Ugaidi Dar-es-Salaam..Ina matumaini ya kudumisha usalama

Ugaidi Dar-es-Salaam..Ina matumaini ya kudumisha usalama

Kabaridi

JF-Expert Member
Joined
Nov 15, 2011
Posts
2,022
Reaction score
534
TATIZO la kwanza dhidi ya amani ya nchi kwa sasa limetajwa kuwa ni uongozi dhaifu, ambao umekuwa ukisababisha kusuasua katika usimamizi wa haki wa sheria za nchi na kuibua ombwe kubwa la kiutawala na kisiasa.
Uongozi huo dhaifu ni tishio kubwa zaidi kwa amani ya nchi kwa sasa, kuliko wakati mwingine wowote na wito ukitolewa kila kona ya nchi kutaka udhaifu huo uepukwe na mkazo uelekezwe katika umadhubuti wa kusimamia sheria.


Kati ya viongozi wenye kutoa wito huo ni pamoja na viongozi wa dini nchini, ambao licha ya kukiri kuwapo kwa uongozi dhaifu ambao kwa sehemu kubwa umekuwa ukichangia matukio ya uvunjifu wa amani na kuzua hofu miongoni mwa wanajamii, wanapendekeza suluhisho la hali hiyo huku Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Uhusiano na Uratibu, Stephen Wasira akikiri ya kuwa katika nyakati fulani serikali haikuweza kuchukua hatua kwa haraka, lakini akisisitiza haikuwa usingizini bali ilikuwa macho muda wote.


Katika kuzungumzia tishio la amani nchini ambalo msingi wake, pamoja na mambo mengine ni uongozi dhaifu, Sheikh wa Baraza la Kitaifa la Waislamu Tanzania (Bakwata) Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaad Musa, anasema kwa matukio yaliyojitokeza nchini hakuna maneno mengine ya kutumia zaidi ya kueleza kuwa kuna udhaifu wa kiuongozi nchini kwa sababu licha ya kuwapo kwa viashiria vyote vya uchochezi na upandikazaji chuki, hakuna kilichokuwa kikifanyika kwa upande wa serikali hadi pale maafa yalipojitokeza.
"Matukio haya ya vurugu ni matendo yasiyokubalika hata kidogo, ni matukio ya kupingwa kwa nguvu zote lakini msingi wake ni kushindwa kuchukuliwa mapema kwa hatua za udhibiti. Kumekuwa na uenezaji chuki kupitia kanda za video na mahubiri. Kila upande (kidini) ni kama sasa unaelekea kukosa imani na upande mwingine.


"Lakini naamini matatizo haya yanaweza kutatuliwa na viongozi wa dini na si serikali pekee. Viongozi tukae na kuzungumza masuala haya lakini ukitazama hata hili suala la kukaa pamoja kujadiliana kati ya viongozi wa dini halifanyiki vizuri, linakwenda kwa kusuasua.
"Nadhani serikali za mikoa pia ziwezeshe viongozi wa dini kuketi pamoja kuzungumzia tofauti zinazojitokeza kati ya wanajamii kupitia dini zao. Lakini kwa kweli haya matukio msingi wake ni ama udhaifu katika uongozi au ni mambo ya makusudi yenye kunufaisha baadhi ya watu.


"Ushauri wangu ni kwamba amani iliyopo ni lazima sasa iwekewe mikakati, tusilinde amani yetu kwa ujanja ujanja tu," anasema Sheikh Alhaad Musa.
Lakini kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo cha Mtakatifu Augustine (SAUT), Padri Dk. Charles Kitima, anasema hali inayoanza kujitokeza nchini dhidi ya umoja wa kitaifa inatokana na kukosekana kwa itikadi ya taifa inayounganisha Watanzania.
Kwa mujibu wa Dk. Kitima, kukosekana kwa itikadi ya pamoja inayounganisha taifa kunatokana na ombwe la kisiasa lililopo nchini kwa sasa ambalo nalo limezaa ombwe la kimaadili linalotumiwa na magaidi wa nje kuvuruga amani ya Tanzania.


Dk. Kitima anasema; "Sura lililokuja nayo hili tatizo (shambulizi la bomu Kanisa Katoliki Olasit jijini Arusha) linaonyesha walengwa ni Wakristo, na kundi linalowalenga linatumia mbinu za kigaidi, hatuwezi kusema wametumwa na dini fulani lakini kanda za uchochezi, mauaji ya Padri Zanzibar (Padri Evaristus Mushi) vyote hivi vinaonyesha kuna mkono wa watu wa nje ya nchi. Je, serikali iko wapi kuwadhibiti hawa?"


Alisema si jadi ya Watanzania kupigana na kuumizana kwa sababu ya dini zao, bali udhaifu wa serikali katika kudhibiti watu wa nje wanaokuja kwa uchochezi na kuwagawa Watanzania ndiyo umekuwa chanzo cha matatizo haya.
Alitoa mfano kuwa miaka ya 1960 wako baadhi ya Wamissionari walikuwa wanarudishwa makwao (nchi wanakotoka) kwa sababu walikuwa wakihubiri ubepari na kupuuza ujamaa. Kwa kuwa ujamaa ndiyo ilikuwa sera ya nchi kila aliyepinga alitambulika kuwa adui wa taifa na hakupewa nafasi, alichukuliwa hatua mara moja.


"Serikali na vyombo vyake havijaenda kwa kina kuchunguza wageni wanaoshirikiana na viongozi wa dini zote Kikristo na Kiislamu wanakuja kwa malengo gani na wanafanya nini, Wanatakiwa wachunguze ndiyo kazi yao. Serikali ina wajibu wa kuwalinda raia wake, jukumu la ulinzi wa raia haliwezi kuwa la kila watu kujilinda," alisisitiza.
Katika hatua nyingine Dk. Kitima, mwanazuoni mwenye misimamo mikali kwenye masuala ya kitaifa, alipinga mbinu ya serikali ya kuwakutanisha viongozi wa dini za Kiislamu na Kikristo akisema mbinu hiyo ni sawa na mkakati wa kulea tatizo kwa kuwa viongozi hao wala waumini wao hawajagombana na wanaishi maisha ya kawaida mitaani.


Badala yake, alishauri serikali itimize wajibu wake wa kuwasaka wahalifu na wachochezi na bila huruma, washughulikiwe kwa mujibu wa sheria au taratibu nyingine za kiutawala.
"Hii ya kutukutanisha viongozi wa dini kujadiliana tofauti zetu haitasaidia, huku ni kutaka kulikwepa tatizo. Maaskofu na masheikh wetu hawajawatuma hawa (wafanya fujo na uchochezi), sasa kukaa kujadiliana tofauti zetu wakati wahalifu hata hawahusiani nasi ni hatua ya kutaka kuwagawa na kuwagonganisha waumini wetu ambao wanaishi kwa kushirikiana. Vyombo vya dola vichukue hatua kuwasaka wanaofanya vitendo hivi vya kigaidi tangu mwanzo na waadhibiwe kwa mujibu wa sheria," anasema.


Mbali na hayo, Dk. Kitima anaionya serikali kutopuuza taarifa za kushughulikia vikundi vya kigaidi kwa kuwa historia imejaa ushahidi wa jinsi vinavyoweza kusababisha matatizo makubwa. Akatoa mfano wa kikundi cha kidini cha Boko Haram cha nchini Nigeria ambacho kilianza taratibu na sasa kina jeshi na kinaendesha matukio ya kigaidi nchini humo.


Alisema serikali ni lazima kudhibiti kila dalili za ugaidi, ikiwamo kutopuuza taarifa za makundi ya watu wanaofanya uchochezi wa kidini, taarifa za kuwapo kwa vyuo vinavyofadhiliwa na watu wa nje kufanya mafunzo yasiyoeleweka na hata baadhi ya nyumba za ibada zinazotumika kwa ajili ya mazoezi ya kujihami.


Lakini kwa upande wake, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine - Kampasi ya Mtwara, Padri Dk. Aidan Msafiri, anazungumzia hali ya upandikazaji wa chuki za kidini nchini akisema; "Kuna tatizo la Waislamu wenye msimamo mkali hapa nchini ambao nadhani ni tatizo si tu kwa watu wa dini isiyokuwa yao, bali hata kwa dini yao wenyewe inayopakwa matope kwa kuhusishwa na matendo maovu yanayotokea katika baadhi ya nchi na kusababisha vifo.
"Sasa ni lazima tuilinde hii tunu ya amani iliyopo kwa muda mrefu nchini wakati wote. Kuna makundi ya kidini yenye msimamo mkali ambayo yamekuwa na mtandao wa kimataifa. Tusipochukua hatua za umakini, matukio makubwa zaidi yenye maafa yanaweza kutokea hapa nchini.
Alipoulizwa kuhusu suluhisho anasema; "Nadhani kati ya hatua za kudumu katika kufuta chuki hizi za kidini ni watoto wa dini zote wafundishwe kupendana, kuanzia shule za awali, tuandikishe watoto wa dini zote katika shule zetu wafundishwe kupendana, isiwe watoto wa dini moja pekee katika darasa ama shule husika. Kuna kuzembea zaidi katika kusimamia amani ya nchi katika awamu hii ya nne.
Kauli ya Waziri Wasira
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Uhusiano na Uratibu, Stephen Wasira anazungumzia kuhusu shutuma za udhaifu wa uongozi akisema ni kweli kuna wakati hatua zimechelewa kuchukuliwa dhidi ya viashiria vya uvunjifu wa amani lakini si kwamba serikali ilikuwa katika usingizi bali ilikuwa macho.


"Ni kweli kuna hali ya kuchelewa kuchukua hatua imejitokeza nyakati fulani katika masuala haya ya midhahara na baadhi ya mambo mengine lakini si kweli serikali ilikuwa imesinzia. Na kwa kweli tunawasikia viongozi wetu wa dini, hatuwapuuzi na tunachukua mawazo yao kwa sababu mbali na ukweli kwamba wao ni viongozi wa dini, lakini pia ni raia wenzetu,"


"Serikali tumeshasema tumepiga marufuku mihadhara ya kidini na mengine ya uchochezi, lakini mwenye kusikia kama jambo hili la kueneza chuki linafanyika popote nchini atupe taarifa na ushahidi nasi tutachukua hatua haraka.


"Lakini nimewaeleza viongozi wa dini katika moja ya vikao vya hivi karibuni kwamba tusikubali wanasiasa wakaigawa nchi katika harakati zao za kutafuta uongozi. Mwalimu Nyerere aliwahi kusema katika hotuba yake mwaka 1995, anayeomba uongozi akiwa Mwislamu au Mkristo ajue hatachaguliwa kwa sababu ya uislamu au ukristo wake. Hii nchi zaidi ya asilimia 75 ya watu nchini ni wa dini hizi mbili, sasa huwezi kupata uongozi kwa kutumia dini moja," anasema Wasira.


Maoni hayo pamoja na kauli ya Wasira yanakuja katika wakati ambao tayari viongozi wengine mbalimbali wa dini nchini wakiwa wamekwishatoa misimamo kuhusu tukio la shambulizi la bomu katika Kanisa Katoliki la Olasit, jijini Arusha na matukio mengine dhidi ya viongozi wa dini kabla ya tukio la Arusha.


Viongozi hao ni pamoja na Rais wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa aliyetoa wito kwa serikali kukomesha mpasuko wa kidini unaolitafuna taifa.


Askofu huyo anasema kwa miongo mitatu sasa, serikali imekaa kimya, ikishuhudia mafundisho na mihadhara ya kidini inayochochea na kuhamasisha uhasama kati ya Ukristo na Uislamu, bila kuchukua hatua kukomesha hali hiyo.


"Matukio mbalimbali yanayoashiria uhasama wa kidini yanayotokea nchini. Kuna mihadhara, CD, DVD, machapisho na mafundisho yanayotishia maisha na usalama wa viongozi wa kanisa na waumini wao, ambayo yamefuatiwa na uchomomaji wa makanisa," anasema Askofu Ngalalekumtwa.


Kwa upande wake, Mkuu wa Kanisa la KKKT, Askofu Dk Alex Malasusa anasema anatoa wito akisema wote wenye jukumu la kulinda na kuitunza amani watimize wajibu wao huo bila woga.


Naye Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo anasema ni busara kushinda uovu kwa wema.


Lakini Romanus Ndunduma, kutoka Shirika la Wabenedictine Abasia ya Ndanda, mkoani Mtwara anasisitiza serikali kuchukua hatua dhidi ya chuki za kidini bila kuhofia kile kinachodhaniwa kuwa mustakabali mbaya wa kisiasa dhidi ya baadhi ya viongozi wa serikali.
 
1735580502564.jpg

In formers ++ SS msilale.
 
Back
Top Bottom