SoC02 Ujasiriamali wa Kidigitali

SoC02 Ujasiriamali wa Kidigitali

Stories of Change - 2022 Competition

SimonSwale

New Member
Joined
Jul 22, 2022
Posts
2
Reaction score
2
UJASIRIAMALI WA KIDIGITALI

Watu wengi wamekuwa wakielewa Ujasiriamali kwa maana isiyo pana. Wapo wanaodhani Ujasiriamali ni kufanya biashara ndogondogo kama kuuza karanga, mikoba, vyakula, viatu au nguo. Lakini wengine hudhani Ujasiriamali ni ujuzi wa kutengeneza vitu au bidhaa kama batiki, sabuni, karanga za mayai au kulima uyoga.Ujasiriamali ni zaidi ya kufanya biashara ndogondogo. Ni zaidi ya ujuzi wa kutengeneza vitu au bidhaa.

Kwa maana pana, Ujasiriamali ni uwezo wa akili na ubunifu wa mtu kutambua fursa, kuiendea fursa, kuipangia mkakati fursa na hatimaye kuthubutu na kuiweka katika uhalisia, yaani kudhalisha bidhaa au huduma yenyewe na mwisho kabisa kuitafutia soko na kuifanya itambulike na watumiaji. Kwa ufupi, Ujasiriamali ni uthubutu na ubunifu wa kutafuta na kupata mali. Hivyo basi, popote pale penye Fursa unaweza kufanya Ujasiriamali.

Hivi sasa tunashuhudia mabadiliko makubwa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ulimwenguni. Fursa nyingi zimezalishwa na zitaendelea kuzalishwa kutokana na mabadiliko haya. Hii inapelekea kuzaliwa kwa 'Ujasiriamali wa Kidigitali' ambapo watu wanatumia fursa zinazotokana na mabadiliko ya TEHAMA kujitafutia kipato.

Zifuatazo ni baadhi Fursa za Ujasiriamali zilizojitokeza kutokana na maendeleo ya TEHAMA:

1.Ubunifu wa Tovuti (Web Designing): Tovuti (websites) hutumiwa na mtu, shirika au asasi kwa kazi mbalimbali kama kuelimisha jamii, kutangaza bidhaa au huduma, kuelezea shughuli za taasisi au kama jukwaa la kuombea kazi na kutuma maoni.Ili kuweza kuwa mbunifu wa Tovuti mzuri inabidi ujifunze lugha za kuprogramu kama HTML,CSS na Javascript lakini pia uweze kutumia programu kama Adobe Dreamweaver.

Ubunifu wa Tovuti ni miongoni mwa ujuzi unaolipa. Kutengeneza Tovuti moja si chini ya Sh.500,000/= kwa mteja wa kawaida na bei inapanda kutegemea na mahitaji yanayotakiwa kuwekwa kwenye Tovuti na hadhi ya kampuni inayotaka Tovuti. Kazi hii haichoshi na inakuruhusu kufanya mambo mengine.

2.Uhandisi wa programu (software engineering): Wahandisi wa programu hutengeneza hujaribisha na kuendeleza mifumo/programu za kompyuta (softwares). Wataalamu hawa hutumia lugha za kuprogramu kama vile python, C au Java. Ujuzi huu unaweza kuwa mgumu kuupata kwani unahitaji utoe muda wa kutosha kujifunza lugha za kuprogramu, kuzizoea na kuanza kutumia, lakini ni miongoni mwa ujuzi unaolipa zaidi duniani. Katika orodha ya watu 10 matajiri zaidi duniani, zaidi ya watu 7 ni wahandisi wa programu (Bill Gates,Elon Musk, Larry Page,Larry Ellison na wengineo).

3.Ubunifu wa Michoro (Graphics Designing): Wabunifu wa Michoro hutengeneza dhana za kuona kama vile nembo, mabango au vipeperushi ambazo hutumika katika utangazaji wa masoko (marketing), kampeni fulani kama uchaguzi au hata ufungaji wa bidhaa (packaging).

Ujuzi huu huchukua miezi 2 au zaidi kuupata kwa kusoma kozi maalumu, kujisomea mwenyewe au kukaa karibu na Wabunifu wa Michoro. Unaweza kujipatia kipato kwa njia rahisi kutokana na Ari yako ya kazi. Mfano, kwa kawaida bango dogo (poster) moja unaweza kuuza kwa Sh.20,000/= au zaidi na bango kubwa (flyers) ni zaidi ya laki 5.

4.Upigaji picha (Photography): Inaaminika picha ya kwanza ilipigwa mwaka 1826 huko Ufaransa. Hadi hivi leo picha hupigwa kila siku na binadamu. Pamoja na ongezeko la simu janja (smartphones) kufanya kila mtu kuweza kupiga picha lakini bado utaalamu wa picha unahitajika ili kutoa picha zinazoendana na hitaji husika.

Picha mara nyingi hutumika kwa kumbukumbu ya tukio husika lakini pia hutumika katika masuala ya urembo, uwasilishaji wa mada au kama burudani tu. Upigaji picha ni miongoni mwa ujuzi unaolipa sana. Picha moja hivi sasa si chini ya Sh.3000/=. Kipato chako kitategemea na Ari yako ya kazi. Ujuzi huu huchukua mwezi 1 au zaidi kuupata kwa kujisomea mwenyewe au kukaa karibu na wanaofanya.

5.Uandishi wa Nakala (Copywriting): Mwandishi wa Nakala (Copywriter) ni mtu anayeandika ujumbe fulani kwa ajili ya matangazo (advertisements) au kutoa tamko kwa jamii. Uandishi waNakala ni miongoni mwa mkakati wa ukuzaji wa masoko unaotumika sana. Ujuzi huu si mgumukuupata, unatakiwa kuwa na ujuzi wa kuandika, kusoma na kuhariri maandiko vizuri pamoja nakuelewa aina mbalimbali za mikakati ya ukuzaji masoko.

Unaweza ukajifunza kwa njia ya mtandao au vitabu, vilevile kwa kufanya kazi pamoja na wahariri wa nakala. Clayton Makepeace anakadiriwa kuwa na utajiri wa dola za kimarekani zaidi ya bilioni 1.5 alizozipata kutokana naUandishi wa Nakala.

6.Uhariri wa Video (Video Editing): Wahariri wa video huunganisha vipande mbalimbali vya video ili kuleta mwendelezo unaotoa dhumuni fulani.Uhariri wa video unaweza kuwa mdogo kwa kuhariri video za kawaida za matangazo ya biashara na harusi au mkubwa zaidi hasa ule wa filamu. Ujuzi huu si mgumu kuupata, unaweza kujifunza mwenyewe kupitia vitabu na YouTube, kukaa karibu na wahariri wa video au kusomea chuoni kama kozi. Michael Kahn anatajwa kuwa ni mhariri wa video tajiri zaidi duniani akiwa na utajiri wa zaidi ya dola bilioni 5 za kimarekani kutokana na uhariri wa video.

Fursa nyingine za Ujasiriamali wa Kidigitali ni pamoja na Uandishi wa vitabu vya kielektroniki (ebooks), biashara ya mtandaoni (e-commerce), Balozi wa Chapa (Brand Ambassador) na msadizi wa mtandaoni (virtual assistant). Fursa hizi pamoja na nilizoelezea hapo juu unaweza kuzitumia kwa kuajiriwa na kampuni au kwa kujitegemea ( yaani freelancing) na kisha kutengeneza kampuni yako.

Naamini kuwa 'Matajiri na watu watakaofanikiwa sana katika kizazi kijacho ni wale watakaochukua nafasi ya kwenda sambamba na maendeleo ya TEHAMA hivi sasa'. TEHAMA itaendelea kuzalisha fursa nyingi za Kijasiriamali ambazo zitakufanya ujipatie kipato kikubwa kwa kazi zisizotumia nguvu bali akili nyingi. Amua hivi leo kuhamia kwenye Ujasiriamali wa Kidigitali. Anza kujifunza moja ya ujuzi nilioeleza hapo juu, anza kutafuta kazi na kuutumia,kupata kipato na endelea na ujuzi mwingine.



View attachment UJASIRIAMALI WA KIDIGITALI.pdf
 
Upvote 2
Back
Top Bottom