SoC01 Ubunifu ndiyo Brand/Chapa yako ya Kukufanikisha

SoC01 Ubunifu ndiyo Brand/Chapa yako ya Kukufanikisha

Stories of Change - 2021 Competition

Filosofia ya Rorya

JF-Expert Member
Joined
Sep 20, 2021
Posts
3,211
Reaction score
3,611
Nyanja: Maendeleo ya Jamii.

Utangulizi.
Katika dunia ya leo ya ushindani mkubwa katika kila jambo, dhana ya ubunifu imedhihiri kuchukuwa nafasi kubwa sana katika kutafuta faida na manufaa ya shughuli za kila siku za maisha ya mwanadamu. Aidha, ubunifu ni kipawa cha akili ambacho kila mmoja wetu amezaliwa nacho isipokuwa tunatofautiana tu viwango vya maamuzi ya kuamsha na kuchochea kipawa cha ubunifu. Ubunifu tunaofundishwa vyuoni na mashuleni ni ziada tu ambayo hiyo hutegemea kwa kiwango kikubwa ubunifu wa kuzaliwa umekaaje. Ili kufanya ubunifu, yafuatayo ni miongoni mwa vigezo muhimu vya msingi na ambavyo vina gharama kubwa kuvikwepa:-

Tathmini uwezo wa akili yako kwanza.
Heri upofu wa macho kuliko upofu wa akili, maana macho hayana uwezo wa kufasiri yanayoona. Binadamu bila akili timamu thamani yake inapungua, vivyo hivyo binadamu mwenye akili timamu inayofanya maovu ya makusudi (ya kudhamiria) akili yake inaweza kufananishwa na silika ya hayawani, maana huenda kukutana na simba mwenye njaa kunaweza kukubakisha salama kuliko kuishi na binadamu huyu.

Fanya mapinduzi ndani yako.
Roho ya ubunifu huasisiwa na mapinduzi ndani ya mtu kwanza ambayo baadaye yanafasiriwa nje ya mtu. Mapinduzi haya huchochewa na kiu ya kutaka mabadiliko ambayo yanapatikana nje ya utaratibu wa kawaida uliozoeleka (yaani yanapatikana kwa ubunifu wa utaratibu mpya kabisa, ambao huu wakati fulani unaweza kuzua hofu ya kupingwa utaratibu mpya, maana binadamu kwa asili ya uumbaji wake hapokei mabadiliko kwa amani). Kamwe usiruhusu dhamira, fursa na uwezo vikakutoka. Mwanafalsafa-mfizikia Albert Einstein (Myahudi aliyezaliwa Ujerumani) alisema “We cannot solve our problems with the same thinking we used when we created them”
“Hatuwezi kutatua matatizo yetu kwa fikra zilezile tulizotumia tulipoyasababisha”
tafsiri isiyo rasmi.

Einstein anatufundisha kubadili jinsi ya kufikiri kwetu ili kutatua matatizo. Katika ubunifu, jizoeshe kubuni vikubwa alafu vitekeleze hatua kwa hatua “As long as you’re going to be thinking anyway, think big Donald John Trump (2008)”
Maadamu unaenda kufikiria hata hivyo, fikiria makubwa Donald JohnTrump (2008)
tafsiri isiyo rasmi.

Buni mbinu zinazozaa matokeo yanayopimika kisayansi.
Watu wabunifu wanajipambanua kwa uwezo wa kuonyesha utofauti katika fikra, matendo na kauli zao, aidha, ni watu waliojizolea sifa nyingi na kukubalika sana kwa sababu wanawapa watu ladha ya tofauti kabisa licha ya kwamba ubunifu wao pia unasaidia kuwakwamua watu toka katika mikwamo. Ubunifu ni ishara ya mtu kuwa imara (active) na kinyume chake ni kweli. Wabunifu mahiri huwa wanaota ndoto za kupata matokeo yanayopimika kisayansi, hivyo wanakuwa na uhakika wa mbinu wanazotekeleza kungali mapema kabla ya kufikia hatua ya kupima matokeo. Kutokuwa mbunifu katika dhamana yako kwa mambo yenye maslahi na mustakabali wako na wa wanaokuzunguka ni hatari sana kwa sababu unazorotesha na kuchelewesha haki & maendeleo. Wasokuwa wabunifu katika dhamana zao ni maadui wa maendeleo yao wenyewe na ya wanaowazunguka.

Kubali tatizo linalohitaji ubunifu wa ufumbuzi wake.
Kama hujakubali tatizo basi huna tatizo unalolitafutia ufumbuzi. Kukubali tatizo siyo ishara ya kushindwa bali ishara ya ujasiri. Mojawapo ya mbinu za kukubali tatizo ni kukaa katika utulivu kwanza. Utulivu huleta fursa ya tafakari makini, pana na ya kina ya namna ya kubuni mikakati maridhawa ya kutoa majibu sahihi kwa tatizo husika. Aidha, shinda hofu kwa kuona majibu ya tatizo kabla hujayapata majibu hayo, hapa ndipo wengi wamefeli, ukiona majibu mapema inakutia moyo kusonga mbele kwa ari. Mhe. Rais Franklin Delano Roosevelt wa Amerika almaarufu kama FDR, picha/taswira ya Amerika ya leo inayomiliki asilima 14 ya pato la dunia nzima ikiwa na pato la takriban dola za Marekani 30 tr kwa mwaka; aliiona mwaka 1933 alipokuwa akitengeneza Dira (mpango mkakati wa kufufua uchumi kufuatia anguko la uchumi “Great Depression 1929-1939”), katika hotuba yake ya kuapishwa kuwa rais wa 32 alisema “the only thing we have to fear is fear itself” “kitu pekee tunachohitaji kuhofia ni hofu yenyewe” Rais FDR aligundua ukubwa wa tatizo la ajira lililofikia kati ya asilimia 80 & 90 katika baadhi ya majimbo na hivyo watu 15 ml wakakosa ajira baada ya baadhi ya mitaji iliyowekezwa kufilisika, watu wakawa wanatoa amana zao kwa kasi kubwa, ndipo akatangaza likizo-ya-kibenki ya siku 4 ili watu washindwe kuhamisha amana zao toka mabenki, Baraza la Congress likapitisha sheria ya Roosevelt ya dharura ya kibenki (Roosevelt Emergency Banking Act); ambayo ilisanifu upya mabenki na kufunga zile ambazo zilifilisika, siku tatu baadaye FDR akawaomba Wamarekani kurudisha amana zao benki ambapo hadi mwisho wa mwezi huo takriban robo tatu ya mabenki yalirudi sokoni. Huu ni mkakati mojawapo kati ya mingi aliyotekeleza kufufua uchumi wa Amerika zikiwemo kilimo, viwanda & biashara. FDR alianza kwa kukubali tatizo.

Funguka kwa watu tofauti.
Unapofungua chaneli za mawasiliano na watu unatengeneza mtandao utaokuunganisha na watu wa kaliba mbalimbali, ragba tofauti na tajiriba zinazohitajika kukuongoza kudhihirisha uwezo wako wa ubunifu wa ufumbuzi wa matatizo yanayokukabili. Epuka kujitengenezea gereza lako kwa sababu unapotengeneza mtandao na watu mnabadilishana mawazo kwa sababu binadamu tumeumbwa kwa uwezo tofauti kila mmoja, hivyo epuka kuhalifu mawazo yako mwenyewe, epuka kuwa hakimu wa kujihukumu makosa yako mwenyewe, epuka kuwa shahidi wa kesi yako mwenyewe, epuka kuwa mwendesha mashtaka yako mwenyewe. Aidha, pana watu waliokwishapitia uzoefu na changamoto kama ya kwako hivyo yakupasa kujuwa kwamba duniani hakuna mwenye shida ambayo hiyo hajawahi kuwa nayo mtu mwingine sehemu nyingine huko. Ili kujuwa kwamba pana mtu mwingine mwenye shida kama yako itakupasa kujichanganya na watu. Unapoamua kubaki mwenyewe kwenye gereza lako basi ujuwe umejifungia milango ya kupata maarifa mapya na kwamba utabaki kujuwa na kuongea kilekile unachojuwa (huna jipya). “When you talk, you are only repeating what you already know; But when you listen, you may learn something new” Dalai Lama. Kuhani huyu anatufundisha kwamba kuna nguvu kubwa katika kusikiliza kuliko kuongea kwamba faida muhimu ni kujifunza jambo jipya.

Unaposikiliza ina maana unasikiliza toka kwa wengine ambayo hii maana yake ni kwamba unajichanganya na watu, yaani hauko mwenyewe, umejiweka huru toka kwenye gereza lako, maana utasikia jipya toka wapi, toka kwa nani kama hujatafuta kuwa na wenzako? Tanzania na dunia isingejuwa kwamba zile kontena katika bandari ya Dar es Salaam zina makinikia ya thamani iliyovunja rekodi ya zaidi ya Tshs.400 tr kama Mhe. Rais Dkt. Magufuli hasingefunguka na kutafuta wataalam-huru wengine kutafiti na kuthibitisha yale yaliyosemwa na wataalam wa mshahara? Mhe. Rais alikuwa tayari kuwa msikivu kama anavyofundisha Kuhani Dalai Lama kwenye falsafa yake, na usikivu wa rais ukamfundisha mambo mapya ambayo yayo hayo akayatengenezea ubunifu wa namna ya kuyasimamia kwa tija ya taifa, mojawapo ya mambo mapya aliyojifunza rais na dunia nzima ni kwamba ripoti ile ya wataalam huru wa jiolojia iligundua madini na vito ambavyo havikuwahi kujulikana kama vipo Tanzania, labda vilijulikana kwa warasimu tu. Shuleni hatukufundishwa kuwa Tanzania ina madini yale mapya yaliyokuwa kwenye ripoti ile, sababu ya kutofundishwa haya shuleni haijulikani. Ila wageni walijuwa kwa miaka yote tangu wapepelezi wa kikoloni wa Afrika akina John Hanning Speke, Sir Richard Burton, David Livingstone na Henry Morton Stanley, walipokamilisha pamoja na wenzao kutengeneza jiografia ya Afrika (wao wakipangiwa Nile hadi Afrika Mashariki) na rasilimali zake miaka ya baada ya 1870s.

Dhamiria kuacha alama badala ya nadharia.
Binadamu wanaamini alama (vitu vinavyoonekana kwa macho. Actions speak louder than words) kuliko nadharia tu. Tunaishi kwenye kizazi kinachotaka vitendo, hakitaki nadharia, japokuwa vitendo huanza kwenye nadharia kwanza. Kizazi hiki (kwa walio wengi) kinaamini kuwa nadharia ni lugha inayoongeleka na kueleweka kwa warasimu, wanafalsafa, wanataaluma, watengeneza sera na wengine wanaofanana na hao. Kwao wanaelewa lugha ya vitendo halisi tu; lugha inayofasiriwa kwanza kwenye macho yao kabla ya akili zao. Upimaji wa vitendo halisi (alama) ni wa wazi na wa moja kwa moja tofauti na upimaji wa nadharia. Makosa ya kwenye vitendo ni rahisi kubainika kuliko makosa ya kwenye nadharia ambayo huhitaji wakati fulani uwezo wa kifalsafa kuyabaini. Utimilifu wa ahadi hutakiwa kuwa kwenye vitendo na siyo kwenye nadharia, ahadi ikitimia kwenye vitendo hukuza imani ya watu kwa viwango vya juu kuliko ikibaki kukwama kwenye nadharia tu.

Taifa la Tanzania linatarajia mambo makubwa yenye tija kutokea baada ya miradi mikubwa ya kimkakati kukamilika na mtaji uliowekezwa kwazo kurudi maradufu licha ya miradi hii kuvutia uwekezaji wa mitaji mingine mipya (multiplier-effect). Maendeleo makubwa yatokanayo na uwekezaji unaoendelea hivi sasa yatatukia (posthumously) kama vichipukizi vya mitaji hiyo inayowekezwa kwa gharama ya saburi. Kati ya yanayotarajiwa ni pamoja na ukuaji wa masoko ya mitaji, bidhaa na huduma ambavyo navyo vitaboresha mnyororo wa thamani katika uzalishaji mali na utoaji huduma katika sekta zote muhimu kwa uchumi mdogo na mkubwa wa taifa.

Uwekezaji mkubwa katika miradi ya maendeleo popote duniani hutegemea mambo ya msingi kama: nishati nafuu ya umeme au gesi, miundombinu bora ya haraka na nafuu ya usafirishaji, upatikanaji wa maji ya kutosha, huduma za mawasiliano ya haraka na nafuu, mfumo-bora-rafiki wa kodi, amani na utangamano wa nchi, sheria zilizoboreshwa hususan zinazohusiana na uwekezaji, hadhi ya nchi kimataifa (je, imewekewa vikwazo?) nk.

Kwa mikono yangu na akili zangu mwenyewe.

Naomba kura yako.
 
Upvote 3
Back
Top Bottom