Herbalist Dr MziziMkavu
JF-Expert Member
- Feb 3, 2009
- 42,872
- 34,363
Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. David Mathayo.
Serikali ya Uingereza imetoa dola za Marekani milioni 13.4 kwa ajili utekelezaji wa mradi mkubwa wa kilimo nchini.
Serikali ya Uingereza imekabidhi fedha hizo kwa shirika lisilokuwa la kiserikali la BRAC-Tanzania, ambalo litasimamia utekelezaji wa mradi huo wa miaka 4, ambao umepewa jina la Lead.
Mradi huo uliozinduliwa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. David Mathayo, unatarajiwa kutekelezwa katika mikoa 18 nchini. Kwa kupitia mradi huu, tunaweza kuzalisha ajira nyingi sana kwa Watanzania, wakulima, wafanyabiashara na wafugaji, alisema Mathayo wakati wa uzinduzi huo.
Alisema mradi huo utaisaidia serikali ambayo inakabiliwa na uhaba wa fedha kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo ya kilimo ambao ni uti wa mgongo wa taifa.
Mradi huu unalenga kuongeza kipato kwa wakulima, kuwaongezea uwezo wakulima wadogo na kuongeza tija na ufanisi katika sekta nzima ya kilimo, pamoja na kuhakikisha usalama wa chakula. Mathayo alisema mradi utalenga maeneo mawili makuu, kilimo (hasa cha mahindi) na maendeleo ya mifugo.
Katika utekelezaji, alisema mradi utahusisha wakulima wa mifugo 48, 000 katika mikoa husika, na utasaidia kutoa ufumbuzi matatizo ya muda mrefu yanayowakabili wakulima na kuongeza uwezo wa kitaalamu, kuwasaidia kupata masoko ya mazao yao na mbegu bora na zenye viwango.
Balozi wa Uingereza nchini, Diane Melrose, amelielezea shirika la BRAC kama mfano wa kuigwa, hasa katika utekelezaji wa miradi inayowalenga watu maskini ulimwenguni.
Mwanzilishi na Mwenyekiti wa BRAC--International, Afazia Hasan Abed, alisema shirika lake limeshafanya maandalizi ya utekelezaji wa mradi huo, kutoa mafunzo kwa wataalam watakaosaidia wakulima, na kuwakusanya wakulima na wafugaji.
Ni matumaini yangu makubwa, mradi utasaidia wakulima na Tanzania kupiga hatua katika sekta ya kilimo alisema.
CHANZO: NIPASHE