CUF njia panda uchaguzi Tarime
2008-09-26 09:14:05
Na Muhibu Said
Hatua ya vyama vya Chadema na NCCR-Mageuzi kusimamisha wagombea ubunge katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Tarime, mkoani Mara, imekiweka Chama cha Wananchi (CUF) njiapanda, baada ya makao makuu ya chama hicho hadi sasa kushindwa kuamua mgombea wa chama kipi kati ya vyama hivyo `wampigie debe`.
Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na TLP, ni vyama vilivyoamua kuunda ushirikiano wa kisiasa katika kambi ya upinzani na miongoni mwa makubaliano waliyofikia katika ushirikiano huo, ni pamoja na kushirikiana katika chaguzi kwa lengo la kukishinda katika uchaguzi na kuking`oa Chama Cha Mapinduzi (CCM) madarakani.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF Tanzania Bara, Wilfred Lwakatare aliliambia Nipashe ofisini kwake jijini Dar es Salaam juzi kuwa, hadi sasa makao makuu ya chama hicho, hawajafikia uamuzi wa mgombea wa chama kipi wamuunge mkono katika uchaguzi kwa madai kwamba suala hilo linahitaji busara kabla ya kuamua.
``Sisi baada ya kuona uwezo wetu ni mdogo wa kushinda jimboni humo, tuliamua kumwondoa mgombea wetu. Wenzetu NCCR na Chadema wamesimamisha wagombea. Mgombea wa chama kipi kati ya hivyo tuelekeze nguvu zetu, suala hilo linahitaji busara ya hali juu kuamua,`` alisema Lwakatare.
Hata hivyo, alisema watafikia uamuzi wa mgombea wa chama kipi wampigie debe, mara tu watakapopata taarifa kutoka kwa uongozi wa CUF Tarime kutokana na upepo wa kisiasa katika kinyang`anyiro cha uchaguzi huo utakavyokuwa ukienda.
``Tutakapopata taarifa kutoka uongozi wa CUF Wilaya ya Tarime, ndipo tutaamua namna ya kushiriki uchaguzi huo,`` alisema Lwakatare.
Hata hivyo, Lwakatare alisema kwa sasa wamempeleka Tarime, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya CUF, ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza Kuu la chama hicho, Mustapha Wandwi, kushiriki uchaguzi wa marudio wa udiwani.
Uchaguzi wa ubunge katika jimbo la Tarime , ambao unafuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wake, Chacha Wangwe aliyefariki dunia kwa ajali ya gari katika eneo la Pandambili, Wilaya ya Kongwa, mkoani Dodoma, Julai 28, unatarajia kufanyika Oktoba 12, mwaka huu.
Katika uchaguzi huo, Chadema imemsimamisha Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Charles Mwera wakati NCCR-Mageuzi, imemsimamisha Enock Haruni, maarufu kama `Machomanne`, ambao watapambana na mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kimemsimamisha Christopher Ryoba Kangoye kuwania kiti hicho.
SOURCE: NIPASHE
Tarime ni soo!
2008-09-26 16:35:51
Na Mwandishi Wetu, Tarime
Wakati siku za kuelekea uchaguzi mdogo wa kumsaka mbunge wa Jimbo la Tarime zikizidi kukaribia, hali ya kisiasa mjini hapa imeanza kuwa tete baada ya wafuasi wa vyama vinavyoshiriki uchaguzi huo kuendelea kufanyiana visa mfululizo, vikiwemo vile vya kumwagiana pilipili na kuwatwangana mawe mikutanoni.
Uchaguzi huo mdogo, unatarajiwa kufanyika Oktoba 12, ili kujaza nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Marehemu Chacha Wangwe, aliyefariki mjini Dodoma Julai 28 mwaka huu baada ya kupata ajali ya gari.
Jana, muendelezo wa visa vya baadhi ya wafuasi wa vyama hivyo vya CCM, CHADEMA, NCCR-Mageuzi na DP ulifikia pabaya baada ya Mwenyekiti wa UDP, mchungaji Christopher Mtikila kupigwa jiwe la kichwa wakati akiwa kwenye mkutano wa kampeni kwenye viwanja vya Sabasaba.
Mtikila alijeruhiwa vibaya na kukukimbiziwa hospitali mjini hapa ambako inadaiwa alishonwa nyuzi saba.
Kutokana na vibweka vinavyoendelea katika kampeni za kuelekea siku ya uchaguzi huo, , viongozi mbalimbali wa vyama vilivyosimamisha wagombea wamekuwa wakitoa kauli tofauti kuhusiana na yanayojiri.
Dk. Sengondo Mvungi (NCCR-Mageuzi)
Yeye aliripotiwa kuwa kiongozi wa kwanza kufanyiwa vurugu wakati wa kampeni jimboni humo.
Mvungi alikumbana na kadhia ya kutimuliwa kwa mawe wakati akimnadi mgombea wa chama chake cha NCCR.
Baada ya hapo, Dk. Mvungi ambaye pia ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alilaani tukio hilo na kueleza kuwa ni la hatari, kwani hakuna chama chenye hakimiliki ya jimbo hilo.
Pius Msekwa (CCM)
Makamu huyu Mwenyekiti wa CCM, naye alionja ya joto ya jiwe ya kufanyiwa vituko vya kampeni hizo wakati alipokuwa akimnadi mgombea wa chama chake, Bw. Ryoba Kangoba.
Msekwa alifanyiwa fujo na kuzomewa na watu wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa vyama pinzani.
Aidha, wafuasi wawili wa chama chake wameripotiwa kuumizwa baada ya mmoja kupigwa jiwe na mwingine kumwagiwa pilipili.
Kutokana na hali hiyo, bosi huyo namba mbili wa CCM akailalamikia hali hiyo na kuripotiwa akitishia kulifikisha suala hilo kwa Rais Jakaya Kikwete ili hatimaye zifanyike taratibu za kudhibiti hali ya namna hiyo ambayo ni ya hatari.
Christopher Mtikila (DP)
Baada ya kasheshe la jana la kupigwa mawe kwenye uwanja wa Sabasaba, amekaririwa akilalamikia hali hiyo aliyodai kuwa imetokana na njama za wapinzani wake.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mtikila amekaririwa leo asubuhi akisema: ``Nilitoa taarifa mapema kwa Msimamizi wa Uchaguzi na OCD.. niliwaeleza juu ya agizo la mimi kupigwa mawe...``
Freeman Mbowe (CHADEMA):Mbowe na chama chake cha CHADEMA wamekuwa nao wakilalama kuonewa na askari polisi walio katika operesheni kali ya kulinda amani katika jimbo hili.
Aidha, kwa nyakati tofauti, yeye, Katibu Mkuu wake Dk. Wilbroad Slaa na Mbunge wa Viti Maalum wa chama hicho, Halima Mdee, wamekuwa wakitoa madai ya kuonewa kwa kunyimwa viwanja vya kufanyia kampeni za mgombea ubunge wa chama chao, Bw. Charles Mwera.
Prof. Ibrahim Lipumba (CUF)
Baada ya kutosimamisha mgombea jimboni humo ili kuwapa fursa wenzao wa upinzani jimboni humo, Prof. Lipumba na chama chake wamekuwa katika wakati mgumu wa kuamua wamuunge mkono mgombea yupi baada ya wenzao kuwasaliti kwa kusimamisha mgombea zaidi ya mmoja, kinyume cha makubaliano.
Mkanganyiko huo unadaiwa kutokea baada ya vyama vinavyoungana nacho katika umoja wao wa vyama vikiwemo vya CHADEMA, TLP na NCCR-Mageuzi kushindwa kumsimamaisha mgombea mmoja, hasa baada ya NCCR na CHADEMA kusimamisha wagombea wawili tofauti.
Hata hivyo, ingawa CUF Tarime wameamua kumuunga mkono Bw. Charles Mwera wa CHADEMA, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Bw. Wilfred Lwakatare, amekaririwa asubuhi ya leo akisema kuwa wamemtuma jimboni humo kiongozi wao Mustafa Wandwi ili kuangalia ni mgombea yupi anayeelekea kukubalika zaidi ili hatimaye wamuunge mkono.
Wakati huohuo, Jeshi la Polisi jimboni humo limesema liko makini katika kudhibiti vitendo vyote vinavyoashiria kuvunja amani.
Akizungumza na Alasiri juzi, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara, Liberatus Barlow, amesema FFU na polisi wengine kibao waliomwagwa jimboni humo wamejipanga vilivyo katika kuhakikisha kuwa uvunjifu wa amani unadhibitiwa ipasavyo.
Wakati huohuo, katika kuthibitisha kuwa Polisi wako makini, tayari wameshawanasa watu wanne wanaotuhumiwa kumvurumishia mawe Mchungahji Mtikila jana na kuwawezesha kuburuzwa kortini.
Walionaswa na polisi katika tukio hilo la jana na ambao leo wamepandishwa kizimbani ili kujibu mashtaka.
Kamanda Barlow amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Mussa Peter, Mwita Chacha, Hafidh Stanslaus na Mwita Kilongo.
Amesema watuhumumiwa hao, mmoja alikamatwa wakati wa tukio la kupigwa kwa Bw. Mtikila na wengine watatu walikamatwa jana katika msako wa Polisi uliofuatia kujiri kwa tukio hilo la kupigwa kwa Mtikila.
SOURCE: ALASIRI
`Ndoa` ya Chadema, TLP, CUF yavunjika
2008-09-13 09:40:54
Na Simon Mhina
Ushirikiano wa kisiasa kati ya vyama vinne vya upinzani, umesambaratika baada ya vyama vitatu kati ya hivyo kuamua kusimamisha mgombea mmoja katika uchaguzi mdogo wa Tarime.
Wenyeviti wa vyama hivyo, Augustine Mrema (TLP) Profesa Ibrahim Lipumba (CUF) na James Mbatia (NCCR- Mageuzi) juzi walifanya kikao cha kujadili uchaguzi huo, na kumtenga mwenzao wa Chadema, Freeman Mbowe.
Japokuwa Profesa Lipumba alisema kwamba taarifa za kumwalika Mbowe zilitumwa, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilibrod Slaa, alisema hakuna mwaliko wowote uliotumwa kwa bosi wake na Chama chake hakina mawasiliano yoyote na viongozi wa vyama hivyo vitatu.
Hata hivyo, Profesa Lipumba hakuweza kueleza kwamba walitumia njia gani kumpelekea Mbowe taarifa.
``Unajua hapa katikati kumetokea sintofahamu zilizosababishwa na kifo cha Wangwe (Mbunge wa zamani wa Tarime, Chacha), kuna kamgogoro baridi kanafukuta ndio maana hawakuhudhuria,`` alisema.
Alisema vyama vitatu vimeamua kuweka mgombea mmoja ili kuhakikisha wanapata ushindi mkubwa Tarime.
Lipumba alisema baada ya kikao cha viongozi wakuu, wamepeleka madaraka yao kwa viongozi wa vyama vyao Jimbo la Tarime.
``Vikao vya wenyeviti wa taifa havitoshi, tunataka wenzetu wa Tarime nao wakutane, wao wanajuana na wanaelewa mazingira yao zaidi. Tunataka nao watuletee mapendekezo yao,`` alisema.
Hata hivyo, kiongozi huyo alisema kwamba ushirikiano wa vyama hivyo, hauondoi haki ya kila chama kufanya shughuli zake kwa mujibu wa sera na katiba yake.
Awali akitoa taarifa za kikao hicho, Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Uchaguzi wa NCCR, Faustine Sungura, alisema kwa kauli moja, viongozi hao wamependekeza mgombea wa Chama hicho apitishwe.
Alimtaja mgombea aliyependekezwa kuwa Enock Haruna Marwa maarufu kwa jina la Macho Manne.
Sungura alisema kikao hicho kilichofanyika siku nzima, viongozi wa Chadema waliingia mitini.
Alisema haelewi ni kwanini viongozi wa Chadema waliingia mitini bila kutoa taarifa yoyote.
Awali akizungumzia sakata hilo, Dk. Slaa alisema pamoja na kutengwa na wenzao, wataendelea na maandalizi yao ya kuingia vitani.
``Tutaingia vitani kivyetu vyetu, hatuwezi kurudi nyuma. Lazima jimbo la Tarime tutalirudisha mikononi mwetu,`` alisema.
Alisema kutokana Chadema kutengwa ghafla na wapinzani wenzake, kitachukua hatua kadhaa kuhakikisha Jimbo hilo haliendi CCM kama ilivyokusudiwa.
Alisema Tarime kuna rasilimali nyingi ambazo zinaporwa, hivyo waporaji wanaweza kuhakikisha wanasaidia mkakati wowote wenye lengo la kuifanya Tarime iwe ya CCM.
Mbunge huyo alisema Chadema kina mtaji mkubwa wa kisiasa Tarime, hivyo hakitishwi wala kubabaishwa na uamuzi wa kutengwa.
Vyama vya Chadema, TLP na CUF vilianza ushirikiano rasmi bungeni na kuunda kambi rasmi ya upinzani ambayo inatambulika rasmi bungeni.
Tangu kifo cha Wangwe kilichotokea kwa ajali ya gari Julai 28, 2008 iliyotokea kijiji cha Pandambili, Kongwa mkoani Dodoma akiwa safarini kwenda Dar es Salaam, kumekuwa na mvutano wa wazi baina ya viongozi wa kambi hiyo.
Tukio la kipekee lililotokea ni pale mazishi ya Wangwe yalipoahirishwa Julai 31, 2008 kutokana na familia kutaka uchunguzi wa kujitegemea juu ya chanzo cha kifo cha mbunge huyo, hali iliyowagawa viongozi hao kwenye makundi mawili.
Chadema wamekuwa wakilaumu wenzao kwamba walitaka kutumia msiba huo kupata faida ya kisiasa Tarime na kukiangamiza chama hao. Lawama ambazo pia zimeelekezwa kwa CCM.
SOURCE: NIPASHE