Katika mji wa Karamay mkoani Xinjiang Uighur, China kuna soko moja la usiku ambalo ni maarufu sana. Soko hili linajulikana kwa jina la 'Farasi Wanane'. Baada ya matembezi ya siku nzima wenyeji wetu walitupeleka ili nasi tujionee yanayojiri kwenye soko hilo.
Kawaida soko la 'Farasi Wanane' licha ya kuuza vyakula vya aina mbalimbali, kwa siku hiyo tulipofika tulikuta sherehe ya kuchoma ngamia. Kawaida sherehe hii inafanyika kwa kuchoma nyama ya ngamia kwenye tanuri, huku wasanii wakisindikiza shughuli hiyo ya kuchoma ngamia kwa dansi mbalimbali za kienyeji. Halafu nyama ya ngamia inatolewa kwenye tanuri taratibu, ambapo wapishi nguli wa mji huo, ambao kawaida huwa ni wazee wanaichukua nyama hiyo na kuiweka kwenye meza kubwa.
Kabla ya nyama hii kugawiwa kwa watu, wanatafutwa watu wawili watatu wanaojitolea kuonja. Baada ya shughuli ya kuonja kumalizika nyama inakatwa na kugawiwa kwa watu. Nyama hii inasindikizwa na chakula kitamu sana kiitwacho ‘chaofan’ ambayo ni pilau ya watu wa Xinjiang. Chakula hiki mimi huwa nakipenda sana.
Waswahili wanasema kazi na dawa, nasi tulibarizi na kutangamana vizuri na wenyeji wetu tukila vyakula vya aina mbalimbali pamoja na kudansi. Tukiwa kwenye pirika za kudansi, bahati nzuri nilikutana na mama mmoja aitwaye Nuerdong ambaye alivutiwa sana na uchezaji wangu kwenye dansi yao. Kusema kweli alifurahi sana kuona kwamba ninapocheza naipatia sana dansi hiyo. Baada ya kuongea naye mama huyu akanielezea kwamba yeye ni mkazi wa kituo cha kutunza wazee cha Haitangbieyuan kilichopo Wuerhe, na hapo akaamua kunialika nami niende kumtembelea kwenye makazi yao.
Kwa bahati nzuri katika ratiba yetu ya ziara pia tulipangiwa kutembelea kituo hicho, hivyo siku ya tatu tulifunga safari na kwenda kwenye makazi haya ambayo yalijengwa kutokana na mahitaji ya wanakijiji. Katika kituo cha Haitangbieyuan wapo wazee wenye umri wa miaka zaidi ya 60 ambao wanaweza kuishi hapa kwa
hiari yao bila ya kulipa kodi ya nyumba.
Kila yadi moja ambayo imepambwa vizuri kwa mimea na miti ya matunda iliyopandwa ndani, ina makazi matano. Licha ya hayo, kituo hicho pia kina zahanati moja na ukumbi kwa ajili ya wazee kujiburudisha. Bibi Nuerdong huja kwenye ukumbi huu kufurahia nyimbo na kucheza dansi. Na kwa kuwa mara hii alinialika nyumbani kwake, nikapata fursa tena ya kushiriki katika dansi yao.
Watu wa Xinjiang wanasifika sana kwa kuwa wakarimu. Hivyo kama kawaida ya wenyeji wa huko, nyumbani kwa bibi Nuerdong pia kuliandaliwa vyakula vya aina mbalimbali, yakiwemo matunda, nyama ya kondoo, chaofan (pilau) na vingine vingi. Nilipopata fursa ya kukaa chini na kuzungumza naye alieleza kwamba hivi sasa maisha yao yameboreka sana tangu kujengewa makazi hayo ya wazee. Anasema amehamishiwa kwenye makazi haya miaka minne iliyopita, na sasa anafurahi sana kwani ana nyumba kubwa na nzuri na kila wanachohitaji kipo karibu na makazi yao.
Wazee hawa wengi wao walikuwa wakijishughulisha na kilimo lakini makazi yao hayakuwa ya kuridhisha. Hata hivyo serikali ya mji wao ilibuni mradi wa kuwajengea makazi wazee hawa, huku ikiwapatia fursa ya kuendelea na shughuli zao za kilimo na wengine hata kupata kazi rasmi. Hivi sasa kwa ujumla maisha yao yamebadilika kabisa. Ni kweli, hata mimi nilipofika nilishangaa kwa furaha kuona wazee wanaenziwa namna hii, huku moyoni mwangu nikiwa natamani na wazee wa mahali pengine kote duniani wangekuwa wanatendewa kama hivi.
Muda wa kuondoka ulipofika, Bibi Nuerdong alisisitiza sana lazima atusindikize. Jambo hili lilinifanya nijisikie faraja kwa ukarimu na makaribisho makubwa aliyonionesha bibi huyu. Ni matarajio yangu kwamba furaha na uchangamfu alio nao bibi huyu utasambaa kwa wazee wengine wote.