Uchafuzi wa Mazingira na ufumbuzi wa tatizo hili

Uchafuzi wa Mazingira na ufumbuzi wa tatizo hili

Whitefather10

New Member
Joined
Aug 22, 2022
Posts
2
Reaction score
0
Habari wana TANZANIA TUITAKAYO.

Utangulizi.

Ninayofuraha kupata wasaa huu kuandaa andiko langu linalohusiana na mazingira.

Neno mazingira limefafanuliwa katika mawanda mapana lakini ngoja nilitolee maana rahisi na ya kawaida ikimaanisha jumla ya vitu vyote vinavyotuzunguka vilivyo na visivyo na uhai kama vile miti, Maji, Mawe na vinginevyo vyote vinavyotuzunguka. Mazingira ndiyo msingi mkubwa wa Maisha ya binadamu na viumbe wengine kwani huyategemea kwa kiwango kikubwa kujipatia malighafi, hewa safi na dhana nyingine muhimu katika ujenzi wa jamii zetu.

Sambamba na kuiona dhana ya mazingira katika tafsiri nyepesi si busara kupita bila kutoa ufafanuzi kuhusu kiini cha Mada ambacho ni uchafunzi wa mazingira. Neno uchafunzi wa mazingira linamaanisha mlundikano wa taka au uchafu katika mazingira ambazo huleta madhara makubwa katika mazingira na ustawi wa Maisha ya binadamu kiujumla. Uchufuzi wa mazingira husababishwa na mambo mengi sana lakini kabla hatujakwenda kuona sababu hizo ni vyema tukagusia kidogo viashiria vya uchafu katika mazingira ambavyo ni hewa chafu, mlundikano wa taka aina zote, kutuama kwa maji taka muda mrefu katika makazi ya watu na moshi utokao viwandani.

Visababishi vya uchafuzi wa mazingira hasa katika miji mikubwa hususani ndani ya jiji la Dar es Salaam na viunga vyake zinapofanyika shughuli nyingi za kibinadamu ni moja; utupaji taka holela barabarani, masokoni, mitaroni na sehemu za uwazi na hii ndo changamoto kwa kiwango kikubwa. Watu wengi wamekua na utamaduni mbovu wa uchafuzi wa mazingira kwa kujua na kwa makusudi kutupa hovyo taka wamalizapo kutumia bidhaa walizokua wanatumia mfano chupa za vinywaji, Maganda ya matunda, karatasi, mifuko na vifungashio vya plastiki pamoja na maboksi yaliyokwishatumika suala hili naliunganisha na ukosefu wa elimu ya uelewa Pili; kukosekana kwa viwekea taka mitaani na maeneo zifanyikapo shughuli za kiuchuni mfano masokoni hata ndani ya daladala. Jambo hili huchangia kiasi kwa kikubwa kuongeza na kuzagaa kwa taka katika mazingira kwani mbali ya kuwa na wazoa taka wanaopita kwa vipindi lakini wanapofika kuchukua taka kwenye sehemu zilizotengwa wanabeba zilizoko kwenye vibebeo ila zilizoko chini wanaziacha hivyo kupelekea ongezo kubwa la uchafu wa mazingira.

Tatu, mlundikano wa maji mitaroni na mifumo mibovu ya usafirishaji maji taka. Kutokana na miundombinu mibovu ya usafirishaji maji taka hasa maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu hupelekea kuziba kwa mifumo ya usafirishaji maji taka hasa mitaro. Vilevile kuna wakati watu huzibua bomba chemba za vyoo ambazo hubeba masalia ya maji taka ya vyooni na wanapozibua Maji taka hayo husalia mitaroni na hivyo kufanya mazingira yaendelee kuwa machafu na kuacha harufu mbaya kali. Vilevile maeneo mengi ya masoko mfano soko la Ilala Boma hakuna miundombinu rafiki ya usafirishaji maji kwani ukifika kila wakati utakuta maji yametuama katikati ya soko na kufanya baadhi ya wafanyabiashara kukimbia vizimba vyao kutokana na hali hiyo isiyo rafiki kwao.

Nne, kukosekana kwa uthubutu wa vyombo imara vinavyosimamia utunzaji na uhifadhi wa mazingira kwa weledi. Pamoja na kuwa na vyombo vya usimamizi wa mazingira Tanzania mfano Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira lililoanzishwa chini ya Sheria ya usimamizi wa mazingira Sura ya 191 ya mwaka 2002 na kulipa jukumu la kuhakikisha utunzaji na uhifadhi wa mazingira lakini bado kuna dosari kubwa katika uendeshwaji wake.

Baraza limeshindwa kuishi kwenye majukumu yake kikamilifu kama yalivyotolewa kwenye kifungu cha 4 cha Sheria hiyo sura ya 191 ya mwaka 2002. Suala la ukusanyaji taka na uzoaji/ubebaji limekua na kasoro sana maeneo mengi jijini Dar es Salaam kwasababu vyombo vya usimamizi wa mazingira vimezipa taasisi na makampuni binafsi jukumu hilo bila ufuatiliaji wa kina. Kuzipa kampuni binafsi jukumu hilo bila ushirikishwaji wa jamii unaleta kasoro kwani wengi huchukulia kama suala la kimaslahi binafsi hivyo hata wakiona uchafu umezagaa mtaani wanachukulia kama suala la vyombo vya usimamizi wa mazingira na wadhabuni.

Madhara yanayotokana na uchafuzi wa mazingira hususani ndani ya jiji la Dar es Salaam.

Madhara yatokanayo na uchafuzi wa mazingira katika maeneo mengi huwa yanasababisha hasara nyingi sana katika jamii kwani hupelekea kwanza kabisa mlipuko wa magonjwa ya kuambukizwa mfano kipindupindu na malaria kwa kiasi kikubwa hili hutokana na kutuama kwa maji na kulundikana kwa taka chafu ambazo huoza na kutoa wadudu ambao kiafya huadhiri afya zetu. Kupata magonjwa tu ni suala la kwanza ila suala la pili ni garama kubwa zinazotumika kutibu wagonjwa wa kipindupindu punde utokeapo mlipuko. Kwa ufafanuzi uliotolewa na wizara ya afya chini ya Waziri Ummy inakadiriwa mgonjwa mmoja garama yake ni kati ya Tsh.300,000 hadi Tsh.500,000 ambapo serikali hupata hasara kwa kugaramia matibabu ya wagonjwa hao tena wakiwa kwenye wodi zao zilizotengwa.

Pili husababisha harufu chafu hasa masokoni na pembezoni mwa barabara kutokana na kuziba na kutuama kwa maji sio kipindi cha mvua tu bali muda wote. Tatu hupelekea kuwa na mazingira machafu ambayo hayavutii na baadae kupoteza mwonekano wa miji yetu kwa kiasi kikubwa hatimaye kupelekea kudorora kwa uchumi kwa kutowavutia watu kujihusisha na shughuli zozote maeneo hayo.

Nini kifanyike ili kuepukana na tatizo la uchafuzi wa mazingira?

Yafuatayo ni mapendekezo yangu ambayo kwa kiasi kikubwa yatasaidia kutibu tatizo hili kama ifuatavyo;
Kwanza, kuweka vibeba taka (dusterbin/containers ) maeneo yote yenye mikusanyiko mikubwa ya watu kama masokoni, stendi za vyombo vya usafiri na mitaani palipo na makutano makubwa ya watu. Napata ujasiri wa kuzungumzia suala hili kwani kwa kiasi kikubwa litasaidia kutibu uzagaaji taka na itakua muaribaini wa ukusanyaji taka kwa wepesi pia kuwapa urahisi wabebaji wakati wanapita maeneo yote yaliyotengwa.

Ukweli uko hivi kuiga kitu sehemu nyingine chenye manufaa sio dhambi naomba kutolea mfano mji wa Moshi namna zoezi Zima uhifadhi na utunzaji wa mazingira linazopewa kipaumbele kupitia elimu na utendaji wake linavyosaidia ukusanyaji taka na ubebaji kuwa rahisi. Moshi wamekua na mfumo mzuri wa kuweka vyombo maalumu mfano wa makontena makubwa ambayo wameyaweka masokoni na sehemu zenye mikusanyiko mikubwa ya watu kama Chombo rasmi cha kukusanya taka zote na kila mtu ameelekezwa namna ya kupeleka taka kwenye chombo hicho hivyo ni ngumu kuona taka masokoni au mitaani zikiwa zimezagaa.

Pili, kutumia njia ya kurudisha taka kuwa malighafi na kuzibadilisha kuwa bidhaa mpya. Hakuna kitu kisicho na faida kwa upande mwingine ukiachilia mbali ubaya wake, naomba kusema ya kwamba taka ambazo zimeonekana ni uchafu tukizitumia vizuri zinageuka kuwa malighafi na kupunguza mlundikano wa uchafu jalalani(dampo) pia kuwa fursa kwa wanajamii kiujumla. Kivipi sasa zitageuka kuwa fursa, kama nilivyofafanua kwenye hoja ya kwanza tukiwa na utaratibu mzuri wa kuweka vibeba taka maeneo yote yenye mikusanyiko mikubwa ya watu na vibebea taka hivyo tukivigawa kulingana na aina ya taka mfano taka za kijani kama (mbogamboga,nyasi,masalia ya vyakula), taka jamii za karatasi mfano boksi na taka jamii ya ya plastiki zikiwa kwenye kibebea chake zitatumika kama malighafi ya kuzalisha bidhaa mpya. Ili kuthibitisha hayo naomba kutoa mifano hai ya baadhi ya kampuni zilizogeuza taka kuwa malighafi na fursa kwa jamii.

Biobuu; hili ni kiwanda kilichoanzishwa na bwana Kigen Compton mwaka 2021 kikizalisha vyakula vya mifugo kwa kutumia masalia ya taka na nzi pamoja na kuzalisha mbolea zitumikazo mashambani kuoteshea mbogamboga. Green waste _ hiki ni kiwanda kilichoanzishwa huko Zanzibar miaka ya 2020 kikitumia taka za kijani kama mbogamboga zilizooza na nyasi kuzalisha mboji itumikayo mashambani iitwayo Bokashi.

Ujerumani and Moshi - manispaa ya Moshi kupitia kamati za mazingira mwaka 2021-2022 walianzisha kampeni ya usafi wa mazingira wakapata nguvu kutoka Ujerumani wakaanzisha kiwanda cha kuzalisha Mboji kwa kutumia taka zitolewazo masokoni.

Amref na kamati za mazingira walifanikiwa mwaka 2021 kutumia fursa ya ukusanyaji taka jamii ya karatasi kama boksi na majani yaliyouka kuzalisha bidhaa iitwayo mkaa taka jijini Dar es Salaam na kufanikiwa kutoa ajira kwa wanajamii wengi hasa waishio maisha ya chini. Kuna wengine waliofanikiwa kutengeneza tofali za kujengea kwa kutumia taka za plastiki kama chupa zilizokwishatumia.

Tatu, kutoa elimu ya utunzaji wa mazingira na kuwafanya watu wawe rafiki wa mazingira ili waweze kulinda na kudumisha usafi kwenye mazingira yanayowazunguka. Sambamba na kupewa jukumu lote la kushughukia uhifadhi na utunzaji wa mazingira chini ya Baraza na kamati za mazingira lakini kumekuwa na dosari kubwa kwenye utendaji kwani vyombo hivyo vimeshindwa kushirikisha vizuri jamii katika suala la mazingira zaidi sana vimetoa kipaumbele kwenye asasi binafsi mfano kampuni kwa kuzipa dhabuni kujihusisha na ubebaji taka suala ambalo linakosa ufanisi kwani uzagaaji taka na uchafu unazidi mitaani.

Kipi kifanyike ni kurudisha majukumu mikononi mwao kwa kuwapa elimu wanajamii na kuwashirikisha katika zoezi zima la uhifadhi wa mazingira. Tukumbuke kampuni binafsi zinajikita kwenye maslahi na sio uzalendo hivyo hata kukiwa na dosari sehemu hawataweza kujitoa kwani kufanya hivyo wanahisi kutawapatia hasara lakini serikali kushirikiana na wanajamii watatatua dosari hiyo kwa haraka ili madhara yasiwe makubwa.

Hitimisho.
Nje ya Mada kuu ningependa niwakumbushe watu na kuwasisitiza juu ya upandaji wa miti ya kivuli na matunda majumbani mwetu ili tupate hewa safi pamoja na vivuli vya kupumzika tuwapo majumbani mwetu siku za mapumziko. Ukweli ni kwamba ongezeko la joto kwa kiasi fulani hutibiwa na miti kuzunguka nyumba na makazi yetu kwani uwepo wa miti huleta upepo na hewa safi .
Asante.
 
Back
Top Bottom