JULAI 28, Kanisa Katoliki humkumbuka Victor I aliyekuwa papa wa kwanza kutoka Afrika, aliyezaliwa Libya akafariki dunia mwaka 198.
Afrika ilitoa tena papa aliyeitwa Papa Melchiades aliyetoka kabila la waberiberi aliyefariki dunia Januari 11, 314. Zinedine Zidane, aliyekuwa mcheza mpira wa Ufaransa, naye ni mberiberi kama alivyokuwa papa huyu.
Afrika ilibahatika tena ilipotoa papa kwa mara ya tatu na ya mwisho, yaani Papa Gelasius I, naye Mberiberi..
Bara linaloweza kudai kwamba halijawahi kutoa papa ni Amerika ya Kusini kwani Mitume wa Yesu, walitoka Israel iliyoko Asia na wakazi wa Australia na Amerika Kaskazini ni wahamiaji waliotoka Ulaya.
Zamani ilikuwa haiwezekani mtu ambaye tayari ni askofu kwingine ateuliwe kuwa papa. Waumini wa Roma walikuwa wanamchagua shemasi wanayemridhia, kisha maaskofu wa jirani na Roma wakiongozwa na askofu wa Ostia wanampa daraja la uaskofu ndipo aanze kazi ya upapa.
Ndivyo Celestine III alivyoteuliwa kuwa papa Machi 30, 1191 akiwa hajapata upadri aliuopata Aprili 13, 1191 yaani siku 14 baada ya uteuzi wake, na kesho yake akapewa uaskofu.
Julai 16, 1054 ilikuwa ni siku mbaya zaidi katika Ukatoliki, ambapo kanisa lilitengana na kuwa makundi mawili yaani Kanisa la Magharibi na la Mashariki.
Kuepusha matatizo kama haya, maaskofu wote duniani walikutana Lateran mwaka 1179 wakakubaliana kwamba kazi ya kumchagua papa iachwe kwa makardinali tu.
Je, kardinali ni nani? Kwa maana halisi ya neno kardinali, kila Mkatoliki unaweza kumuita kardinali.
Sheria za Kanisa Katoliki yaani Can. 100-102, 265, zinaelekeza kwamba ni lazima padri au mlei atambulike ni wa jimbo au shirika gani. Kitendo cha kusajiliwa na kujulikana sehemu uliyopo kinaitwa in-cardination.
Hivyo, padri hawezi kuondoka jimbo kama la Njombe alikosimikwa (incardinated) bila ruhusa ya askofu wake, akaenda kuanzisha kituo cha maombi pale Riverside, ambako ni Parokia ya Makuburi kwenye jimbo jingine kabisa, yaani DSalaam ambako hajasajiliwa.
Hili ndiyo matumizi halisi ya neno in-cardination ambalo kama lilivyo neno cardinal linatokana na neno cardo, yaani kitendo cha bawaba kuusimika mlango usibanduke ukutani.
Baadaye , neno cardinal liliishia kutumika kwa mapadri na maaskofu walioitwa Roma kwa papa ambako aliwasimika kwenye makanisa yaitwayo Titular na wakahesabika kuwa ni wa jimbo la Roma.
Kanisa linaruhusu umisionari halali wa kufanya kazi eneo jingine duniani hata kama unahesabika kwingine mradi taratibu zifuatwe. Eusebius Nzigilwa ni askofu wa Mozotcori ingawa haishi huko Tunisia bali yuko Tanzania kama msaidizi wa askofu wa D'Salaam.
Polycarp Pengo aliyeko DSalaam kwa ajili ya uchugaji wa jimbo hilo, ukardinali wake unamfanya ahesabike kuwa ni wa Roma kwenye kanisa liitwalo Nostra Signora de La Salette.
Niliufafanua ukardinali Agosti 30, 2009 kwenye gazeti hili.
Je, mtu asiye Mkatoliki anaweza kuchaguliwa kuwa papa? Mwaka 374, Aurelius Ambrosius alipoteuliwa awe askofu wa Milan huko Italia, alisita kukubali kwa sababu hakuwa Mkatoliki, bali alikuwa mpagani.
Aliposhawishiwa sana na hatimaye akakubali, hatua ya kwanza ilikuwa kumbatiza hapo Novemba 29, 374. Siku nane baadaye, Desemba 07, 374 ndipo akapewa daraja la uaskofu, siku inayoadhimishwa na kanisa hadi leo kumkumbuka.
Mafundisho ya Kanisa Katoliki kama yanavyotuelekeza kwenye vifungu 1557-8 vya Katekism yanasema kwamba unapopewa daraja la uaskofu basi unakuwa umepata upadri uliokamilika.
Kumbe, ikilazimika Kanisa Katoliki limteue papa asiyekuwa Mkatoliki, basi itampasa kwanza abatizwe kama tulivyoona kwa Ambrosius, kisha apewe daraja la uaskofu kama tulivyoona kwenye Katekismu kifungu 1557-8.
Kitendo cha mtu kupewa uaskofu bila kupitia hatua ya ushemasi na upadri, kinaitwa consecration per saltum.
Haitarajiwi hata siku moja upapa au uaskofu apewe mwanamke halafu tumuite kuwa ni mchungaji wetu wakati Yesu mwenyewe hakuchagua wachungaji wa kike bali wanaume kumi na mbili.
Mwandishi yeyote anayeelekea kufahamu sana mambo ya Vatican hupewa jina Vaticanista. Orodha zinazosambaa duniani zikiwataja Papabili yaani wanaotarajiwa kuwa papa ni za hawa Vaticanista.
George Weigel Vaticanista wa gazeti la Newsweek alieleza kwamba mwaka 2004 Padri Thomas Herron na wa Philadephia na George Kardinali Pell wa Australia walitabiri kwamba Joseph Kardinali Ratzinger ndiye atakuwa papa baada ya John Paul II.
Wakati Vaticanista John Allen, mmarekani wa National Catholic Reporter, alitumia kurasa 21 kumponda Joseph Ratzinger akisema hatachaguliwa kuwa Papa.
George Weigel ndiye Vaticanista aliyediriki kumtaja Polycarp Kardinali Pengo wa D'Salaam kwamba ingawa hakufikiriwa kwenye uchaguzi wa 2005, lakini anatazamwa na baadhi huko Roma kama papa wa siku zijazo.
Makardinali wanapowasili Roma kwa ajili ya uchaguzi wa papa, kila siku huwa wana mikutano rasmi iitwayo General-Congregation wanakojadili masuala yanayolikabili kanisa kama dira ya uchaguzi.
Lakini, pia huwa kuna mikutano isiyo rasmi ambayo George Weigel anaiita prattiche ambako ndipo hasa siasa za uchaguzi wa Papa hufanyika.
Prattiche inaweza kuwakutanisha idadi yoyote na wakakaa popote jijini Roma kujadili wamchague nani.
Giovani Kardinali Benelli alizitumia vizuri prattiche kuhakikisha Albino Lucian anajulikana na hatimaye akachaguliwa kuwa Papa John Paul I.
Katika Prattiche za mwaka 2005 vikundi viwili vya walei yaani Focolare na Sant'Egidio vilionekana kushawishi ili Dionigi Kardinali Tettamanzi wa Milan, Italia ateuliwe kuwa Papa.
Haya ni machache kati ya mengi ambayo hufanyika kabla ya kuingia kwenye kanisa liitwalo Sistina ambako uchaguzi wa papa hufanyikia.
Wengi hupenda papa atoke eneo lao. Kardinali wa kwanza Afrika kushiriki uchaguzi wa Papa alikuwa ni Teodosio Gouveia wa Msumbiji aliyeupata ukardinali miaka 14 kabla ya Laurean Rugambwa wa Bukoba.
Septemba 26, 1997, Agostino Kardinali Casaroli alitamka mbele ya Papa John Paul II na wageni wengine kwamba anaona inafaa baada ya John Paul II iwe ni wakati wa Italia kushika tena upapa.
Lakini hata hivyo, makardinali wa Italia wamegawanyika katika makundi mawili. Wapo wanaofanya kazi pale Vatican, wanaitwa Curiarists na ambao wamo majimboni wanaitwa pastoralists.
Kama itakuwa ni zamu ya kurudishwa upapa Italy, basi majina ya Waitalia yaliyongara kwenye prattiche za mwaka 2005 yanaweza kupata nafasi kubwa safari hii.
Angelo Kardinali Scola alitajwa sana mwaka 2005 kwamba alikuwa katika kundi la pili la kufikiriwa baada ya akina Joseph Ratzinger.
Kardinali Scola hata safari hii haachi kutajwa zaidi ukizingatia kwamba amepata bahati ya jimbo la Venice pia jimbo la Milan.
Ukipewa Jimbo la Venice alilokuwa wakati wa uchaguzi wa 2005, ni heshima ndani ya Kanisa Katoliki kwani unaitwa Patriarch na unaruhusiwa kuvaa mavazi ya kardinali hata kama hujawa kardinali.
Jimbo hili la Venice, limeshatoa mapapa watatu yaani Pius X (1903) , John XXIII (1958) na John Paul I (1978).
Wakati Jimbo la Milan alilomo sasa, ambalo ndilo kubwa kuliko yote nchini Italia, nalo limeshatoa mapapa watatu yaani Pius IV (1559), Pius XI (1922) na Paul VI (1963).
Kwa sifa hizi ni wazi kwamba Angelo Kardinali Scola ana bahati kubwa ya kujikuta amekabidhiwa majimbo yaliyopitiwa na mapapa sita, bahati ambayo wengi hawajawahi kuipata.
Kwa sifa hizi, si rahisi Vaticanista wasimuweke Angelo Kardinali Scola kwenye orodha yao ya mwaka huu ya watu wanaofikiriwa zaidi kwamba wanaweza kutokea wakawa papa.
Shughuli ya kupiga kura kumchagua Papa huanza kwa makardinali kuapishwa kwamba watatunza siri na hawatatumia ujanja wowote wa kurekodi matukio ya mle ndani.
Anayekiuka usiri huo basi anakuwa amejifukuzisha mwenyewe ndani ya kanisa Katoliki kama alivyojifukuzisha Askofu Emmanuel Millingo.
Kura huhesabiwa mbele ya wote na watu waitwao Scurtiners ambao wakimaliza zinahakikishwa tena na wengine waitwao Revisors ndipo matokeo yanakubalika.
Kwenye uchaguzi wa mwaka 2005, mshindi alitakiwa apate zaidi ya nusu ya kura za makardinali. Safari hii atatakiwa apate kuanzia asilimia 67.
Yanayoandikwa kuhusu yanayotokea ndani ya chumba cha uchaguzi kwa sababu ni siri huwa ni ya kubahatisha na wakati mwingine ni mashindano ya kujionesha uwezo wa kuibua siri kuliko wengine.
Mfano ni vitabu viwili, kimoja cha David Yallop In God's Namena kingine cha George Weigel God's Choice.
Wote hawa wawili wamezungumzia uchaguzi wa 1978 uliompata Papa John Paul I, aliyedumu kwa siku 33 tu akafariki dunia.
David Yallop katika ukurasa wa 66 hadi 67 anaonyesha kwamba kwenye kura za uchaguzi huo, Sergio Kardinali Pignedoli alifika hadi raundi ya tatu na kupata hadi kura 18.
Wakati George Weigel katika ukurasa wa116 hadi 117 anaonesha kwamba hakuvuka hata raundi moja na kama alipata kura basi hazizidi mbili.
Kura zinapoonesha kuwa mshindi hajapatikana, basi zinakusanywa na kuwekewa dawa (chemical) ambayo zitakapochomwa itaufanya moshi uonekane mweusi na walioko nje wajue kwamba papa hajapatikana.
Mshindi anapopatikana, kura zinachomwa moto, lakini safari hii inawekwa dawa ya kuufanya moshi uwe mweupe ili watu wajue kwamba sasa papa ameshapatikana.
Si rahisi kujua papa anayekuja ni nani na hivyo si rahizi kujua atakuwa na jina gani. Kama anayekuja atachagua jina Paul basi atakuwa Paul VII, atakayechagua jina Pius ataitwa Pius XIII, atakayechagua jina John ataitwa John XXIV, na kama ni Benedict litarudiwa basi ataitwa Benedict XVII.
|
|