Uchaguzi huu si huru hata kidogo
08.10.2008 0140 EAT
Mgombea ubunge CHADEMA afunguliwa mashitaka
*Wamo pia mgombea udiwani, Mnyika
*CCM yapongeza mkong'oto wa Polisi
Na George John, Tarime
Majira
JESHI la Polisi mkoani Mara limewafunguliwa mashitaka matatu watu 29 wakiwamo akiwamo mgombea ubunge wa CHADEMA jimbo la Tarime, Bw. Charles Mwera.
na wagombea ubunge na udiwani wa chama cha demkrasia na maendeleo CHADEMA ambao juzi jioni walitiwa mbaroni kuwekwa mahabusu kwa saa zaidi ya nne katika kituo kikuu cha polisi mjini Tarime.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara, Bw. Liberatus Barlow, aliwaambia waandishi wa habari mjini hapa jana, kuwa polisi walikata watu 29 juzi saa 1.15 usiku wakati wakitoka kwenye mkutano wa kampeni katika kitongoji cha Buhemba nje kidogo ya mji wa Tarime.
Alisema watuhumiwa hao wamefunguliwa kesi tatu za kufanya mkutano kinyume cha sheria, kufanya maandamano haramu na kuharibu mali, mashitaka ambayo polisi wanadai hivi sasa yanachunguzwa.
Kwa mujibu wa Kamanda Barlow maandamano hayo yalilenga kuharibu mali mbalimbali za wananchi wa Tarime vikiwamo vituo vya mafuta vya mjini hapa.
Miongoni mwa viongozi walioonja nguvu hiyo ya Kamanda Venance Tossi ni Mwenyekiti wa Taifa wa Vijana, Bw. John Mnyika, mgombea ubunge ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri Tarime, Bw. Mwera, mgombea udiwani kata ya Tarime Mjini, Bw. John Heche na mjumbe wa Halmashauri Kuu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama hicho mkoa wa Iringa, Dkt. Kigwitu Kapwani.
Wengine waliotiwa mbaroni katika kamatakamata hiyo ya Polisi ni Bw. Werema Mwita, Katibu Mwenezi wa Wilaya, Bw. Babu Range, Mkurugenzi Msaidizi wa Vijana na Bw. Alex Chacha, Meneja wa Kampeni za ubunge na udiwani na wanawake na watoto wenye umri wa chini ya miaka 16.
Alisema katika vurugu hizo, viongozi na wafuasi wao walivunja kwa mawe magari matatu yakiwamo mawili ya Polisi aina ya Land Rover namba TP0901 na TP1509 na basi la kiraia aina ya Scania namba T548AGN ambalo lilivunjwa kioo cha nyuma.
Kamanda Barlow alisema kutokana na watuhumiwa kukaidi amri ya Polisi, askari walilazimika kutumia nguvu kubwa ikiwa ni pamoja na kurusha mabomu ya machozi na risasi za moto na kufanikisha kuwatia mbaroni wahusika.
Hata hivyo, kutokana na wengine kujeruhiwa, walipewa fomu namba tatu (PF3) na kwenda kupata matibabu hospitali ya wilaya ya Tarime na kwamba wahusika wote wako nje kwa dhamana.
Hata hivyo, kutokana na polisi kurusha ovyo mabomu hayo hata sehemu zisizohusika, ilisababisha wananchi wengi kuchukizwa na kitendo hicho, ambacho kilisababisha baadhi ya wafanyabiashara kupoteza mali zao.
"Polisi hawakuwa na sababu ya kuturushia mabomu wakati hapakuwa na fujo, sasa angalia nimepoteza zaidi ya sh. 150,000 baada ya wateja kukimbia bila kulipa bili zao za vyakula na vinywaji," alidai mtu anayemiliki mgahawa wa Girango mjini hapa.
Naye Richard Mwaikenda, anaripoti kuwa wakati CCM imelipongeza Jeshi la Polisi kwa kutumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya viongozi na wafuasi wa CHADEMA, uongozi wa CHADEMA kwa upande wake, umelaani kitendo hicho na kukiita cha kinyama.
Kwa upande wa CCM, pongezi hizo zilitolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Propaganda wa Chama hicho, Bw. Richard Tambwe, katika mkutano na waandishi wa habari jana kwenye ofisi za CCM Wilaya ya Tarime.
Alisema Jeshi hilo limetimiza wajibu wake kwa kuwaadabisha wafuasi wa CHADEMA, akidai kwamba walikuwa wachokozi kwa kuwapiga mawe askari waliokuwa wanawaamuru kuacha maandamano.
Alisema mara nyingi CHADEMA ndio waanzilishi wa vurugu kwenye mikutano ya CCM na vyama vingine, likiwamo tukio la kumpiga mawe Mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila alipohutubia kwenye viwanja vya Sabasaba.
Alizidi kuilaumu CHADEMA kuwa wafuasi wake wanaendeleza vurugu dhidi ya CCM kwa kuchoma na kumvisha mbwa sare za CCM.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, mjini Tarime jana, Mkurugenzi wa Vijana wa CHADEMA, Bw. John Mnyika, alilaani kitendo cha Jeshi hilo kutumia nguvu kwa kuwapiga mabomu ya machozi bila makosa wananchi na wafuasi wao.
Alisema kutokana na kitendo hicho alichokiita cha kinyama dhidi ya raia, jeshi hilo linatakiwa liombe radhi, kwani ni aibu kwao na kwa wananchi.
Pia Bw. Mnyika alikemea tabia ya askari, kuwakamata na kuwapiga viongozi na wagombea wa chama hicho na kuwapekua mifukoni na hatimaye kuwaibia fedha zao zikiwamo sh. 240, 000 za Mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Iringa, Dkt. Kapwani.
Alimtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, Inspekta Jenerali Said Mwema kumkamata Kamanda aliyemtaja kwa
jina la Lyamba aliyedai aliendesha operesheni hiyo.
Katika sakata hilo, wafuasi wapatao 25 na viongozi kadhaa wakiwamo mgombea ubunge, Bw. Charles Mwera na mgombea udiwani, Bw. John Heche, kukamatwa, kupigwa na kuswekwa mahabusu kuanzia saa moja hadi saa 7 usiku walipoachiwa baada ya kuandikisha maelezo.
"Nashangaa polisi wanasema tulikamatwa kwa kosa la kuandamana bila kibali, hivi walitaka tutumie utaratibu gani wa kuondoka kwenye mkutano huo, kwani sisi tulijipanga viongozi na wagombea tukiwa kwenye magari manne, huku tukisindikizwa na baadhi ya wananchi waliokuwa wanatembea kwa miguu kwenda majumbani mwao," alihoji Bw. Mnyika.
Bw. Mnyika aliziomba Taasisi za kutetea haki za binadamu za kitaifa na kimataifa, kulaani na kukemea kitendo hicho alichokiita cha kinyama.