Sema Tanzania
JF-Expert Member
- May 18, 2016
- 251
- 466
Mara nyingi mafanikio ya mtu mzima ni zao la malezi bora ya utotoni, mazingira sanjari na jamii inayomzunguka. Endapo wazazi ama walezi watafanya jitihada za dhati za kumjenga na kumuandaa mtoto ili kusudi awe raia makini na anayejitambua basi mchango wa mtu huyu kwa maendeleo ya jamii utakuwa wa kipekee na wa aina yake.
Makala ya leo yanaangazia kujenga uelewa miongoni mwetu juu ya chimbuko la Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watoto (UNCRC) ambao nchi yetu pia iliridhia. Lengo ni kutekeleza yale yote yanayotuhusu kama wazazi ama walezi kwa vitendo. Tafadhali, soma makala haya kisha pata wasaa wa kumjuza na jirani yako. Awali ya yote, tuanzie na tafsiri ya neno ‘Mtoto’.
Mtoto ni mtu yeyote mwenye umri wa chini ya miaka kumi na nane (18). Hii ni tafsiri ya wazi iliyomegwa kama ilivyo kutoka kwenye Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watoto, Mkataba wa Afrika kuhusu Haki na Ustawi wa Mtoto, Sera ya Maendeleo ya Mtoto pamoja na Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009. Katika hali na namna yoyote ile, jamii haina budi kutambua kwamba, mtoto ni mtu kamili, si sehemu ya mtu mwingine.
Katika umri tajwa hapo juu, mtoto huhitaji malezi bora ili aweze kuishi vizuri, kushirikishwa, kulindwa na kuendelezwa kiakili kwa ajili ya maisha yake ya baadae pindi awapo mtu mzima. Pasi na kupepesa macho ama kuyumbisha kope, sote kwa pamoja sharti tujiulize swali hili la msingi: Je, haki za mtoto ni nini?
Haki za mtoto ni haki za binadamu zilizo katika muktadha wa uzingativu wa haki mahsusi za ulinzi na huduma zote wanazostahili watoto kote ulimwenguni. Ni stahili za msingi ambazo watoto huzaliwa nazo, hukua nazo, huwastawisha na kuwaendeleza. Watoto wana haki za kipekee kwa sababu ya umri wao mdogo na hali yao ya utegemezi ambayo inaweza kuwafanya wadhulumiwe na kutendewa vitendo vibaya. Watoto wote wana haki sawa bila kujali jinsia, rangi, kabila, dini, hadhi au hali ya afya.
Hebu tukurudishe katika historia japo kwa uchache. Hivi una habari kuwa fufutende la kudumisha haki za mtoto lilianza rasmi miaka ya 1940? Naam, ni katika kipindi ambacho Umoja wa Mataifa uliandaa Azimio rasmi la Kidunia juu ya Haki za Binadamu ambalo lilirasimishwa na kushika hatamu mnamo mwaka 1948. Azimio hili lilibeba tamko kuu linalohusu haki za watu wote ulimwenguni wakiwemo watoto.
Aidha, kukua kwa uelewa miongoni mwa jamii na ongezeko la mahitaji maalum ya watoto kulipelekea kuanzishwa kwa andiko rasmi la kimataifa juu ya haki za watoto. Ilipofika mwaka 1959, Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa ulianzisha azimio la pili lililohusu haki za mtoto lengo likiwa ni kuamsha nia juu ya masuala yanayowahusu watoto. Maandalizi ya Azimio ama Mkataba juu ya Haki za Watoto hayakuwa rahisi, yalichukua miaka mingi, muda na kutumia nguvu za ziada mwiongoni mwa waandaaji.
Ilipofika tarehe 20 Novemba 1989, serikali za mataifa yote ikiwemo Tanzania yaliwakilishwa kwenye Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mtaifa kuuridhia Mkataba juu ya Haki za Mtoto sanjari na utiaji saini. Tukio hilo ndilo lililouweka mkataba juu ya haki za mtoto kwenye sheria ya kimataifa na utekelezaji wake kuanza rasmi katika nchi zote zilizoliridhia.
Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watoto (UNCRC) unazitambua haki za watoto kwa marefu na mapana yake na katika nyanja zote zikamilishazo maisha. Aidha, nyanja za haki zote za mtoto zimewekwa kwenye makundi matatu (3) muhimu; nayo ni: kundi la haki ya kulindwa, kundi la haki ya kupatiwa mahitaji na kundi la haki ya kushirikishwa. Ndani ya makundi haya matatu, ndimo ambapo haki zote zinazowahusu watoto zimepata kujumuishwa.
Mkataba juu ya haki za mtoto umejikita katika misingi mikuu minne (4); ambayo ni: kuyaweka mbele maslahi ya mtoto, kukomesha ubaguzi, uzingativu wa maoni ya mtoto katika kufanya maamuzi juu ya masuala yanayomhusu, kukua, kuishi na kuendelezwa.
Mkataba wa Haki za Watoto (UNCRC) wa mwaka 1989 ndilo andiko la kwanza la kisheria na hutambulika kimataifa linalofafanua haki zote kwa ukamilifu wake na katika muktadha uliosheheni nyanja zote. Hili ndilo azimio kubwa zaidi lililoridhiwa na nchi nyingi zaidi ulimwenguni huku zikiweka dhamira ya kuzilinda haki za watoto pasi na kero.
Kudumisha haki za mtoto ni kujenga jamii na Taifa lenye raia wenye kuheshimiana, wenye uzalendo, fikra chanya, uendelevu, umoja na mshikamano lakini pia wenye ustaarabu wa kiwango cha juu. Watoto wakiheshimiwa wangali wadogo, hukua na kustawi vyema huku wakiifurahia dunia kwa kuiona kuwa ni mahali salama pa kuishi. Wakati wa kuunga mkono haki za watoto ni sasa, inaanza nasi, inaanza nawe. Tuwapende na kuwalinda, watoto ni tunu ya familia, jamii na taifa.
Watoto wamesimamia mustakabali wa maisha yao, kazi ya kuwaunga mkono ni yetu sote. Novemba 20 mwaka huu, Mkataba wa Haki za Watoto (UNCRC) umevaa sura mpya ya miaka 30 tangu kurasimishwa kwake. Je, utafanya nini kuhakikisha watoto wote wanapata haki sawa nchini Tanzania na duniani kote?
Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116 ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook, Instagram na JamiiForums: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org.