SoC02 Ua la faraja: Tafakuri ya athari za ukoloni Mambosasa

SoC02 Ua la faraja: Tafakuri ya athari za ukoloni Mambosasa

Stories of Change - 2022 Competition

Mwanakapaya

New Member
Joined
Oct 3, 2021
Posts
2
Reaction score
1
Ua la Faraja riwaya iliyoandikwa na William.E. Mkufya mwaka 2001. Katika makala haya najadili kwa ufupi jambo moja tu linalojitokeza zaidi kuanzia kurasa wa 356 mpaka 364.

Kusudi la makala haya ni kubainisha namna ukoloni mambosasa unavyoziathiri nchi za Kiafrika ikiwamo Tanzania na kujaribu kupendekeza njia mwafaka za kukabiliana na changamoto hizo.

Rais wa kwanza wa Ghana, hayati Kwame Nkrumah (1965) katika kitabu chake maarufu kiitwacho Neo-Colonialism, the Last Stage of imperialism alieleza kwamba ukoloni mambosasa ni hatua ya mwisho ya ubeberu (sera ya kupanua nguvu na ushawishi wa nchi kwa kutumia ukoloni, jeshi au mbinu zingine) ambayo ni hatari zaidi kuliko hatua zingine.

Kwa Nkrumah, nchi nyingi zinazoendelea hususan za Kiafrika, ikiwemo Tanzania zina uhuru dhahania.Ni uhuru unaotambulika kimataifa lakini kiuhalisia uhuru huo ni wa kupeperusha bendela pekee. Mifumo ya kiutamaduni, kiuchumi na kisiasa inadhibitiwa kutoka nje.

Mataifa yanayodaiwa kuiendesha mifumo hii ni pamoja na Marekani, Ufaransa, Uingereza, Ujerumani na hivi sasa China. Uendeshwaji huo unawezeshwa na taasisi ambazo ni wakala wa ukoloni mambo sasa. Taasisi hizo ni pamoja na Benki ya dunia, Umoja wa mataifa, taasisi ya fedha ya kimataifa, shirika la biashara duniani pamoja na serikali za mataifa makubwa duniani.

Taasisi hizi hushinikiza utekelezwaji wa agenda mbalimbali katika mataifa.

Afrika imeathirika na ukoloni mambosasa katika mambo mbalimbali kama ifuatavyo:

Mosi, Waafrika wametelekeza mila na desturi zao. Mwandishi analieleza hili kwa kumtumia mhusika wake Dkt Hans anapomwambia Omolo kwaba “Msahau kwao ni mtumwa … Waafrika sasa wamekuwa watumwa wa mila na tamaduni za wenzao, kuanzia imani hadi uchumi na siasa.

Mwafrika akitaka kufanya jambo sharti ajipime kwanza kwa Mzungu au Mwaarabu”. Hapa tunaona athari za ukoloni mambosasa ambapo jamii imeathirika kiasi kwamba imetupilia mbali mila na desturi zake.

Hivi sasa, Waafrika wanafanya mambo yao kwa kuiga wafanyavyo wazungu au Waarabu. Mathalani jando na unyago ni mila na desturi ambazo zilifundisha vijana mabadiliko ya miili yao na namna ya kukabiliana na mihemko ya kimwili. Aidha, jando na unyango lilikuwa ni darasa bora zaidi la ndoa kuliko “kitchen Party” na “Send Off”. Kufifia kwa mila na desturi hizo kumefanya vijana kuanza ngono pasi kuwa na maarifa ya kutosha.

Pili, Waafrika wanaingiza kila kitu nchini kutoka ughaibuni. Suala la kuiga kila kitu kutoka kwa Wazungu au Waarabu na kukifanya kama kilivyo pasi kuhawilisha na mazingira halisi ni matokeo ya ukoloni mambosasa ambapo Waafrika wamefanywa kasuku wa Wazungu.

Mwandishi anaona kuwa kuiga si dhambi lakini ni muhimu kuchagua cha kuiga. Katika hili serikali za nchi za Kiafrika zinapewa wito wa kuacha kuiga na kufanya yale ambayo wanaambiwa kufanya na mataifa ya ughaibuni.

Dkt. Hans anasema: “Serikali zetu zina wapumbavu wanaoshabikia kila kinachosemwa na Mzungu. Tukiletewa chanjo na kulazimishwa tuchanje watoto wetu, hatukai chini kwanza na kuchunguza usafi na ubora wa hizo chanjo.

Ni raisi kwa mtu mwovu huko Ulaya kuingiza kitu kibaya cha kuteketeza vizazi vya baadaye” Hapa mwandishi kupitia mhusika wake Dkt. Hans anaiasa serikali na jamii kwa ujumla kuwa makini hasa inapoingiza dawa,vyakula au bidhaa yoyote toka ughaibuni kwani wakati mwingine huwa na madhara.

Hivi karibuni kuliibuka mzozo juu ya chanjo ya UVIKO ambapo wapo baadhi ya Watanzania walionesha hofu juu ya usalama wa chanjo hizo.

Hii inatokana na hofu hii ya kasumba ya kuiga na kuchukua kila kitu toka kwa Wazungu pasi ya kufanya uchunguzi wa kutosha. Tunatahadharishwa kutowaamini wazungu kwa asilimia mia badala yake tusaili kila tunachoambiwa na kupewa.

Tatu, Waafrika wamekumbwa na tatizo la mmomonyoko wa maadili. Ukoloni mambosasa umesababisha Waafrika wachangamane na jamii ya kimataifa na kwamba wanajikuta wakiiga tabia zisizo adilifu.

Mwandishi anaonya kuwa Afrika isiwe jalala la upuuzi wa Ulaya. Vijana wanajikuta wakifanya kama wafanyavyo watu wa mataifa ya Ulaya na Marekani.

Tabia za matumizi ya madawa ya kulevya, ugaidi, kuvaa nusu uchi, kurekodi video za ngono na kupiga picha za uchi na kisha kuweka mtandaoni ni baadhi tu ya mambo yanayomomonyoa maadili ya Kiafrika.

Aidha, mwandishi anaikumbusha jamii kudumisha maadili yake na si kuziachia taasisi za kidini pekee ambazo kwa mujibu wake hazitoshi kujenga maadili ya Mwafrika.

Mwandishi anasema: “Ukristo na Uisilamu hauna maandalizi yanayoweza kumkamilisha Mwafrika kama hauheshimu asili na mila ya Mwafrika”. Mwandishi anasema: “Ukristo na Uisilamu hauna maandalizi yanayoweza kumkamilisha Mwafrika kama hauheshimu asili na mila ya Mwafrika”.

Mwandishi anamtaka kila mtu kuijua asili yake na kuenzi maadili ya jamii yake. Tunaona Omolo anapomuuliza Dkt. Hans kuwa amejuaje masuala ya historia ilhali ni daktari anajibiwa hivi: “Historia ya mtu siyo somo la darasani ambalo una hiari ya kuliacha na kuchagua kusoma kitu kingine. Ni wajibu wa kila mtoto kujijua asili yake na historia ya pale alipo sasa.”

Hapa jamii inaaswa kujibidisha kuijua historia yake na kuenzi asili yake ikiwemo maadili ya jamii. Tunatakiwa kuachana na kasumba ya kuishi kama Wazungu wakati sisi ni Waafrika. Tuige mambo yasiyokinzana na maadili na si kila kitu.

Nne, Waafrika wamepoteza utu na asili yao. Mwandishi anabainisha kuwa “mataifa yote ya Kiafrika yameundwa katika mipaka ya watawala wao wa kizungu.

Mataifa yao ya asili yalivurugwa, yakawekwa katika mipaka mipya ambayo yaliweza kutawalika. Walivurugiwa uchumi wao, mila zao, tawala zao, imani zao … kwa kifupi, wazungu waliuua utu wao na kuunda utu mpya wa Mwafrika. Utu usio Uzungu wala Uarabu wala Uafrika… watu walipodai uhuru kwa heri na shari walifanikiwa kuupata lakini ulikuwa uhuru wa watu guni”.

Hapa mwandishi anabainisha namna ambavyo mataifa ya Kiafrika yalijikuta chini ya minyororo ya ukoloni mambosasa.

Watu wake wamejikuta hawana utu na asili yao kutokana na kuingiliwa na Wazungu na Waarabu hali inayofanya kuwa watumwa wa kifikra. Hali hii inachelewesha maendeleo ya nchi zetu kwa ujumla.

Dkt. Hans anahoji: “Hebu fikiria taifa la watu lisilo na uasili, mila, imani, falsafa, uzalendo wala mwelekeo kisha wako ‘huru’ katika ulimwengu ulioelemewa na nguvu za wale waliowavuruga !” Hii inadokeza kuwa nchi za Kiafrika ikiwemo Tanzania, kutokana na mfumo wa ukoloni mambosasa hazina mwelekeo na zinaendeshwa na mataifa yenye nguvu duniani, mataifa ambayo ndiyo yalizifanya kukosa mwelekeo. Hii ni hatari katika ustawi wa mataifa haya.

Kwa kuhitimisha, tunaona ipo haja serikali kuboresha sera zake ili kuhakikisha tunafufua utu na asili yetu kwa kujenga taifa lenye mila, imani, falsafa, uzalendo na mwelekeo wake thabiti.

Ndimi,
Mwanagenzi
Mawasiliano: manyukakapaya@gmail.com
 
Upvote 0
Back
Top Bottom