SoC04 Typhoid, ugonjwa unaouzwa kama nyanya na hospital binafsi

SoC04 Typhoid, ugonjwa unaouzwa kama nyanya na hospital binafsi

Tanzania Tuitakayo competition threads

Rambau manite

New Member
Joined
Jun 10, 2024
Posts
1
Reaction score
2
" Daktari, Mimi Typhoid yangu naijua nikihisi tu naenda kununua dawa nakunywa na napona vizuri tu" Sentensi hii madaktari tumekua tukikutana nayo mara Kwa mara pindi tuwaonapo wagonjwa wengi huku mitaani.

Cha kusikitisha zaidi Ugonjwa huu umekuwa ukitumika kujiingizia faida Kwa hospital binafsi bila hata kuwa na chembe ya huruma Kwa wagonjwa Hawa.

Je homa ya Typhoid ni nini na vipimo vyake sahihi ni vipi??

Homa ya Typhoid ni ugonjwa hasahasa wa mfumo wa chakula unaosababishwa na bakteria ajulikanae kama Salmonella typhi Kwa lugha ya kilatini, mdudu huyu hushambulia mfumo wa chakula wa mwanadamu sanasana sehemu za seli za utumbo mdogo zinazofanya kazi ya ufyonzaji wa chakula kutoka kwenye utumbo mdogo kisha kukiingiza kwenye mfumo wa mzunguko wa damu Kwa ajili ya matumizi mbalimbali mwilini.Vijidudu hivi huapatikana sana kwenye mazingira yenye vyakula na majibu ambayo hayajaandaliwa kwa usafi stahiki.

Dalili kuu za ugonjwa huu ni kama zifuatazo;

1. Homa Kali
Ugonjwa huu huanza na dalili kuu ya homa Kali sana yenye muundo wa ngazi, Homa hii hutambulika Kwa Jina Hilo kutokana na joto la mwili kua linapanda kila uchwao huku likiongezeka siku baada ya siku, kwa mfano mgonjwa huyu akiwa anapimwa joto lake kila siku litakua tofauti yaani mfano Leo ni nyuzi joto 39 basi kesho litakua 40 na kuendelea.

2. Maumivu ya kichwa
Ugonjwa huu pia huambatana na maumivu makali ya kichwa ambapo inakadiriwa zaidi ya asilimia 80 ya watu wenye changamoto hii ya Typhoid wanapata maumivu makali ya kichwa, Kwa lugha rahisi katika kila watu 10 watakaothibitika kuwa na changamoto hii watu 8 kati yao watakua na maumivu ya kichwa pia.

3. Kupitisha choo cha kijani
Ikumbukwe kwamba njia ya chakula pia hupitisha nyongo, kitaalamu nyongo ni kemikali inayotengenezwa na kuhifadhiwa kwenye ini, Nyongo Ina kazi nyingi tofauti tofauti ikiwemo kurahisisha mmeng'enyo wa chakula hasahasa vyakula vya mafuta na pia husaidia ufyonzaji wa vitamini mbalimbali mwilini. Baada ya nyongo kutumika huwa inafyonzwa pia kurudishwa kwenye mfumo wa ini, kutokana vijidudu vya ugonjwa huu kushambulia ufyonzaji kwenye utumbo mdogo hii pia hupelekea nyongo kushindwa kunyonywa vizuri kwenye utumbo mdogo na hatimaye kukipa choo rangi hiyo ya kijani Kwa kitaalamu choo hicho utambulika Kwa Jina la "Pea soup Diarrhea".

4. Mwisho kabisa dalili nyingine ambatanishi kama za tumbo kuunguruma kutokana na ufyonzaji wa chakula kuwa duni na ulimi kuwa na rangi tofauti na Ile ya kawaida na kutokwa na vipele mithili ya damu iliyogandiana kwenye sehemu za kifua na tumbo, vipele hivyo ambavyo kitaalamu hujulikana kama "Rose spots" ni Moja ya viashiria vikubwa Kwa mtu mwenye changamoto hii ya homa ya Typhoid.

JE NI VIPIMO VIPI VYA TYPHOID HUFANYIKA ??

Vipimo vya homa hii ya Typhoid vipo vingi lakini tunaweza kuvigawa kwenye makundi mawili, kwanza ni vile vinavyofanyika Kwa njia ya Damu na vingine ni Kwa njia ya Choo kama ifuatavyo;

Vipimo vya njia ya Damu,

1. Widal test
Kipimo hiki ndicho kinachofanyika sana mitaani kwetu. Sababu kubwa ya baadhi ya sehemu hasahasa hospital BINAFSI na maabara za mtaani kutumia kipimo hiki ni Kwa sababu wagonjwa wengi huwa wanapenda kupata majibu ya vipimo vyao Kwa uharaka na kipimo hiki pia ukilinganisha na vipimo vingine huchukua muda mfupi zaidi hivyo kupelekea wagonjwa wengi kupata majibu ya vipimo vyao Kwa uharaka mkubwa kitu ambacho hupelekea wagonjwa wengi kumiminka mahala kwenye Kipimo hiki na kuwaingizia faida kubwa wapimaji, lakini kipimo hiki sio kizuri hata kidogo Kwa sababu nyingi mojawapo ikiwa ni kuwa kipimo hiki hakiwi chanya Kwa Typhoid peke ake Bali Kwa changamoto nyingi ikiwemo Malaria na ugonjwa wa Brucella hivyo majibu yake yanaweza kuwa na ukakasi mkubwa na kumpelekea Daktari kutoa matibabu ambayo sio sahihi.

2.Blood Culture
Kipimo hiki ni sahihi zaidi na kinachopendekezwa na wizara ya Afya pamoja na shirika la Afya duniani yaani WHO , kinahusisha kuotesha wadudu Hawa wa bakteria Kwa njia ya Damu Kwa muda wa siku 3 paka 5 maabara, ni kipimo kizuri na sahihi Kwa ugonjwa huu wa Typhoid Kwa sababu kinakua chanya Toka siku ya kwanza dalili za ugonjwa huu zinapoanza kujionesha na pia kinaonesha dawa Gani nzuri itafaa kutumika Kwa ajili ya mdudu huyo.

Vipimo vya Choo,

1. Stool Culture
Hiki ni kipimo kizuri pia Kwa ajili ya ugonjwa huu wa Typhoid ambapo choo huchukuliwa Toka Kwa mgonjwa na kisha kupelekea maabara ambapo vijidudu sababishi vya ugonjwa huu huoteshwa Kwa kutumia vifaa maalumu ndani ya maabara na huchukua siku tatu paka Tano kupata majibu isipokuwa tofauti na kile kipimo cha kuotesha damu ambacho kinakua chanya Toka siku ya kwanza kipimo hiki chenyewe kinakua chanya kuanzia siku tatu baada ya dalili za awali kuanza kujionesha.

MAPENDEKEZO

1. Hospitali BINAFSI na vituo vya maabara vya mtaani vizingatie Afya za watu Kwa kufanya vipimo sahihi na vinavyopendekezwa na wizara ya Afya.

2. Watu wacheki Afya zao kabla ya kuanza kutumia dawa ili kuepusha usugu wa dawa za antibayotiki kitu ambacho kinaiingizia serikali hasara kubwa kila mwaka na pia mgonjwa mwenyewe kupata hasara Kwa kutumia dawa ambazo ni gharama sana kulinganisha na zile ambazo ni rahisi kupata usugu

3. Sio kila homa ni Typhoid na sio kila kuunguruma ama kuumwa na tumbo ni Typhoid, fika hospital onana na Daktari akuchukue historia Yako vizuri ili upate matibabu sahihi.

4. Watoa huduma za Afya watoe elimu sahihi Kwa wagonjwa wao dhidi ya ugonjwa huu na namna Bora ya kuufanyia vipimo.

Ni Mimi mwandishi wako Michael Rambau.
 
Upvote 1
Back
Top Bottom