SoC02 Uhuru ndio njia ya kukuza Ajira na Uchumi

SoC02 Uhuru ndio njia ya kukuza Ajira na Uchumi

Stories of Change - 2022 Competition

Sister Abigail

JF-Expert Member
Joined
Sep 2, 2020
Posts
2,886
Reaction score
9,088
Takwimu za Benki ya Dunia za 2019 zimeonesha wakulima katika nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara ni 53%. Ikimaanisha kuwa Zaidi ya nusu ya watu wan chi za kusini mwa jangwa la sahara hujihusisha na kilimo, ambacho kiuchumi kinajulikana kama sekta msingi ‘Primary Sector’. Nchi ambazo watu wake wengi ni wakulima ni Burundi na Somalia ambazo zina wakulima 84% na 80% mtawalia.

Mbali na nchi za Afrika kuwa na watu wengi kwenye kilimo, bado hali imekuwa tete kwa kipindi hiki ambacho Urusi inapigana na Ukraine tangu Februari 2022 ambapo ngano imepanda bei maradufu kutokana na nchi hizo kuwa wazalishaji wakubwa wa ngano na nchi za Afrika kuwa ni nchi zinazopokea ngano kutoka katika nchi hizo. Jambo la kushangaza Urusi na Ukraine zina asilimia ndogo sana ya wananchi wake wanaojihusisha na kilimo. Ambapo 6% ya watu wa Urusi wanajihusisha na kilimo na 14% ya wa-Ukraine wanajihusisha na kilimo kwa takwimu za 2019 zilizotolewa na Benki ya Dunia.

Nchi ya kusini mwa Jangwa la Sahara ambayo iko vizuri kiuchumi ni Afrika ya Kusini ambayo 5% ya watu wake wanajihusisha na kilimo.

Picha inayoweza kuonekana kwa uwazi kabisa katika takwimu hizo ni kuwa kadiri watu wanavyojihusisha na Sekta Msingi ‘Primary Sector’ nafasi za uzalishaji wenye tija unakuwa chini na hivyo ajira kuwa adimu. Wazo hili liko sambamba na mawazo ya wachumi ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikosoa nchi kujikita katika sekta msingi. Hata kwa takwimu za uhamiaji, vijana wamekuwa wakikimbilia katika maeneo ambayo wananchi wake hawajihusishi sana na kilimo. Kwa watu wa kusini mwa Jangwa la Sahara wengi hukimbilia Afrika Kusini.

JE, KILIMO NI SULUHU AU NI KUZIDISHA UMASIKINI?
Mbali na kilimo kutoonesha mwanga wa kuongeza ajira katika nchi zinazoendelea bado wanasiasa wamekuwa wakiweka msisitizo wa vijana wake kujihusisha na kilimo ili ‘Kujiajiri’ badala ya kusubiri kuajiriwa. Ni kweli kwamba mtu anayelima anaweza kuhesabiwa amejiajiri kitakwimu na kuonesha kuwa 'Unemployment rate’ imepungua hata hiyo haiwezi kuleta picha halisi kwa kuwa vijana hao wataonekana wamejiajiri huku kilimo husika kikiwa hakiwaondoi kwenye wimbi la umasikini Zaidi ni kuwafanya waishi katika Uchumi Tumbo ‘subsistence Economy’.

Kinachoonekana ni kuwa vijana wanatakiwa waonekane wanafanyakazi ili wahesabiwe wamejiajiri bila kuangalia uhalisia wa kitu gani vijana wanakipata kwenye kilimo husika. Kimsingi kwenye Uchumi wa Kilimo ‘Agricultural Economics’ kuna tofauti kubwa ya ‘Peasants’ na ‘Farmers’ kumwambia kijana aende kulima ni kuhamasisha kuwa Peasant kitu ambacho ni alama ya umasikini, na ndio sababu nchi zote zenye asilimia kubwa ya wananchi wake kama wakulima ni nchi masikini kuliko nchi ambazo zina watu wachache kama wakulima.

Ajira zinapaswa kuangaliwa kwa namna pana. Ajira ni tofauti sana na shughuli. Vijana wanaofanya kilimo Tanzania nan chi nyingine zenye watu wengi kama wakulima, kiuhalisia watu hao wanakuwa wanafanya ‘Shuguli’ lakini sio ‘Ajira’ kwa kuwa hata kinachopatikana na shughuli hizo hakiwezi kuwalinda walau kwa misimu miwili ya bila kazi. Hii ndio sababu vijana wanaojihusisha na kilimo hulazimika kukimbilia shughuli nyingine baada ya msimu wa kilimo kuisha. Ili kupata fedha ya kuwavusha kwenye kipindi hicho ambacho hawana shughuli.

Hivyo basi, kuhesabu kilimo kuwa ni ajira/kujiajiri ni suala lisilozingatia maana halisi ya ajira, ambapo kimsingi wanajiohusisha na kilimo ni watu wanashughulika tu na hawana ajira, na wala hawawezi kufananisha na watu walioko kwenye sekta nyingine.

AJIRA ZITATOKA KWENYE UHURU
Mchumi nguli ambaye ameshinda hadi tuzo ya Nobel, Amartya Sen, alitafsiri maendeleo kama kuongeza uhuru wa mtu mmoja mmoja. Na alionesha ni kwa namna gani kuongeza uhuru wa watu kunakuza pato la taifa na kuleta maendeleo na ajira. Nchi za Afrika, zinaongoza kwa kuminya uhuru kwa kuwa na sheria kandamizi ambazo zinazuia kwa kiasi kikubwa kwa nguvu kazi kushiriki katika fursa mbali mbali za kujipatia kipato ndani nan je ya mipaka ya nchi.

Kwa sasa dunia inaingia kwenye uchumi wa kidigitali kama ambavyo mchumi David O’Connor ameonesha kwa kusema kuwa taasisi za kidigitali ndizo zinazopanda kwa kasi kuliko kampuni nyingine akitolea mfano wa Facebook na Google. Hata hivyo nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara zimekuwa na sheria kandamizi dhidi ya mambo ya digitali hali inayofanya vijana washindwe kujiajiri katika sekta hiyo ambayo haihitaji vitu vingi.

Umoja wa Mataifa unatambua Internet Access kama haki za binadamu lakini nchi kadhaa za Afrika zimekuwa zikizuia upatikanaji wa mtandao kutokana na matukio tofauti tofauti nchi nyingi zikisema ni kwa ‘Maslahi mapana ya taifa’. Nchi ambayo imezuia internet hivi karibuni ni Uganda ambayo ilizuia mtandao wake katika kipindi cha uchaguzi mkuu Januari 2021. Tanzania kulikuwa na shida ya mtandao kipindi cha Uchaguzi Mkuu 2020. Nchi nyingine zenye kuzuia mtandao ni Zimbabwe, Togo, Burundi, Chad, Mali na Guinea ambazo zilifanya hivyo mwaka 2020.

Suala la mtandao limewapa watu wengi ajira zinazowafanya watimize malengo yao kwa shughuli kama za Kufanya Taxi za mtandaoni kama Uber, Bolt nk, utengenezaji na uuzaji wa maudhui kwa bloggers na Vloggers. Hata hivyo hawa wote wanaguswa na sheria kandamizi kama Sheria ya Makosa ya Mtandao, Sheria ya Takwimu na Sheria ya Mawasiliano ya kielectroniki na Posta(EPOCA) ambazo zote zinafinya uhuru na kuzuia matumizi ya fursa zilizopo katika sekta hiyo.

Suala linguine linalosababisha ufinyaji wa mazingira ya kujiajiri ni unyanyasaji wa kijinsia ambao haujatungiwa sera hadi sasa. Kazi kama za mama n’tilie, kazi za baa zinaonekana ni kazi za watu waliokata tamaa ilhali ni kazi inayoweza kufanywa hata na muhitimu kama ilivyo katika nchi zilizoendelea. Lakini wanaofanya kazi hizo hufanyiwa matendo ya kinyanyasaji ikiwemo kushikwa shikwa bila ridhaa kuonekana makahaba hali inayofanya watu wengine ambao wangeweza kufanya kazi hizo kuogopa kuingia kwenye kazi hizo na kurundikana kwenye sekta msingi.

UTATUZI
Ni muhimu kwa Serikali kuondoa Sheria zote kandamizi na zinazominya uhuru wa watu kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi. Kuwa na sera ya kitaifa ya Jinsia ili kufanya kila kazi kuwa ‘Profession’. Aidha ni muhimu kuondoa sheria mbovu kama zile zinazowatia hatiani wasio na makazi na maskini kwa jina la uzururaji kama ilivyo katika kifungu cha 176 na 177 cha Sheria ya Makosa ya Jinai

Wasalaam,
Abigail Nabal

IKIWA UNEPENDEZWA NA MAONI YANGU,TAFADHALI NAOMBA KURA YAKO.ASANTE.
 
Upvote 1
Back
Top Bottom