayo kama ambavyo tumeanza sasa ambapo tunasaidiwa hata vyandarua, na tunachekelea kwa hilo!
Huko mbele tutakuja kusaidiwa na Wazungu hata miswaki, na kwa ujinga wetu tutaendelea kuchekelea; huku wenzetu tuliokuwanao nyuma wakichanja mbuga kiteknolojia na kimaendeleo kiasi cha kufikia hata hatua ya kutuma vyombo anga za mbali!
Wakati wenzetu wengine tuliopata nao uhuru wakati mmoja sasa wana treni za kasi zinazotumia umeme, sisi hata reli aliyotuachia mkoloni inatushinda kuiendesha. Wakati wenzetu wana mashirika yao imara ya ndege ambayo ni alama ya taifa, sisi ATCL yetu iko taabani.
Kwa ufupi, tumepotea na tunahitaji kuitafuta njia aliyotuonyesha Nyerere. Kwa bahati mbaya CCM ya sasa haiwezi kuturejesha kwenye njia sahihi kwa sababu haina viongozi wenye
vision japo ya miaka 50 au zaidi.
Ndiyo maana nasisitiza; Mtanzania yeyote mwerevu na mwona mbali
(visionary) ataona kwamba rais tunayemhitaji na anayeifaa Tanzania yetu, ni yule anayetu....."alie na maono ya kuifanya Tanzania ijitegemee kwa kutumia rasilimali zetu tulizopendelewa na Mungu na sio anaetaka kutufanya wote tukahemee vibaba, badala ya kufanya kazi"'
Source: Raia Mwema