Akilimtindi,
Nadhani uhuru haukutolewa na "yeye mwenyewe" kama ulivyosema. Uhuru tunaotumia unatolewa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano, Toleo la 2005.Turejee Ibara ya 18 ya Katiba, na nina nukuu " kila mtu a) anao uhuru wa kuwa na maoni na kueleza fikra zake,
b) anayo hki ya kutafuta, kupokea na kutoa habari bila ya kujali mipaka
ya nchi
c) Anayo uhuru wa kufanya mawasiliano na haki ya kutoingiliwa katika
mawasiliano yake,
d) anayo haki ya kupewa taarifa wakati wowote kuhusu matukio
mbalimbali muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na pia masuala
muhimu kwa jamii.
Hakuna atakayetueleza kuwa ufisadi huu mkubwa si jambo au tukio muhimu kwa maisha ya Watanzania. Serikali kama haitaki kuchokonolewa ilikuwa na wajibu wa kutoa "taarifa sahihi" kwa mujibu wa Katiba, na kwa kuwa haikutoa "tukitafuta" tusilaumiwe. Ni haki yetu.
Isitoshe Ibara ya 20 inaenda mbele zaidi,
20(1) kila mtu anao uhuru wa kukutana na watu wengine kwa hiari yake na kwa amani, kuchanganyika, kushirikiana na watu wengine, na kwa ajili hiyo kutoa mawazo yake hadharani na ....kuendeleza imani au maslahi yake au maslahi mengineyo". Kama kwa kutoa mawazo yetu, na "kuwasema mafisadi..." anayedhani tumevunja Sheria ya nchi ajitokeze hadharani na aeleze ni sheria ipi ya Taifa hili tumevunja. Tatizo letu ni kukosa ushujaa na ujasiri katika kutetea haki, maslahi na rasilimali za Taifa letu, ambazo ninarudia tena, si za Rais, wala Serikali bali ni zetu, na Rais na Serikali tumewakabidhi kuzitunza tu kwa dhamana. Hivyo Akilimtindi, naungana nawe, lakini nadhani haki hiyo tusipewe na mtu, awe Rais, au nani bali tupewe na Katiba na sheria za nchi. anayesema kuwa tunachonganisha, tunachochoea naye awekwe kwenye mizani kupimwa anamtetea nani na kwa maslahi ya nani. Nikisema hivi, ni dhahiri ninapinga kabisa kuwasema tu watu, kuwaseng'enya, kuendekeza umbeya. Lakini tunapokuwa na tetesi, japo Dogo, Serikali inawajibika kutoa majibu sahihi kwa kuwa inavyombo vya uchunguzi, nyaraka zote ziko mikononi mwake. Isipotoa isitulaumu kuwa kuna uchochezi bali ijilaumu kwa kutotekeleza vizuri majukumu yake, tena ya Kikatiba. Wenye kujua haki zao, Katiba, na Sheria za nchi hawatatishwa hata kidogo, na Mhe. wa Awamu ya Tatu aling'anka na watu kufyata kwa vile tu vyombo vya Habari na Watanzania walivumilia wakiamini "usafi wake.." kumbe mambo tofauti. Tumeumwa na nyoka, hata jani tu latutisha sasa na hatutaachia kamwe. Tuungane, Tushikamane, Uhuru utarejea unakostahili, haki zitalindwa na Rasilimali zitalindwa. Kama tulipoibua tukaambiwa ni kelele za mlango na hazimzuii mwenye nyumba kulala, na leo yeye mwenyewe aliyetoa kauli hizo katamka hadharani, tena kupitia Bunge Tukufu kuwa ni kweli, na kuwa asilimia 75 zitarejeshwa na kuelekezwa kwa mkulima Tunataka nini zaidi, akiri au aombe msamaha vipi? Hii siyo kusema ninakubaliana na aliyosema, La hasha, amezua maswali mengi zaidi kuliko majibu. Tutaendelea hadi majibu yote yapatikane. Tuendelee na mshikano huo huo, hakuna mtu mmoja peke yake anaweza kushinda vita hivi! Kwa Pamoja ushindi uko dhahiri.