Herbalist Dr MziziMkavu
JF-Expert Member
- Feb 3, 2009
- 42,872
- 34,363
Maoni ya Katuni
Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) juzi imetangaza matokeo ya mitihani ya darasa la saba kwa watahiniwa waliomaliza elimu ya msingi mwaka huu, mtihani ambao kwa mara ya kwanza nchini ulisahihishwa kwa teknolojia mpya ya kompyuta OMR.
Matokeo hayo, yanaonesha wanafunzi waliofaulu ni 427,609 kati ya 844,938 waliofanya mtihani huo, ambapo ongezeko la ufaulu ni asilimia 19 ikilinganishwa na ufaulu wa mwaka 2012 ambapo ufaulu ulikuwa asilimia 30.6.
Akitangaza matokeo hayo, Katibu Mkuu (TAMISEMI), Bw. Jumanne Sagini alisema alama ya juu ya ufaulu kwa wavulana ilikuwa 244, wasichana ikawa 241 kati ya alama 250, tofauti na mwaka jana ambapo alama ya juu ilikuwa 237.
Aliongeza kuwa wavulana 218,093 pamoja na wasichana 209,516 walifaulu kwa kupata alama A-C, kati ya wanafunzi 844,938 waliofanya mtihani huo Septemba mwaka huu.
Bw. Sagini aliongeza kuwa kutokana na ongezeko la fursa ya kutoa elimu ya sekondari nchini, wanafunzi 411,127 kati ya 427,609 waliofaulu mtihani huo, wamechaguliwa kuijiunga na kidato cha kwanza katika shule za Serikali kwa awamu ya kwanza. Alisema takwimu hizo zinaonesha idadi ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2014 imeongezeka kwa asilimia 31.37.
Kwanza tunapongeza jitihada ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa kuratibu vizuri elimu ya msingi hadi ikafikia kupatikana matokeo hayo ambayo yanaonesha mabadiliko ikilinganisha na matokeo ya miaka ya nyuma.
Inawezekana kumefanyika marekebisho katika maandalizi ya ufahamu kwa wanafunzi mwaka huu, jambo ambalo linatakiwa litiliwe mkazo zaidi kwa ajili ya kupatikana matokeo bora zaidi.
Maandalizi mazuri ya wanafunzi wa shule za msingi ndiyo mhimili mkubwa wa matokeo mazuri ya elimu baadaye nchini, kama maandalizi ya elimu katika ngazi ya msingi yakiwa mabovu, taifa linaweza kuishia na 'wasomi' mbumbumbu katika ngazi za elimu ya juu.
Tumeshuhudia taarifa za miaka miwili iliyopita kuwapo kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza ambao walikuwa hawawezi kusoma wala kuandika, ilishangaza sana na haikufahamika wanafunzi hao walifauluje mitihani yao ya darasa la saba kama hawakujua kusoma wala kuandika, na mbaya zaidi haikueleweka nia ya kuwafikisha kidato cha kwanza wanafunzi wa aina hiyo.
Tunaamini kuwa elimu ya msingi nchini inapewa kipaumbele zaidi na hata serikali ikalazimika kuongeza nafasi za elimu ya sekondari kwa kujenga shule zaidi katika ngazi ya Kata, nia ikiwa kila mwanafunzi anayefaulu apate fursa ya kujiunga na masomo ya sekondari.
Kuimarika kwa elimu ya msingi kuende sambamba na uimarishwaji wa shule za sekondari, na hasa sekondari za Kata ambako ndiko vijana wengi wanakopata fursa ya kuendelea na elimu ya sekondari.
Ingawa bado yapo matatizo ya walimu, madarasa, maabara pamoja na miundombinu mingine ya kuziimarisha shule za sekondari zinazoendelea kujengwa nchini kote.
Katika hatua nyingine, Bw. Sagini alisema kuanzia sasa, mtoto yeyote atakayefika darasa la tatu kama atakuwa hana sifa za kuingia darasa la nne, atalazimika kurudia darasa, hatua hiyo inafuatia kuwepo kwa idadi kubwa ya wanafunzi wanaomaliza darasa la saba wakiwa hawajui kusoma, kuandika na kuhesabu.
Taasisi isiyo ya kiserikali ya Uwezo Tanzania (TWAWEZA) hivi karibuni ilitoa taarifa za tafiti ilizozifanya na kuonyesha asilimia 24 ya wanafunzi wa darasa la saba hawana uwezo wa kusoma hadithi rahisi ya mwanafunzi wa darasa la pili iliyoandikwa kwa lugha ya Kiswahili.
Utafiti huo pia ulibaini kuwa asilimia 50 ya wanafunzi hao hawawezi kusoma hadithi ya Kiingereza ya darasa la pili na asilimia 11 hawawezi kufanya hesabu rahisi za darasa la pili.
Hizo zote ni moja ya harakati za kuonesha kuwa zipo changamoto lukuki zinazotakiwa kufanyika ili kurejesha kiwango cha elimu ya msingi, matarajio yawe wanafunzi wanaohitimu elimu hiyo wafanane na jitihada za walimu wao za kuwaandaa kwa miaka yote saba.
Ni imani yetu kuwa matokeo ya mwaka huu, yatazidisha juhudi za walimu pamoja na wanafunzi ili idadi ya ufaulu iongezeke maradufu kwa mwaka 2014.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI