SoC03 Udhaifu wa Mahakama ya Tanzania ni kikwazo cha Utawala wa Sheria

SoC03 Udhaifu wa Mahakama ya Tanzania ni kikwazo cha Utawala wa Sheria

Stories of Change - 2023 Competition

Konny Joseph

Senior Member
Joined
Aug 28, 2016
Posts
118
Reaction score
199
UTANGULIZI

Kwa mujibu wa Ibara ya 4 ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, mamlaka ya nchi imeundwa na mihimili mitatu ambayo ni serikali,mahakama na bunge, na kila mmoja kati ya mihimili hiyo huwa na kazi yake katika kulinda na kusimamia maslahi ya taifa.

Kwa mujibu wa katiba bunge huwa na kazi ya kutunga sheria wakati huohuo likiwa na jukumu la kuangalia uwajibikaji wa serikali katika kutekeleza majukumu yake.

Mahakama huwa na jukumu mama la kutafsiri sheria na kusimamia utoaji wa haki kama chombo chenye mamlaka ya mwisho juu ya uamuzi wa jambo lolote linalohusu haki na muelekeo mwema wa taifa kwa ujumla wake.

Serikali kwa upande wake huwa na jukumu la kusimamia utekelezwaji wa sheria na taratibu zinazotungwa na bunge.Muhimili huu ndio wenye jukumu la kuhakikisha taifa linakwenda kulingana na sheria zilizopo.

Jukumu la bunge kuisimamia serikali kutekeleza majukumu yake hufanywa kupitia uwakilishi wa wanachi bungeni na sio kupitia mtu mmoja mmoja.Kwa msingi huo hata kama kutakuwa na udhaifu fulani kwa serikali katika kutekeleza jukumu lake, bunge linao uwezo wa kuingilia jambo hilo kwa utashi wake(in its own motion) au kupitia msukumo wa ujumbe ndani ya bunge, na sio kwa msukumo wa mtu au kikundi fulani kilicho nje ya bunge.

Kwa muktadha huo, mahakama ndio hubaki sehemu pekee ambayo mtu binafsi au kikundi cha watu kinapoona jambo lolote linalolenga uvunjifu wa haki za watu,kuvuruga utawala wa sheria,au kukwepa uwajibikaji kwa serikali,huweza kuwasilisha lalamiko hili mahakamani na mahakama kuchukua nafasi yake katika kutoa uamuzi wa haki katika tatizo hilo.

Ni katika mazingira haya ndio mahakama huisabika kuwa ndio chombo chenye mamlaka ya mwisho ya kutoa haki kwa maslahi ya taifa kama inavyoelekezwa katika Ibara 107A(1) ya Katiba.

Ni katika mazingira haya haya ndio mahakama huisabika kuwa ndio msuluhishi wa mwisho katika kusimamia haki na utawala wa kisheria katiaka nchi.

Na katika kutekeleza dhima hii nzito ndipo ambapo tunaweza kuona uthabiti au udhaifu wa mahakama katika kutekeleza majukumu yake kama chombo cha kutoa haki katika nchi.

Kwa kawaida mahakama ya Tanzania haina historia mbaya katika kusimamia haki na utawala wa sheria pale jambo linapohusu watu binafsi(individual conflict),changamoto kubwa tulioiona katika mahakama ya Tanzanioa ni pale inapotokea jambo linalohusisha serikali,Serikali ikawa ni moja ya upande wa lalamiko,aidha mlalamikaji au mlalamikiwa,hapo ndipo udhaifu ya mahakama ya Tanzania ninaolenga kuuongelea unapoonekana.

Pamoja na ukweli kwamba sheria ya Tanzania inaruhusu serikali kushitajkiwa na kuwajibishwa kulingana na kosa lolote itakalofanya au kufanywa na moja ya watendaji wake kupitia Sheria ya Mwenendo wa Mashitaka kwa Serikali(Government Proceeding Act,Cap 5,RE 2019)ila bado uwezo wa mahakama ya Tanzania kusimamia utaratibu huo umekuwa ni mdogo mno kiasi cha kukatisha tamaa wanaharakati na wananchi kwa ujumla wenye nia ya kutafuta haki ya kisheria kupitia muhimili huu.



UDHAIFU WA MAHAKAMA

Labda sasa nitowe mifano midogo ya kudhihirisha udhaifu wa mhimili huu.

Mnamo tarehe 27/07/2021 Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu(LHRC)kilifungua shauri Namba 11 la mwaka 2021 kuomba mapitio ya Mahakam Kuu(Judicial Review)kuhusu National Payment System Act,Cap 437 pamoja na kanuni zake zilizoweka tozo katika miamala ya fedha kwa njia ya simu.

LHRC walifungua kesi hiyo kufuatia kupitishwa kwa mapendekezo ya Bajeti ya serikali 2021/2022 pamoja na sheria ya fedha iliyopelekea kuweka tozo katika miamala ya fedha inayofanywa kwa njia ya simu,jambo ambalo liliongeza mzigo na kuzua malalamiko makubwa kwa wananchi wa kawaida.

Kilichoshangaza ni kwamba Jaji wa Mahakama Kuu,Kanda ya Daresalaam,Mh John Simon Mgeta alitupilia mbali shauri hilo kwa kisingizio kwamba kiapo cha mleta maombi hakikukidhi vigezo.

Kitu cha kujiuliza ni kwa nini Jaji Mgeta asingetoa ushauri kwa mleta maombi kurekebisha hati yake ya kiapo kama ambavyo jaji alivyoishauri serikali kurekebisha hati ya mashtaka katika kesi ya jinai ya iliyokuwa inawakabili Mh.Freeman Mbowe na wenzake.

Tuseme ni serikali pekee kama mmoja wa wanufaika wa mahakama ndio mwenye haki kusahihishwa pale inapotokea hitilafu ya kiufundi (techniqal issues) katika kuleta mashauri mahakamani.

Ikumbukwe kwamba mnamo Sep 2018,baada Mahakama ya Tanzania kuelemewa na mzigo wa mapingamizi ya awali(Preliminary Objection)ilipitisha sheria kuondoa changamoto hiyo ili kuiwezesha mahakama kutoa haki kwa wananchi badala ya kujikita katika kutupilia mbali kesi nyingi zinazowasilishwa mahakamani hapo kwa sababu ya kasoro na hitilafu ndogo ndogo zinazoweza kurekebishika au kuvumilika.



Sheria hiyo ya Marekebisho mbalimbali (Miscellaneous Amendment,No.3,2018)ilirekebisha vifungu mbalimbali vya kisheria ikiwemo Sheria ya Mwenendo wa Madai(Civil procedure Code,Cap 33,RE 2019) ambayo ndio sheria mama kwa kesi zote zenye mfumo wa madai.

Lengo kuu la mabadiliko haya ya sheria ni kuiwezesha Mahakama kujikita na misingi ya malalamiko kwenye kesi zinazowasilishwa mbele yake badala ya kuangalia Zaidi khitilafu ndogondogo zinazojitokeza katika namana ya kuwasilisha malalamiko hayo.

Ikumbukwe kwamba chimbuko la sheria hii ni Ibara ya 107(2)(e) ya katiba ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania inayoitaka mahakama kutobanwa na kasoro za kiufundi katika mchakato wa utoaji haki,badala yake ijikite zaidi na kuangali uzito wa lalamiko linalowasilishwa mbele yake.

Katika tathmini ya kawaida tu kesi hii ilikuwa na maslahi makubwa kwa taifa kwa kuwa ni kesi ambayo iligusa maslahi mapana ya watanzania walio wengi kama sio wote.Ilikuwa ni matarajio ya wengi kwamba Mahakama ingeipa kesi hii uzito mkubwa na wa aina yake na kutoa maamuzi ambayo ni ya kulinda maslahi ya Taifa na utawala wa kisheria.

Tofauti na matarajio ya watanzania walio wengi,Mahakama yetu iliishia tu kujikita katika mapungufu ya kiufundi yaliyojitokeza badala ya kujikita katika kulitafutia ufumbuzi lalamiko husika.

Katika kesi ya Zitto Kabwe dhidi ya Mwanasheria Mkuu,Kesi No.1ya mwaka 2020, akipinga Kifungu cha 6(1)cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma,Na.11ya mwaka 2008 kilichotumika kumuondosha Prof.Assad katika wadhifa huo.

Ingawa Mahakama ilikubaliana na Zitto kuwa kifungu hicho ni batili kwa kwa kuwa kinakinzana na katiba na kuwa Prof.Assad aliondolewa kinyume na katiba,ilikataa maombi ya kubatilisha uteuzi wa CAG wa sasa,Mh.Charles Kichele,kwa madai kwamba aliteuliwa kwa mujibu wa katiba na anazo sifa za kushika nafasi hiyo.Hapo ndio unapoona maamuzi ya Mahakama yetu yanapojikanganya.

Mahakama hii ndio imesema kuwa ibara 6(1)ya Sheria ya Ukaguzi wa Umma imekiuka katiba ya nchi.Mahakama hii hii pia ndio iliyokiri kwamba Pro.Assad aliondolewa kinyume na katiba.Ajabu ni kwamba Mahakama hii hii inarudi tena na kusema kuwa Uteuzi wa Charles Kichele upo kwa mujibu wa katiba.

Swali la kujiuliza mi katiba ipi iliyovunjwa kwa kumvua wadhifa huu Prof.Assad na ni katiba ipi iliyohalalisha uteuzi wa Charles Kicwhwele.

Kimsingi kama katiba ilishavunjwa kwenye utenguzi haiwezekani iwe imefuatwa kwenye uteuzi mwengine.Kitu chochote kilichopatikana kwa njia batili,kitabaki kuwa batili tu,wala hakiwezi kuhalalishika kwa namna yeyote ile.

Ni sawa na kusema,mtu alipata hela kwa njia ya wizi,itabaki kuwa ni chumo haramu tu wala haitamhalalikia kwa kigezo tu kwamba mtu huyo anayo haki ya kumiliki hela hizo.Jambo la msingi ni kwa namana gani pesa hizo zimepatikana.

Haya ni madhaifu machache katika madhaifu mengi xana yaliopo kwenye mahakama ya Tanzania ambayo,siyo tu kwamba yanakwamisha utawala wa sheria ndani ya nchi bali pia yanashusha heshima ya muhimili huu kwa umma,na kulifanya taifa kupoteza imani katika utendaji wake.

Nathubutu kusema kwa sasa Mhimili huu umebeba taswira kuwa umekuwa ni tawi la serkali,kwa kuwa karibia maamuzi yake yote yanakuja kwa kulinda na kuheshimu matakwa na maslahi ya serikali zaidi badala ya kulinda maslahi ya Taifa.

Hii ndio sababu watu wengi wanakimbilia kuishtaki Serikali ya Tanzania katika mahakama za kimataifa kama Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu(ACtHPR)na Mahakama ya Afrika Mashariki(EACJ)kwa kuwa ndio sehemu zilizobaki ili kulinda mstaqbali wa utawala wa kisheria kwa maslahi ya Taifa.

Kwa ripoti ya hivi karibuni,Tanzania ndio nchi inyoongeza kwa kushitakiwa kwenye Mahakama za kimataifa kwa nchi za Afrika Mashariki.Hii yote ni kutokana na ukweli kwamba watu wamepoteza imani na Mahakama za ndani,ndio maana wameamua kukimbilia kwenye mahakama za nje.

Naamini moja ya sababu ya udhaifu huu ni namana mahakama ya Tanazania ilivyiundwa kwa mujibu wa katiba ya sasa.Hii ikiwa ni pamoja na namna mchakato wa majaji wanavyopatikana,muingiliano mkubwa baina ya Mwanasheria Mkuu na Mahakama,Mamlaka makubwa aliyonayo Mwendesha Mashtaka Mkuu wa serikali kwa Mahakama na madaraka makubwa aliyonayo Rais ambayo yanamuwezesha kuingilia hata maamuzi na utaratibu wa kimahakama.

HITIMISHO

Ni matumaini yangu kwamba njia pekee ya kuondokana na tatizo hili ni kupitishwa kwa katiba mpya iliyopendekezwa.Hii itakuwa ni moja ya njia sahihi katika kuziba udhaifu huu mkubwa uliojitokeza katika utawala wa kisheria kwa Taifa letu.

Ni katiba hii itakayoweza kuiweka Mahakama ya Tanzania kuwa huru katika kutekeleza majukumu yake bila kuwa na ushawishi wa aina yeyote kutoka serikalini.

Ni katiba hii hii itakayoweza kupunguza ushawishi mkubwa wa watendaji wa serikali na nguvu kubwa ya Rais kuweza kuingilia mambo ya kimahakama.

Kuwa na Mahakama yenye nguvu itakayoweza kumuwajibisha yeyote yule anapofanya kosa ni matumaini ya Watanzania wote katika kulinda maslahi ya Taifa.

Ni matumaini yetu kuona tunapata mahakama yenye nguvu kama walionayo majirani zetu Kenya.Mahakama ambayo inakuwa na uwezo wa kutengua hata matokeo ya uchaguzi wa Rais katika kulinda maslahi ya Taifa.Mahakama ambayo ina uwezo hata wa kubatilisha sheria iliyopitishwa na bunge yenye lengo la kuvuruga maslahi ya Taifa.

Nitoe wito kwa watanzania wote kuungana katika mchakato wa kupigania katiba mpya kwa kuwa ndio suluhisho la mapungufu mengi tunayoyaona katika mfumo mzima wa uendehaji wa nchi yetu.​
 
Upvote 2
Nimekusoma na umeongea ukweli mtupu, judiciary kazi yao kubwa ni kutafsiri sheria baada ya kutungwa na Bunge, na wakati mwingine judiciary inaweza ikasimamisha matumizi ya sheria iliyotungwa kama haikutungwa vema, siku ambayo judiciary itaanza kujitegemea na kuachana kuwa tawi la magogoni, ndio siku nchi hii tutaishi kwa haki, elewa Amani ni lazima iandamane na haki, hawa majaji wetu ni njaa,ubinafsi, ulafi ndio unawasumbua,why president wa nchi ndiye awateue, why wasiombe kuwa Judge?,ila mabadiliko ya kweli yanaletwa na street battles sio humu kwenye soft landing
 
Back
Top Bottom