Mabinti wawili,mtu na dada yake walikwenda kutembea kijijini kwao pamoja na wazazi wao. Baada ya kuwasili kijijini pale waliamua kwenda kusalimu ndugu, jamaa na marafiki ambao walikua hawajawaona muda mrefu sana. Walianza safari ya kwenda kwa mama mmoja ambae alimlea dada mkubwa alipokua mdogo kabla wazazi wao hawajahamia mjini kutafuta maisha. Barabara ilikua imebadilika kidogo hivyo dada mkubwa alimuongoza njia mdogo wake huku akijitahidi kukumbuka nyumbani kwa mlezi wake wa siku nyingi.
Baada ya kutembea mwendo kidogo wakiongozwa na kumbukumbu za utotoni hatimae walifika nyumbani kwa mama mlezi. Nje ya nyumba alikuwapo kijana mmoja mwenye umri kama miaka ishirini hivi kwa kukadiria. Mama mlezi aliyekua ndani alimuagiza akachote maji kwenye simtank iliokuwepo nje. Ndipo alipokutana na mabinti wale wawili waliokua wamewasili wakimsubiri mama atoke nje. Kijana yule aliwasalimu “shkamoo dada” nao wakaitikia “marhaba, hujambo? Katika hali isiyo ya kawaida kijana yule alijibu kwa kusalimia tena na baada ya kujibiwa alisalimia tena kwa mara ya tatu. Kisha, akabeba ndoo yake na kwenda kukinga maji kama alivyoagizwa.
Mabinti wale walimtazama yule kijana huku wakitafakari na kujadili atakua na shida gani. Wakati akisubiri ndoo yake ijae maji yaliyokuwa yakitoka kidogo kwenye bomba, kijana alionekana akiongea mwenyewe bila sauti kusikika huku akitembea kwenda kushoto na kurudi kulia mara kadhaa. Sehemu alizokanyaga wakati akitembea zilikua ni zilezile. Baada ya ndoo yake kujaa, aliibeba, akamuita mama yake nje na kumkabidhi .
Mama alifurahi sana alipowaona mabinti zake baada ya kitambo kirefu. Akamuagiza kijana alete vigoda ili waweze kuketi na kuongea. Baada ya kukaribisha wageni kijana alijitenga pembeni na kuketi peke yake. Mama aliulizia mambo mbalimbali kuhusu mjini. Pia alielezea changamoto mbalimbali wanazopitia ikiwemo baridi kali na ukosefu wa blanketi za kujifunikia hasa nyakati za usiku hivyo akaeleza jinsi yeye na wazee wengine wengi hapo kijijini wanavyosumbuliwa na kifua na maumivu ya mifupa kutokana na baridi kali; hali inayochangiwa na ukosefu wa fedha za kununua zana za kujikinga na baridi.
Mabinti wale wawili wakaulizia kuhusu yule kijana. Mama akaeleza kuwa kijana alizaliwa na ulemavu wa akili. Akasema, “Mimi nilimchukua na kuanza kuishi nae kama mtoto wangu baada ya kuona alikua anaishi katika mazingira magumu sana nyumbani kwao. Niliwaomba wazazi wake nimchukue wakaridhia.” Mama alielezea kwa uchungu. “Huwa anaongea mwenyewe mara nyingine hata anapokua bafuni akioga lakini ni kijana mchapakazi sana”. Ukiacha hizi changamoto ni mtu ambaye ukimuelekeza taratibu na kwa upendo anaelewa kazi za mikono vizuri.
“ Nilipomchukua angali bado mdogo nilimpeleka shule. Alipenda sana kwenda shule kwasababu alitaka kuwa kama watoto wengine wa rika lake. Alipofika darasa la saba alikua bado hawezi kusoma wala kuandika. Siku ya mtihani wa taifa wa darasa la saba aliwahi kurudi nyumbani nikamuuliza kulikoni akasema amefukuzwa kwenye chumba cha mtihani. Baada ya safari ya miaka saba yenye changamoto nyingi hakurusiwa kufanya mtihani wa taifa.”
Baada ya hapo mama alianza kumfundisha kazi za mikono. Mama alielewa kijana wake anaelewa zaidi akifundishwa kwa vitendo. Alianza kumtafutia vibarua majumbani kwa watu ili aweze kutengeneza kipato kama vijana wengine na aanze kujitegemea. Kijana alianza kufanya vibarua vya kusafisha nyumba za watu na kukata kuni. Watu walijua kijana hawezi kusoma,kuandika wala kuhesabu pesa hivyo walimpa kazi ngumu na malipo kidogo sana. Alikata magogo makubwa na kuambulia shilingi elfu mbili tu kwa kutwa nzima. Walezi wake walipopata hizi taarifa walisikitika sana lakini kijana alifurahi alipoona angalau ameanza kutengeneza kipato chake yeye mwenyewe. Walezi wake walimfundisha kutunza pesa kwa ajili ya matumizi ya baadae.
Mama aliendelea kueleza jinsi kijana wake anavyopenda kusali bila kukosa ibada ya kila jumapili. “Kwa kawaida anapenda avae vizuri apendeze mara nyingi huvaa suti. Katika mapato yake ya wiki nzima atachukua sio chini ya shilingi elfu tano na kwenda kuitoa kama sadaka kanisani. Anaamini Mungu ataipokea sadaka yake na kumsaidia kufanikisha malengo alionayo”.
Mara nyingi alipokua anatoka kanisani alikua anakutana na wadada warembo nao walimuomba awanunulie soda na vitafunwa. Tena walimuuliza, “utaweza kweli?” na kijana huyu kuonesha kwamba anaweza aliwapeleka sehemu yenye mgahawa na kuwanunulia wote vinywaji na vitafunwa kadri ya uwezo wake. Hivyo alirudi nyumbani akiwa amemaliza kipato chake chote akiamini ni jambo jema kusaidia watu wengine.
Baada ya muda alitokea mzee mmoja aliekua anamfahamu yule kijana pamoja na walezi wake. Akamtembelea yule mama na kumtaarifu kuwa alimuona kijana wake akinunulia wasichana warembo chai na vitafunwa na mara nyingine akitoa ofa ya kuwalipia watu vinywaji bar. Ndipo walezi wake walipojua mapato ya yule kijana yanaishia wapi. Wakamuita na kumuelewesha kuwa anachofanya si sahihi. Baada ya hapo, mama alianza kukadiria muda atakaochukua kumaliza kazi atakayopewa na kumuwekea muda wa kurudi nyumbani. Pia alimwambia kijana ampe mapato yake ili amsaidie kuhifadhi.
Mabinti wale wawili walimfuata kijana na kumuuliza ana malengo gani katika maisha nae akajibu “Nakusanya hela ili nijenge angalau chumba kimoja,nioe mke na mimi niwe baba mwenye familia kama wanaume wengine.”
Wale mabinti walimuaga kijana na mama yake mlezi na kuanza safari ya kurudi nyumbani kwao. Njiani waliendelea kujadili kuhusu watu wanaozaliwa na ulemavu wa akili na changamoto wanazopitia.
Je ,wazazi wanatambua mapema watoto wao wenye mahitaji maalumu? Jamii inawahudumiaje watu wasiojiweza? Mifumo ya elimu inawasaidiaje wanafunzi wanaopenda kujifunza lakini wanashindwa kuelewa kusoma na kuandika kutokana na ulemavu wa akili? Serikali inawawezeshaje wazazi wenye watoto wenye ulemavu wa akili hasa wazazi wenye kipato cha chini?
Baadhi ya watoto wenye ulemavu wa akili huhitaji usimamizi wa karibu wa mara kwa mara kutoka kwa madaktari wazoefu wa ulemavu wa akili. Huduma hizi zimekua zenye gharama kubwa kutokana na uchache wa wataalamu hawa na ugumu wa huduma zinazotolewa kwa wagonjwa. Wagonjwa wengine huhitaji kumeza dawa ambazo zinauzwa kwa bei ya juu sana. Serikali ina mtazamo gani kuhusu hili swala?
Wazazi wengine hulazimika kuwaficha ndani watoto wao wenye mahitaji maalumu wakiogopa mtoto kupotea na dhana potofu katika jamii husika, “Amemtoa kafara mtoto wake ili apate mali nyingi, hiyo ni laana, alikosea masharti”.
Je mtoto mwenye ulemavu wa akili anaposahau njia ya kurudi nyumbani anakoishi jamii hutoa msaada gani wa kumfikisha salama kwa wazazi wake?
Kutokana na changamoto nyingi zinazotokea anapozaliwa mtoto mwenye ulemavu wa akili, watoto hawa wamekuwa wakichukuliwa kama mizigo. Je, mimi na wewe tunasaidiaje kuboresha maisha yao?

Upvote
2